26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

MAMBO 10 YANAYOKUFANYA USHINDWE KUFANYA MAZOEZI

Mazoezi ya kukimbia
Mazoezi ya kukimbia

Dk. Fredirick L Mashili, MD, PhD. 

KUNA watu wanapenda kufanya mazoezi na wako wasiopenda. Kwa wasiopenda lazima kunakuwa na sababu moja, mbili au zaidi zinazowafanya kulikwepa jukumu hili ambalo kiukweli linafaida tele katika maisha yetu. Mara nyingi wanakuwa wanatamani kufanya hivyo lakini hujikuta wakishindwa kutokana na sababu fulani fulani, mwishowe hujisikia vibaya kwa kuwa wanafahamu fika kwamba kufanya mazoezi ni muhimu kwa afya.

Uwe katika kundi la kupenda au kutokupenda kufanya mazoezi, ukweli unabaki pale pale kwamba kila mmoja wetu anatakiwa kutimiza dakika zisizopungua 150 kwa wiki (wastani wa dakika 30 kwa siku) za mazoezi yanayotumia nguvu au kasi ya wastani ili kudumisha afya na kujikinga na magonjwa.

Zifuatazo ni sababu kubwa kumi zinazowafanya watu kutofanya mazoezi.

Kukosa muda

Ukifikiria muda wa kazi na ule wa kuwa na familia, unaweza kuona kama hakuna muda wa kufanya mazoezi. Hii si sahihi, viko vitu vingi tunavyoweza kufanya kama sehemu ya kazi na hata sehemu ya kuwa na familia ambavyo pia hutupa fursa ya kufanya mazoezi. Tumia ngazi kwenda ofisini, tembea kwenda kupata chakula cha mchana au paki gari yako mbali na ofisi ili upate fursa ya kutembea. Ikiwezekana tembea kwenda dukani kununua chochote unachohitaji na wakati mwingine tembea kwenda kuwachukua watoto shuleni. Unaweza pia kutembea na familia yako muda wa jioni au katika siku za mwisho wa juma.

 Kukosa nguvu

Siku nzima kazini, shuleni au kuwahudumia watoto inaweza kabisa kukumalizia nguvu hivyo kukufanya ushindwe kufanya mazoezi. Fanya mazoezi katika muda ambao mwili bado una nguvu ya kutosha, hususani wakati wa alfajiri. Amka dakika 15 mpaka 20 mapema zaidi ya muda wako wa kawaida na fanya mazoezi kama vile kuruka kamba, kupiga push ups au aerobic dance. Tembea wakati wa chakula cha mchana au nenda gym kabla ya kurudi nyumbani wakati wa jioni. 

Unachofanya katika muda wako wa ziada

Kuwa na mambo mengine ya kufanya katika muda wako wa ziada kunaweza kuchukua muda ambao ungeutumia kufanya mazoezi. Yape mazoezi kipaumbele. Chagua vitu vya kufanya katika muda wako wa ziada ambavyo havikufanyi kukaa bali kukupa fursa ya kufanya mazoezi. Kutana na marafiki katika klabu za michezo, fanya manunuzi kwenye sehemu zenye maduka mengi (mall) ili upate fursa ya kutembea tembea, kutana na marafiki kwenye bustani baadala ya baa na baadala ya kutazama sinema kwenya TV ukiwa umeketi nyumbani, tembea kwenda na kutoka kwenye jumba la sinema lililokaribu yako.

 Hujajenga tabia ya kufanya mazoezi

Kuzoea kufanya vitu vyenye faida huja kwa ugumu kidogo. Jiwekee lengo la kufanya mazoezi kwa mfululizo ndani ya mwezi mmoja bila kukosa. Baada ya wiki tatu mpaka nne, utajikuta umezoea na hautahitaji kujilazimisha kufanya hivyo. Kumbuka sababu zinazokufanya ufanye mazoezi na jiwekee malengo madogo madogo yanayotimizika kama vile kuweza kuruka kamba mara 50 bila kupumzika baada ya wiki moja.

 Hakuna muamko/hamasa

Kama huna sababu ya msingi ya kufanya mazoezi, hautaweza kufanya hivyo. Jielimishe ili upate ufahamu kuhusu umuhimu wa mazoezi kwa afya yako hata kama hauna tatizo la unene. Soma vitabu na makala mbali mbali zitakazokuelimisha jinsi ambavyo mazoezi yanaweza kuzuia magonjwa sugu kama kisukari na shinikizo la juu la damu. Kwa hamasa zaidi, jiwekee zawadi kila unapotimiza malengo yako madogo madogo.

 Ni kazi mno

Unaweza kudhani kufanya mazoezi ni kazi kubwa kama hujawahi kuwa na mpangilio huo hapo awali. Anza taratibu kwa kufanya vitu virahisi kama vile kutembea na kupanda ngazi. Anza na kufanya mazoezi kwa muda wa dakika 10 mfululizo na ongeza muda kadri unavyozoea.

 Lishe mbovu

Kama mlo wako hauna virutubisho vya kutosha unaweza kukosa nguvu ya kufanya mazoezi. Achana na vyakula vya haraka haraka kama chips mayai na punguza vitu vitamu kwenye mlo wako. Kula mlo wenye nafaka zisizokobolewa, mboga mboga na matunda pamoja na protini. Vyakula hivi vitakupa nguvu na stamina ya kufanya mazoezi na wakati huo huo kukupa afya bora.

 Hali yako ya sasa kiafya

Huenda ukawa na unene uliokithiri, umewahi kupata shambulio la moyo au unadhani umri wako umekwenda na huwezi kufanya mazoezi. Inawezekana ukahitaji kumuona kwanza daktari lakini ifahamike kwamba kila mmoja wetu anao uwezo wa kufanya kiasi fulani cha mazoezi bila kujali ukubwa, umri au hali.

 Hakuna sehemu ya kufanyia mazoezi

Huhitaji kuwa na vifaa vizuri au kwenda gym kuweza kufanya mazoezi. Unaweza kufanya mazoezi bila kutumia gharama kubwa kwa kutumia vitu kama kamba, mipira ya kuvuta na vishikio vya kupigia push up. Unaweza pia kuwa na DVD yenye programu za mazoezi ambayo unaweza kuitumia ukiwa nyumbani.

 Kutokuona matokeo

Unapokuwa hauoni matokeo uliyotarajia unaanza kukata tamaa. Usikate tamaa, endelea kufanya mazoezi. Mazoezi yanaubadilisha mwili wako zaidi ya wewe unavyoona. Yanasaidia kupunguza shinikizo la damu, yanaongeza nguvu na pumzi na yanakukinga na magonjwa sugu kama kisukari na baadhi ya saratani. Unaweza usizione faida hizi leo na ukaja kuzikubali miaka mitano au hata 40 ijayo.

 Dk. Mashili ni Mtaalamu wa Fisiolojia ya Mazoezi na Homoni. Pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS). Kwa maelezo zaidi unaweza wasiliana naye kwa 0752255949, barua pepe, [email protected]. Unaweza pia kujifunza zaidi kwa kutembelea moja wapo ya tovuti zake: www.jamiihealthtz.com au www.jamiiactive.org

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles