26.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 6, 2021

Membe azidi kung’ang’aniwa

*Dk Bashiru asema yeye ni Mgeni wa timu Lowassa, Timu Membe, siyo mgeni wa katiba ya CCM

*Asema hamzuii kumjibu kwenye mitandao na anayoyajibu yataipa nafasi wana CCM kupimana

HARRIETH MANDARI, GEITAKATIBU Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, ameendelea kumshukia aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, huku akishangaa kitendo cha kujibu wito wake kupitia mitandao na kumtaka ajifunze hekima na busara kutoka kwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Dk. Bashiru alitoa kauli hiyo juzi usiku akiwa mkoani Geita, ikiwa ni mwendelezo wa kauli nyingine aliyoitoa Ijumaa wiki iliyopita akiwa mkoani hapa.

Katika kauli yake ya kwanza, Dk Bashiru alimtaka Membe kufika ofisini kwake wazungumze juu ya tuhuma kuwa anaandaa mipango ya kumkwamisha Rais Dk. John Magufuli.

Baada ya kauli hiyo kusambaa katika mitandao ya kijamii Membe ambeye ni Mbunge wa zamani wa Jimbo la Mtama, alieleza kushangazwa na utaratibu uliotumika kumwita akibainisha kuwa pengine ni ugeni wa kazini wa Bashiru, lakini akaahidi kwenda kumwona akirudi safari ya nje ya nchi.

Kuhusu Membe

Jana Dk. Bashiru alisema alimwita Membe akiwa kama mmoja wa kada wa chama na mtu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje ambaye pia ni mwananchama wa CCM.

Alisema yeye kama katibu wa chama ana haki ya kukutana na viongozi wa sasa na wa zamani kwa nia ya kujadili masuala ya kuimarisha chama.

“Moja ya haki ya kiongozi kwa nafasi yangu ni ya kukutana na viongozi wa chama, baada ya mimi kuteuliwa kwenye nafasi hii nimekutana na makada na viongozi mbalimbali wa CCM akiwemo Rais mstaafu Benjamin Mkapa, Maria Nyerere, hao wote ni makada kama alivyo Membe.

“Wengine ni Warioba (Waziri Mku Mstaafu, Sinde), Dk Salim Ahmed Salim, Hussein Bashe (Mbunge wa Nzega Mjini), Joseph  Butiku, Nape Mnauye (Mbunge wa Mtama),” alisema.

Alisema pia alikutana na Waziri Mkuu Mstaafu, John  Malecela ambaye alimuhimiza juu ya umuhimu wa kukaa karibu na mabalozi wa nyumba 10 kwani wao ni muhimili wa chama.

“Mzee Malecela alinikumbusha kuwa CCM ingepata tabu kupita uchaguzi wa mwaka 2015 ila ikanusurika kwa sababu ya mchango mkubwa wa ukaribu mzuri wa  mabalozi wa nyumba 10, ndiyo moja ya nguzo za uhai wa CCM ambao walisaidia kupambana na timu Lowassa, timu Membe na nyinginezo zilizotaka kupasua nchi na chama akasema.

“Aliniambia ukaribu wa mabalozi ni muhimu kwani hawana timu Membe wala timu Lowasa timu January Makamba (Mbunge wa Bumbuli) na wengine mnaowajua, akasema mabalozi ndiyo wanakua kazini kusaidia chama lakini timu hizo huwa kazini kutafuta uongozi.

“Sasa iweje mimi kusema nataka Membe aje ofisini kwangu imekuwa jambo kubwa, najua yeye ni kada, tangu niteuliwe hajawahi kunisalimia, ningehitaji busara zake.

“Pia nimesikia mabarabarani huko kwamba anaendeleza makundi,  kazi yangu mojawapo ni kuratibu shughuli zote za kitaifa, sikutarajia kujibiwa mtandaoni na akasema eti mimi ni ‘mgeni wa mambo’,  mimi  ni mgeni wa timu Membe na timu Lowassa, ila  sio mgeni wa CCM.

“Sio mgeni wa kanuni za CCM, ana hiari ya kuja sina mashtaka nae, aje tujadili changamoto zinazowakumba wakulima wa korosho pia tujadili na kuimarisha diplomasia.

“Mbona anakimbilia mashtaka, halafu anachanganya anasema habari ya TIS (Usalama wa Taifa) kwenye mitandao, someni Katiba ya CCM, mimi kazi yangu ni kusimamia taratibu za CCM,  mimi ninahusika na TIS? Someni Katiba kama mimi ninahusika kwa namna yoyote nayo, anajua tangu amekuwa waziri na kada anajua nani anahusika nayo.

“Vilevile anamhusisha Musiba (Cyprian) katika mkutano wangu na yeye, kwanza Musiba ana nini jipya? amemtaja hata naibu katibu mkuu wa Zanzibar, ambaye ni mjumbe  wa sekretarieti, lakini mjumbe huyo anajua taratibu ndiyo maana hapayuki kwenye mitandao,”alisema.

Dk. Bashiru aliendelea kusema. “Chama siyo chombo cha kusimamia wanaharakati wala hatupimi ukweli wa wanaharakati, unajua nchi hii tulifika mahala kakikundi kalijitokeza na kujifanya ndio kako juu ya sheria wakataka kukisambaratisha chama.

“Namhimiza Membe aje sio kwa ajili ya mashitaka aje tujenge chama, simzuii kunijibu kwenye mitandao na anayoyajibu yanatupa nafasi sisi wana CCM kupimana, kasoro mbali mbali, na nimeziona  meseji zake kuwa mimi ni mgeni, hakuna timu nani wala nani ndani ya chama, wote tuna hadhi moja kwa haki ya wananchama,”aliongeza.

Kuhusu Lowassa

Dk. Bashiru alisema alikutana na Lowassa katika ukumbi wa Nkuruma kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),  ambapo Lowassa alimipa mkono na kumpongeza.

“Akasema unafanya kazi nzuri, baada ya hapo akapiga  siasa na mimi nikamjibu  kwa  siasa, ni mzee muungwana sana

“Tulitofautiana pale aliposema  kwamba tumeshinda kule (Monduli) kwa magari ya polisi wakati  alikuwa  hapati hata watu wa kufanya nao mikutano, ndio nilifafanua tu kwamba  watu walimkataa na tukamshinda kwa asilimia 95 .

“Lakini hajawahi kuzusha, hajawahi kutoa kauli za dharau dhidi ya Rais wetu, pia sio kwamba amekutana na mimi peke yangu ingawaje siku ile haukua mkutano rasmi (walipokutan UDSM), kwa maana ya kutembeleana, lakini tulisalimiana na akanipa mkono tena kwa kuwa alikua mbele yangu akageuka kunipa mkono tukasalimiana, namheshimu sana na namheshimu kwa uamuzi wake wa kutoka kwenye Chama Cha Mapinduzi na kwenda chama kingine,” alisema.

Dk Bashiru alisema kitu ambacho  yeye asingekipenda  ni kwa mtu kubaki ndani ya chama kinafiki na kuendeleza makundi ya kukigawa chama.

“Mimi ndiye mkurugenzi wa uchaguzi kikatiba  na nisingependa migogoro iliyowakumba makatibu wakuu wenzangu waliotangulia wakati wa uchaguzi nikutane nayo.

“Mkakati wangu ni kuua makundi ndio, mkakati wa Kamati Kuu, wa Halmshauri Kuu ya Taifa chombo ambacho pia nawajibika nacho na ndiyo uongozi wa mwenyekiti wetu.

“Mimi sina shida na ndugu Lowassa kwa sababu aliko najua, mimi nikitega mitambo yangu huku na yeye anatega ya kwake na mimi nilipoipima Monduli ameona  kilichompata kwenye mitambo yangu.

“Yeye pia ni waziri mkuu wetu mstaafu  ndio maana alienda Ikulu miongoni mwa wastaafu walioenda Ikulu  kwa hiyo tunataka kujifunza vizuri hasa kwa wanasiasa wachanga na wale wa kati kama ndugu Membe  wajifunze hekima na busara za ndugu Lowassa,” alisema.

Nidhamu ndani ya chama

Dk Bashiru pia alihimiza nidhamu ndani ya chama na kukitaka chama hicho kikomeshe tabia ya kutegemea wafadhili badala yake vyanzo vya mapato vianzishwe.

“Lazima chama kikomeshe tabia ya kufadhiliwa na matajiri na badala yake kiendeshwe na miradi ya chama na michango ya hiari na nguvu za wananchama,”alisema.

Aliwataka pia wanachama hao kuacha kupoteza muda kwenye mitandao kwa kuchangia hoja zisizo na tija badala yake washiriki katika shughuli za maendeleo.

Aidha, alisema kwa muda mrefu nidhamu ilipotea wanachama wanafanya kazi kiholela, hawachapi kazi, wanapiga soga na kupoteza muda kwenye mitandao.

“Watu wengi wanapoteza muda kwenye mitandao na sana sana wanayoyazungumza ni porojo si mambo ya kujenga.

“Tumekubaliana mwananchama yeyote atakayetumia vibaya mitandao kumhujumu mwenzake, kufitini na kuzua mambo ambayo yanaleta mtafarufu ndani ya chama, vikao vya chama vichukue hatua haraka inavyowezekana.

Kilimo

Alisema amewahimiza watendaji hao juu ya umuhimu wa kujizatiti katika sekta  muhimu  zikiwemo sekta ya kilimo nay a elimu.

“Kwamba kilimo ndiyo uti wa mgongo wetu kilimo hicho kizalishe chakula chenye ubora, kiinue sekta ya  viwanda kama tunavyojua kwa sasa kilimo kinachangia kidogo sana  kama asilimia 25 hado 30  pamoja kuwa kinafanywa na wakulima kwa asilimia 80 nchini, kitaifa huu ni  ilemavu wa kiuchumi,”alisema.

Akasema haiwezekani kilimo kiwe bora bila matumizi bora ya ardhi, na kwamba ardhi isigawanywe kiholela kwa wawekezaji na badala yake itumike vizuri na vilevile migogoro iepukwe kwani amegundua kuwa ipo migogoro mingi sana ya ardhi katika mkoa wa Geita.

“Ardhi isitolewe kiholela kwa wawekezaji kutoka nje ambao wanakuja kulima maparachichic na mihogo kana kwamba watanzania wananshindwa kulima.

Aliwasisitizia pia juu ya umuhimu wa watendaji hao kufanya kazi kama timu kuwa ni la ni  la lazima.

“Na umoja tunaosemea ni ule wa kuchapa kazi za siasa kama vile kutoa uongozi bora utakaotatua kero za wananchi, utakaotekeleza miradi ya maendeleo ya wanachi,”alisema.

Akaongeza kuwa waenenzi wote waache tabia ya kushiriki katika kampeni za kitaifa yakiwemo mapambano dhidi ya  mapmbano dhini ya UKIMWI, mapambano dhidi ya  rushwa na ufisadi na pia za kilimo, afya na mengineyo ili kuhakikisha ujumbe unafika.

“Tuache tabia za kuleana na kulindana mema yatangazwe hadharani na mabaya pia yatangazwe hadharani,”alisema.

Mimba za utotoni

Kuhusu hali ya mimba za utotoni na utoro mashuleni alisema miundombinu iimarishwe katika shule ili kuiepuka tatizo hilo  na pia kwa wazazi wahakikishe wanatoa malezi bora kwa watoto wao hasa wa kike.

“Wazazi na walezi wahakikishe wanawalea watoto katika malezi ya dini mimi nina watoto wa kike lakini ninawalea katika maadili bora,”alisema.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,340FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles