30.2 C
Dar es Salaam
Friday, May 3, 2024

Contact us: [email protected]

Mgambo wadaiwa kumuua mwanakijiji kwa kukosa Sh 100 ya kujenga choo cha shule

ALLAN VICENT

ASKARI wa akiba (mgambo) wa Kijiji cha Ushokola Kata ya Ushokola halmshauri ya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, wanatuhumiwa kumwua mkazi wa kijiji hicho Juma Abeid Rajabu (40) kwa kutolipa Sh 1,000 ya mchango wa ujenzi wa choo cha Shule ya Msingi Ushokola.

Akizungumza na gazeti hili Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Abel Busalama, alisema tukio hilo lilitokea Jumanne ya wiki hii saa 4 asubuhi.

Alisema watuhumiwa wa tukio hilo ni Moses Kiliano na Maganga Mparis.

Alisema katika siku ya tukio watuhumiwa walikuwa wakikusanya Sh 100 kutoka kila familia kwa ajili ya ujenzi wa choo cha shule na walipofika kwa marehemu hawakumkuta na nyumbani kulikuwa na mkewe mdogo na wanafamilia wengine.

Mkuu huyo wa wilaya alisema mgambo hao walidai wapewe fedha na mke huyo aliposema hana, walimchukua na kumpeleka ofisi ya mtendaji wa Serikali ya Kijiji hicho, wakisema atatoka mumewe atakapofika na kulipa mchango huo.

Busalama alisema baada ya mume huyo kufika ofisini hapo, alipodaiwa fedha hizo alisema kuwa keshalipa majibu ambayo walinzi hao hawakukubaliana nayo hivyo wakaanza kumlazimisha alipe huku wakimpiga.

Alisema baada ya kuona wamemwumiza vibaya walimchukua hadi kituo cha polisi wilayani humo kuomba PF3 ili apatiwe matibabu na baada ya kuipata walimpeleka zahanati ya mtu binafsi itwayo Msamaria na kumwacha hapo na wakatokomea kusikojulikana.

 “Baada ya kuona hali sio nzuri, ndugu zake waliamua kumpeleka Hospitali ya Misheni ili akapate matibabu zaidi lakini wakati juhudi za kumpatia matibabu hayo zikiendelea alifariki dunia”, alisema.

Ndugu wa karibu wa marehemu walilieleza gazeti hili kuwa, mtendaji wa kijiji hicho anashikiliwa na jeshi la polisi wilayani humo kwa upelelezi wa tukio hilo huku mgambo wanaotuhumiwa kusababisha mauaji hayo wakiwa wanaendelea kusakwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles