25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Masha apata dhamana

Law+Masha+PHOTONA WALTER MGULUCHUMA, KATAVI

ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, akiwa na viongozi sita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Katavi, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda kwa tuhuma za kufanya mkutano wa hadhara na kuingia bila kibali katika makazi ya wakimbizi ya Katumba wilayani Mlele na kuachiwa kwa dhamana baada ya mabishano ya kisheria.

Masha na watuhumiwa wenzake sita walifikishwa mahakamani hapo jana chini ya ulinzi mkali wa polisi waliokuwa na bunduki na mabomu ya machozi, na kusomewa mashtaka na mwanasheria wa Serikali, Lungano Mwasubila, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda, Chiganga Ntengwa.

Watuhumiwa wengine ni mgombea ubunge wa Jimbo la Nsimbo, Gerald Kitabu, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mpanda, Abrahamu Mapunda, Katibu wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) Mkoa wa Katavi, Fransico Misigalo, Sinsilausi Kaswele, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Nsimbo, Lameck  Costantino na Katibu wa Chadema Jimbo la Nsimbo, Galus Adamu.

Mwasubila alidai mahakama hapo kuwa Masha ambaye ni mtuhumiwa wa kwanza na wenzake, walitenda kosa hilo Oktoba 19, mwaka huu saa saba mchana katika makambi hayo.

Watuhumiwa hao walisomewa mashitaka matatu ambapo la kwanza ni kuingia katika makazi ya wakimbizi bila kibali cha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Shitaka la pili ni kufanya mkutano katika makazi hayo na shitaka la tatu ni kuingia katika Kambi ya Katumba bila kibali cha mkuu wa makazi hayo.

Baada ya watuhumiwa kusomewa mashitaka hayo, Hakimu Chiganga, aliwataka wajibu ambapo yote waliyakana.

Mwasubila aliiomba mahakama isitoe dhamana kwa Masha kwa kile alichodai kuwa ana kesi nyingine ya jinai katika Makakama ya Kisutu jijini Dares Salaam. Watuhumiwa wengine sita dhamana zao zilikuwa wazi.

Wakili aliyekuwa akiwatetea watuhumiwa hao, Elias Kifunda, alipinga ombi hilo kwa kile alichoeleza Masha alifikishwa Kisutu,  lakini mahakama hiyo bado haijamtia hatiani, hivyo anayo haki ya kupewa dhamana kama akitimiza masharti.

Baada ya mabishano ya kisheria baina ya pande hizo yaliyodumu kwa dakika 30, hakimu Chiganga alilazimika kuahirisha kesi hiyo kwa muda wa dakika 40 aweze  kupitia vifungu vya sheria walivyobishania kabla ya kutoa uamuzi wa kukubali au kukataa dhamana ya Masha.

Baada ya kupitia vifungu vya sheria  alikubaliana na ombi la Kifunda la kutaka Masha kupewa dhamana kwa kile alichoeleza kuwa shtaka aliloshtakiwa nalo Kisutu alimfanyi kunyimwa haki hiyo kwa kuwa bado hajatiwa hatiani.

Baada ya kueleza hicho, mahakama hiyo  ilitoa dhamana kwa Masha na wenzake sita kwa masharti ya kudhaminiwa na mtu mmoja kwa kila mtuhumiwa kwa kiasi cha Sh laki moja, na wote walitimiza masharti na kuachiwa. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 19, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles