26.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Miaka 62 ya Uhuru na maendeleo sekta ya maji

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Ni miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika na maendeleo ya kupigia mfano yanayoonekana kwa macho na takwimu.

Serikali ya Awamu ya Sita katika eneo la huduma ya maji imekuwa mfano Duniani kati ya nchi zinazotekeleza mradi wa maji wa huduma ya maji ya Lipa kwa matokeo, Programu ya Uendelevu wa Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira (Pfor).

Tanzania imekuwa mfano bora katika utekelezaji kati ya nchi zaidi ya 50 na imesukuma nchi nyingine kuja kujifunza hapa nchini kazi hiyo ya kufikisha huduma ya maji kwa wananchi inavyotekelezwa.

Kupitia programu ya Lipa kwa Matokeo (PforR) Wizara ya Maji imetekeleza zaidi ya miradi ya maji 1,500 ambayo imekamilika na inatoa huduma kwa wananchi.

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dk. Victoria Kwakwa, akieleza jinsi Tanzania ilivyofanya vyema katika miradi ya maji na kuwa mfano wa kuigwa na kwa nchi nyingine.

Serikali ya Tanzania imepanga kufikia lengo la upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa asilimia 85 vijijini na mijini asilimia 95. Kwa mapinduzi yanayofanyika katika miradi ya sekta ya maji hadi Desemba 2022 hali ya upatikanaji wa huduma ya maji hapa nchini ilikuwa asilimia 88 mijini na vijijini asilimia 77, kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Maji.

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dk. Victoria Kwakwa, Novemba 2023 akiwa katika mkutano wa viongozi wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika unaohusu masuala ya upatikanaji wa majisafi na salama na usafi wa mazingira nchini Ethiopia ameipongeza Tanzania kwa kutekeleza kwa ubora na viwango Programu ya Uendelevu wa Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (PforR) na kuwa kinara wa nchi nyingine Duniani zaidi ya 50 zinazotekeleza programu hiyo.

Dk. Kwakwa ameitaka Tanzania kutoa uzoefu wa mafanikio yake kwa nchi zaidi ya 23 za Mashariki na Kusini mwa Afrika ambazo zilishiriki mkutano huo muhimu.

Hivi karibuni akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Singida, Rais Samia Suluhu Hassan, alijionea jinsi huduma ya majisafi ilivyoleta mabadiliko katika maisha ya wananchi na kusukuma maendeleo zaidi ya nchi.

“Naona wananchi tunang’aa na kupendeza na hapana shaka huduma ya maji nayo imeleta mabadiliko, sijaona madumu tupu wakati nikipokelewa,” alisema Rais Samia alisema akigusia jinsi changamoto ya huduma ya majisafi kwa wananchi ilivyofanyiwa kazi na Serikali yaani kumtua mama ndoo ya maji kichwani.


Programu ya PforR katika huduma za maji ni mpango ulioanzishwa na Benki ya Dunia (WB) na kuanza kutekelezwa Julai 15, 2019 ikiwa ni sehemu ya programu ya uhakika wa usalama wa maji na usafi wa mazingira vijijini.

Malengo ya PforR ni kuchochea kasi ya utekelezaji wa mpango wa uboreshaji huduma ya maji na usafi wa mazingira kupitia motisha zilizowekwa kwa viashiria ambavyo hupimwa kupitia mafanikio ya utekelezaji wa kazi.

Wakati miradi hiyo ya matokeo ikinufaisha Watanzania, miezi michache iliyopita Rais Samia alizindua mradi mkubwa wa maji wa Tinde – Shelui unaotumia chanzo cha maji cha Ziwa Victoria wenye thamani ya Sh bilioni 24.47 fedha ambazo ni mkopo nafuu kutoka Benki ya EXIM ya India.

Mradi wa maji wa Tinde – Shelui kwa awamu ya kwanza ya utekelezaji ilikamilika Agosti 11, 2023 kwa gharama ya Sh bilioni 24.47 na wananchi zaidi ya 40,000 wa vijiji vya Tinde mkoani Shinyanga na Shelui mkoani Singida tayari wanapata huduma ya majisafi na salama na utekelezaji wa awamu ya pili utagharimu Sh bilioni 16.2.

Takwimu za Wizara ya Maji zinaonyesha vijiji 12, 314 tayari vinapata huduma ya maji bombani na vingine 2,643 imepangwa vitanufaika na huduma hiyo ndani ya miezi 24.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, anasema kufuatia matokeo ya Tathmini ya Hali ya Upatikanaji wa Maji Vijijini iliyofanywa na Wizara ya Maji, mabadiliko makubwa yamefanyika eneo la vijijini tangu kuanzishwa kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).

Anasema Wizara ya Maji imefanikisha huduma ya maji vijijini na kutanabaisha kuwa visima na mabwawa yanachimbwa katika maeneo yote yenye uhitaji kwa sababu vifaa vya kazi hiyo Serikali imenunua na kusambaza nchi nzima.

Anasema mradi mkubwa wa maji wa miji 28 unaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni sehemu ya chachu na matunda ya ziara ya kikazi ya Rais Samia nchini India iliyofanyika hivi karibuni.

Aweso amehawahakikishia Watanzania kuwa mradi wa maji wa miji 28 utakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa mwaka 2025.

Thamani ya mradi huo ni dola za Marekani milioni 500. Mradi huo uliosainiwa Juni 6,2022 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma ambapo Rais Samia Samia alishuhudia na kuwahakikishia wananchi kazi nzuri kwa kusema “Naipongeza Wizara ya Maji chini ya Waziri Jumaa Aweso kwa kazi nzuri inayofanyika na ninawahakikishia wananchi kuwa mradi huu mkubwa wa maji hautaacha mji hata mmoja kati ya miji yote 28 iliyoainishwa”.

Miradi hiyo ya maji inatekelezwa na Serikali kwa uwekezaji mkubwa ili wananchi wapate huduma na upo ukweli halisi wa kujionea.

Tanzania ni tajiri wa rasilimali za maji kwani Atlasi ya Rasilimali za Maji (2019) inaonyesha rasilimali za maji zilizopo nchini ni wastani wa mita za ujazo bilioni 126 kwa mwaka ambapo juu ya ardhi ni mita za ujazo bilioni 105 na ardhini ni mita za ujazo bilioni 21.

Hivyo, kiasi cha maji kilichopo kwa kila mtu kwa mwaka ni wastani wa mita za ujazo 2,105. Hii ni kwa idadi ya watu milioni 59.8 waishio Tanzania Bara kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022. Kiwango kinachotajwa ni juu ya wastani wa mita za ujazo 1,700 kwa mtu kwa mwaka kinachokubalika kimataifa.

Takwimu zinaonesha kwamba inatarajiwa kufikia kiwango cha wastani wa mita za ujazo 1,700 kwa mwaka kwa mtu ifikapo mwaka 2030.
Pamoja na hayo, mahitaji ya maji nchini kwa sekta mbalimbali kwa mwaka 2022 yalikuwa ni wastani wa mita za ujazo bilioni 62 na yanatarajiwa kufikia mita za ujazo bilioni 75 mwaka 2030.

Hivyo, upo wajibu wa kuendelea kuongeza msukumo katika utunzaji wa rasilimali za maji, kuongeza ufanisi katika matumizi ya maji pamoja na kuongeza upatikanaji wa maji ikiwa ni pamoja ujenzi wa mabwawa.

Ni wazi kuwa wakati jamii ina uhitaji mkubwa wa huduma ya maji suala la usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji nalo ni muhimu kwa wanajamii wote popote pale walipo.

Usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji unahusisha tathmini na ufuatiliaji wa rasilimali za maji, kuhifadhi na kudhibiti uchafuzi wa vyanzo vya maji, kugawa maji kwa sekta mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji na kiasi cha maji kilichopo na kuendeleza rasilimali za maji.

Takwimu za Wizara ya Maji zinaonyesha hadi Aprili 2023 vituo 136 vya kufuatilia mwenendo wa rasilimali za maji vilikuwa vimekarabatiwa na vingine sita kujengwa, vibali vipya 1,554 vya matumizi ya maji na vibali 630 vya kuchimba visima vya maji kutolewa.

Pamoja na hayo leseni 105 kuhuishwa na vyanzo vya maji 63 kuwekewa mipaka na Ujenzi wa mabwawa 10 ya ukubwa wa kati na madogo kukamilika na ujenzi wa mabwawa 40 ukiendelea.

Hivyo, ni wazi kuwa wananchi wote wanaotaka kutumia maji kutoka katika vyanzo mbalimbali vya maji wanatakiwa kuomba vibali vya matumizi ya maji kutoka katika bodi za maji za mabonde hapa nchini.

Mtaalamu wa Benki ya Dunia, Esha Zaveri, hivi karibuni amenukuliwa akisema asilimia 60 ya idadi ya watu Duniani hupata janga la uhaba wa maji kwa uchache katika kati ya misimu ya hali ya hewa mwaka mmoja. Miongoni mwa vichochezi vya janga hilo ni kuongezeka kwa idadi ya watu na shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji.

Tukiadhimisha miaka 62 ya Uhuru, ieleweke kulinda na kuendeleza rasilimali za maji hapa nchini ni jukumu la kila mwanchi ili miradi inayoendelea kujengwa na ile iliyokamilika iweze kutoa huduma ya maji endelevu kwa sasa na vizazi vijavyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles