MCT, LHRC zaibwaga serikali kesi ya Sheria ya Habari

0
3269

Eliya Mbonea, Arusha

Asasi tatu za kiraia zimeibwaga serikali baada ya kushinda kesi ya kupinga Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.

Asasi hizo ni Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, ambazo kwa pamoja zilifungua kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupinga baadhi ya vifungu katika sheria hiyo.

Hukumu hiyo imesomwa leo Alhamisi Machi 28, mbele ya Jopo la majaji watatu Jaji Charles Nyachae, Monica Mugenyi na Jaji Justice Ngie.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Nyachae amesema vifungu vilivyo kwenye sheria hiyo ni vibovu na vinavyokiuka mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo ameitaka Serikali ya Tanzania kurekebisha vifungu vya Sheria ya Uhuru wa Habari kutokana na kukiuka Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Sheria hii inapaswa kufanyiwa marekebisho ili iendane na mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiya,” amesema Jaji Nyachae.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo kutolewa, Katibu wa MCT, Kajubi Mukajanga amesema leo ni siku ya kihistoria na ushindi kwa wanahabari na ushindi kwa Serikali kwani imepewa wasaa wa kwenda kurekebisha sheria hiyo.

“Demokrasia leo imeshinda haki ya wanahabari kufanya kazi bila kuingiliwa imethibitishwa leo na Mahakama ya Afrika Mashariki,” amesema Mukajanga.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here