23.7 C
Dar es Salaam
Saturday, September 23, 2023

Contact us: [email protected]

Mapato bandari ya Mwanza yaongezeka

NA ESTHER MBUSSI

-MWANZA

KUFUNGULIWA kwa njia ya Mwanza hadi bandari ya Uganda ambayo ilikuwa haitumiki kwa zaidi ya miaka 10, kumeongeza mapato ya Bandari ya Mwanza, kutoka Sh milioni 619.71 mwaka 2017/18 hadi Sh bilioni 1,138.28 mwaka 2018/19 ikiwa ni wastani wa asilimia 54.6.

Mapato hayo yanatokana na shughuli za kupakia na kupakua shehena katika bandari hiyo.

Kauli hiyo imetolewa juzi na Kaimu Meneja wa Bandari ya Ziwa Victoria, Geofrey Lwesya, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa miradi ya bandari katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli.

 Alitaja sababu nyingine ya kuongezeka kwa mapato kuwa ni kurejea kwa shughuli za usafirishaji wa mizigo katika Bandari ya Musoma ambayo inahudumia meli zaidi ya tatu kwa siku.

“Lakini pia matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) katika makusanyo ya mapato, katika bandari kubwa za Kemondo na Mwaloni, Kyamkwikwi, Mwanza Kaskazini na Kusini, Isaka, Mwigobero Bukoba na Mwalo wake na Nansio nayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa mapato,” alisema Lwesya.

Alitaja sababu nyingine kuwa ni kurejea kwa wateja ambao walikuwa wameacha kutumia bandari ya Mwanza Kusini na Musoma na maboresho ya shughuli za usafirishaji katika mashirika la Reli Tanzania (TRC) na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL).

Akizungumzia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika bandari hiyo kwa lengo la kuboresha, alisema wanafanya  ujenzi wa gati la Ntama katika Bandari ya Sengerema, ujenzi wa gati la Mwigobero katika Bandari ya Musoma ambao tayari umekamilika kwa gharama ya Sh milioni 605.036.

 “Mradi mwingine ni ujenzi wa gati la Nyamirembe katika Bandari ya Chato ambao kwa sasa umefikia asilimia 40 ya utekelezaji, sehemu ya kazi iliyobaki ni kumalizia ujenzi wa jengo la abiria, jengo la mizigo, uzio, vyoo, mnara wa tanki la maji na ujenzi wa mashine ya umeme na chumba cha walinzi.

“Mradi huu unatarajiwa kukamilika Juni 16 mwaka 2020 na utagharimu Sh bilioni 1.7,” alisema.

Licha ya mafanikio hayo, Lwesya aliwataka wadau wa bandari na wasafirishaji wa shehena za mizigo kutoka nchi mbalimbali kutumia Bandari ya Mwanza kutokana na bandari hiyo kuwa ndiyo yenye gharama nafuu na kutumia muda mfupi kuliko zote.

“Mwanza Kusini ndiyo inatuunganisha na wote, tuna gati za kisasa, vitendea kazi vya kutosha na sisi ndiyo wenye bei nafuu kuliko wote na tunatumia muda mfupi.

“WFP ni mteja wetu mkubwa ambapo wanatumia Bandari ya Isaka kusafirisha chakula mara kwa mara kwenda Sudan Kusini, lakini pia Rwanda, Burundi na Uganda nao ni wadau wetu wakubwa,” alisema.   

Lwesya pia amesema kumekuwapo na mikakati mbalimbali ili kuendana na mahitaji ya wateja na soko lililopo ikiwamo kuendelea na wateja waliopo, kutafuta wateja wapya na kurudisha walioondoka kwenye soko na kuzidisha wateja wakubwa.

Alitaja mikakati mingine ni kurasimisha bandari binafsi, ununuzi wa vifaa vipya kwa ajili ya ubebaji wa mizigo na kuajiri wafanyakazi wapya ili kuimarisha utendaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,699FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles