27.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Michepuko kikwazo wanaume kupima Ukimwi

YOHANA PAUL-MWANZA

WAKATI vita dhidi ya mapambano ya ugonjwa wa Ukimwi ikipamba moto nchini, imebainika kuwa baadhi ya wanaume kuwa na uhusiano wa mapenzi na wanawake wengi ni moja ya sababu inayowafanya waogope kupima virusi vya Ukimwi.

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Nacopha), Leticia Kapela, alisema hayo jana, wakati wa maadhimisho ya kilele cha Siku ya ukimwi Duniani mkoani Mwanza.

Alisem kutokana na hali hiyo, wengi wao hujikuta wakisubiri wenzi wao wapime afya zao pindi wanapokuwa wajawazito, ambapo wakiona wako salama na wao huamini kuwa hawana maambuzi ya VVU.

Leticia alisema kuwa wanaume hao badala ya kupima afya zao, husubiri wake zao kupima afya wanapokuwa wajawazito.

“Vita dhidi ya Ukimwi ni ya jamii nzima na Watanzania wote, lakini wapo baadhi ya wanaume wana michepuko inayoweza kujaa mabasi mawili. Hawa hawawezi kwenda kupima VVU kwa kujihofia wenyewe,” alisema Leticia.

Alisema licha ya hali hiyo, pia baadhi ya wanawake ni chanzo cha maambukizi ya Ukimwi kutokana na kujirahisisha kwa wanaume wanaowataka.

“Hivi mwanamke unashindwaje kusema hapana unapofuatwa na mwanaume,” alisema.

Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP), Dk. James Kamuga alisema zaidi ya watu milioni 1.6 nchini  wanakadiriwa kuishi na VVU.

HALI YA MAAMBUKIZI

Akizungumza katika kilele hicho jana kwa niaba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Jenista Mhagama, alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa afya wamefanikiwa kupunguza maambukizi ya VVU pamoja na vifo vitokanavyo na Ukimwi.

“Kupitia juhudi zilizofanyika tumepunguza kiwango cha maambukizi kutoka asilimia 7.0 mwaka 2014 mpaka kufikia asilimia 4.7 kwa mwaka huu (2019).

“Pia takwimu za kitaifa zinaonyesha kuwa toka mwaka 2000 maambukizi mapya yameshuka toka watu 120,000 kila mwaka hadi kufikia watu 72,000 kila mwaka.

“Waathirika wakubwa wa janga hili wakionekana kuwa ni vijana kwani kwa mujibu wa Takwimu za mwaka 2016/17 hadi sasa asilimia 40 ya vijana  kati ya miaka 15-24 ndiyo waathirika wakubwa wa maambukizi kati yao asilimia 80 ni watoto wa kike,” alisema Mhagama

AGIZO LA SERIKALI

Hata hivyo aliitaka Tume ya Kudhibiti na Kupambana na Ukimwi Tanzania (Tacaids) kuhakikisha inasimamia kamati za Ukimwi katika halmashauri zote ili kuondoa ubadhilifu wa fedha za wafadhili na Serikali.

Pia aliwataka wadau wote wa mapambano dhidi ya Ukimwi yakiwamo Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs), kuacha tabia ya kurundikana eneo moja na badala yake wazunguke maeneo yote ya nchi ili elimu ya mapambano dhidi ya Ukimwi ifike kila sehemu na kwa makundi yote.

WAZIRI UMMY KAMPENI

Awali, akisoma taarifa kuhusu mapambano ya Ukimwi nchini, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema kuwa wizara yake kwa kushirikiana na wadau imefanya juhudi kubwa kuhakikisha inapungumza maambukizi na vifo vitokavyo na Ukimwi nchini.

“Mipango na mikakati inayofanywa chini ya wizara yangu kwa kushirikiana na wadau imefanikiwa kuamsha ari ya watu kupima ambapo hadi Septemba mwaka huu tulikuwa na watu milioni 1.2 ambao wameshapima na kujitambua.

“Pia kampeni ya tohara imekuwa na msaada mkubwa katika kupunguza maambukizi kwa wanaume ambapo toka mwaka 2009 hadi sasa jumla ya wanaume milioni 4.4 wamefanyiwa tohara,” alisema Ummy.

Alisema ugawaji wa vipimo vinavyomuwezehsa mtu kujipima mwenyewe pia umesaidia kuongeza mwamko wa jamii kupima Ukimwi ambapo kati ya vipimo 20,000 vilivyogawiwa jumla ya watu 17,000 walirudisha majibu na waliobainika kuwa na maambukizi ambapo walianza kutumia dawa za kufubaza virusi.

“Watu 90 kati ya 100 waliobainika kuwa na maambukizi wamebainika kutumia dawa za kufubaza huku watu 89 kati 90 wameonekana kufanikiwa kufubaza Virusi vya Ukimwi na hivyo kubaki na wenye afya njema,” alisema

TACAIDS NA MKAKATI

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS nchini, Leonard Maboko, alisema agizo mapambano dhidi ya Ukimwi kupitia utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu alilolitoa mwaka jana la kuwataka kufanya kazi na majukwaa ya vijana ambapo sasa kazi hiyo imeanza kuzaa matunda.

“Tunaendelea na mapambano dhidi ya Ukimwi kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo kutekeleza agizo la Waziri Mkuu ambapo haidi sasa tumeshiriki kwenye matamasha ya michezo na mziki kuhakikisha tunafikisha elimu ya kupambana na janga hili,” alisema

TAARIFA YA UNAIDS

Siku ya Ukimwi duniani huadhimishwa kila Desemba mosinya kila mwaka kwa kusherekea na kuunga mkono jitihada zinazofanyika Ulimwenguni za kuzuia maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi, kuongeza uelewa kuhusu Ukimwi na kuwafariji wale waishio na virusi.

Tangu siku ya Ukimwi ilipoanza kuadhimishwa zaidi ya miaka 30 iliyopita, maendeleo katika kuzuia na kujaribu kutibu Ukimwi yamekuwa kwa kiasi kikubwa, dawa za kuwasaidia watu wanye virusi hivyo kuishi muda mrefu, maisha yenye afya na kuzuia uambukizaji, zimepatikana.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Jamii Huonesha Tofauti.” Ikiwa inalenga msaada wa jamii kupitia uraghabishi kuhakikisha kuwa mapokeo kuhusu Ukimwi yanabaki kuwa wazi na ya kueleweka huku ikihakikisha kila mtu anashiriki katika matukio mbalimbali kuhusu Ukimwi.

Kwa mujibu wa UNAIDS, kwa mwaka 2018 watu milioni 37.9 walikuwa wanaishi na Virusi vya Ukimwi, watu milioni 1.7 walipata maambukizi mapya ya ugonjwa huo huku watu 770,000 walifariki kutokana na magonjwa yatokanayo na ugonjwa huo.

Aidha, kwa mujibu wa shirikia hilo hilo, tangu kuibuka kwa ugonjwa wa Ukimwi hadi mwishoni mwa mwaka 2018, watu milioni 74.9, wamepata maambukizi ya Ukimwi huku watu milioni 32 wakifariki kutokana na magonjwa yasababishwayo na ugonjwa huo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,903FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles