30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 25, 2022

MBOWE ATAKA USHIRIKIANO WABUNGE WA CCM,

Na MAREGESI PAUL Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amewataka wabunge waendelee kupendana hata baada ya msiba wa Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (Chadema).

Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, aliyasema hayo mjini hapa jana wakati wabunge na watumishi wa Bunge, walipokuwa wakiaga mwili wa marehemu Bilago.

“Bilago alikuwa na vyeo vitatu kwa maana kwamba alikuwa ni mbunge wetu, alikuwa ni mjumbe wa Kamati Kuu na pia alikuwa ni Mwenyekiti wa Kanda ya Magharibi inayohusisha Mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora.

“Kupitia msiba huu, tunawashukuru wenzetu wote waliojitokeza kuwa pamoja na sisi, lakini ieleweke kwamba, kifo ni fursa ya kuleta upatanisho na ni fursa ya sisi kutafakari juu ya maisha yetu.

“Kupitia kifo, lazima tuelewe kwamba, vyeo na utukufu wetu hapa duniani, mwisho wake ni hapa ingawa katika siasa zetu kuna mahali tunavutana na kuumizana.

“Leo hii, mwenzetu ametutoka na ndiye aliyetukutanisha hapa, kwa hiyo, ni vizuri tusisubiri kukutanishwa na kupendana katika mazingira kama haya badala yake tupendane wakati wote.

“Siku zote ubishani hauna msingi na unapotokea linakuwa ni jambo la kutia simanzi kwa sababu mheshimiwa Bilango alifia Dar es Salaam na isingewezekana atolewe Dar es Salaam bila kuagwa ndiyo maana tuliliarifu Bunge juu ya ibada tuliyoifanya huko kabla hatujaja hapa.

“Vile vile, Bilago alikuwa ni mbunge kule Buyungu na wananchi wa kule wanamlilia huenda kuliko sisi, pia wana utaratibu wao wa kumuaga marehemu.

“Sisi kama chama, tulitaka kumzika marehemu siku ya Jumamosi, lakini baada ya kukaa na familia, wao wakasema watamzika Alhamisi(kesho), kisha tukalieleza Bunge.

“Lakini, sasa tunashangaa, kwamba tunatoa ratiba hii na wenzetu nao wanatoa ratiba yao, why?.

“Hapa tumekutana na kupeana mikono na naomba isiwe mikono ya kinafiki,” alisema Mbowe bila kufafanua zaidi.

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alipokuwa akizungumza mahali hapo, alisema Bunge halikuwa na sababu ya kuchukua madaraka ya familia au Chadema wakati wa mazishi ya mbunge huyo.

“Kwa niaba ya Spika, kama alivyoongea mheshimiwa Mbowe, na mimi naomba niongee japo kidogo ili kuweka mambo sawa.

“Baada ya kifo cha mheshimiwa Bilago, Kamati ya Uongozi ya Bunge na Tume ya Utumishi ya Bunge, vilikutana ili kujadili juu ya kifo hiki kwa sababu kilitokea kwa ghafla na wabunge wengi hawakujua kama mwenzao anaumwa.

“Kwa  bahati mbaya, katika kikao kile mheshimiwa Mbowe hakuwepo kwa sababu alikuwa Dar es Salaam, lakini kwenye kikao chetu aliwakilishwa.

“Katika hili, Bunge halina sababu yoyote ya kupoka madaraka ya familia au Chadema na ndiyo maana Spika aliitisha kikao kujadili msiba huu.

“Katika kikao chetu, tulikubaliana marehemu azikwe Jumatano (leo), ila hiyo ratiba ya marehemu kuzikwa Alhamisi ilikuja baada ya sisi kuwa tumetoa ratiba yetu.

“Najua mheshimiwa Mbowe atakwenda Kigoma msibani na atakutana na mheshimiwa Spika huko, naamini hakitaharibika kitu kwa sababu marehemu atasindikizwa vizuri na familia, Bunge na Chadema wenyewe.

“Kuhusu familia, Bunge litashirikiana nao wakati wote na kama kutakuwa na tatizo lolote, wasisite kuwasiliana nasi ili tuweze kujua namna ya kulitatua,” alisema Naibu Spika.

ZITTO KABWE

Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alisema kifo cha Bilago ni pigo bungeni kwa sababu alikuwa bingwa wa kujenga hoja na mwepesi wa kusamehe kila alipokuwa akitofautiana kimawazo na mbunge mwenzake.

Katika maelezo yake, Zitto alieleza jinsi marehemu Bilago alivyowahi kutofautiana kimawazo na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, kisha wakaelewana baada ya muda mfupi.

“Bilago alikuwa akitufundisha, alikuwa akitichekesha kiasi kwamba kila alipokuwa akisimama kuongea, kila mmoja alikuwa akimsikiliza kwa makini.

“Bilago alikuwa ni zawadi kwetu, alikuwa zawadi ya Watanzania, alikuwa zawadi kwa wana Kigoma na alikuwa zawadi kwa wana Buyungu.

“Alikuwa mcheshi, alikuwa mwalimu na alikuwa mwepesi wa kusamehe na kama mtakumbuka, aliwahi kutofautiana na Profesa Kabudi, lakini baadaye wakasameheana.

“Bilago tutakukubuka, ukifika huko msalimie Hafidh Ally uliyekuwa ukikaa naye jirani, wasalimie wabunge wote waliotangulia,wasalimie wafanyakazi wote wa Bunge walioko huko na waambie mtuwekee nafasi kwa sababu na sisi tunakuja.

“Mwisho, nakuthibitishia kwamba, tutakuenzi katika maisha yetu yote kwa sababu wayungu walitulea mtu,” alisema Zitto huku akitokwa na machozi.

DK.MWINYI

Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,Dk Hussein Mwinyi, ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni,badala ya Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa alisema,Serikali itamkumbuka marehemu kwa  michango yake mbalimbali bungeni.

“Tutamkumbuka kwa michango yake mingi kwa Serikali.Tunaomba tuendelee kushirikiana sote ni wasafiri na hapa tunapita tu,”alisema.

DK.NDUBARO

Kwa upande wake, Mbunge wa Songea Mjini, Dk.Damas Ndumbaro (CCM)  alisema atamkumbuka marehemu kutokana na kumkaribisha bungeni kwa mara ya kwanza kwa usia wa mambo ya michezo asiyalete bungeni.

“Nitamkumbuka marehemu kwa kunikaribisha bungeni kwa mara ya kwanza huku akinitaka mambo ya mpira nisiyalete bungeni,”alisema.

Pia alisema alikuwa na uwezo wa kuzungumza jambo kubwa bila ya kuiumiza Serikali ama mtu.

“Nimepoteza mtani maana sisi na waha ni watani,hivyo nimempoteza mtani ambaye alikuwa ni mtu makini,”alisema.

MWAKAGENDA

Naye Mbunge wa Viti Maalum, Sofia Mwakagenda (Chadema) alisema marehemu alikuwa     mtetezi wa kweli wa sekta ya elimu.

“Alikuwa baba mwema,hakika tutamkumbuka kwa kutusaidia kupigania elimu ya Tanzania,”alisema.

PADRI

Kwa upande wake Padri wa Kanisa la Romani Cathoriki  Parokia ya Mtakatifu Petro,  Swaswa Jijini hapa, Antipas Shayo,ambaye aliongoza ibara hiyo,aliwataka waumini kutembea na mafuta ya upako.

Alisema  Mei 25 mwaka huu Marehemu  alikuwa akitimiza Jubilee ya miaka 25 ya ndoa na mkewe hivyo alikuwa akitembea na mafuta ya upako.

“Mei 25 alikuwa akitimiza miaka 25 ya ndoa, alikuwa na nia njema, alikuwa akitembea na mafuta ya upako,”alisema.

Askofu Shayo alisema  kuna haja ya  kuendelea kumuombea marehemu pamoja na familia yake.

“Mimi na wewe tujiulize tutaishi miaka mingapi na Je tunatembea na mafuta ya upako,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
201,896FollowersFollow
553,000SubscribersSubscribe

Latest Articles