Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
KWA kawaida huwa ni furaha kubwa pale mwanamke anapopata mtoto, inasadikika kuwa hiyo huwa ni furaha kuu katika maisha ya mwanamke.
Inaelezwa kwamba wakati mwingine hata hivyo hutokea mama wa mtoto kukosa furaha, kujikuta mwenye huzuni na hasira, au hata kujiona mpweke, mwoga na mwenye kukosa upendo kwa mtoto hata kufikia kuwa na fikra za kumdhuru.
Daktari Bingwa wa Afya ya Akili, Praxeda Swai anasema hizo zinaweza kuwa dalili za tatizo la sonona baada ya kujifungua au kwa lugha ya kitaalamu ‘postpartum depression’.
Anasema idadi kubwa ya wanawake sawa na asilimia 30 hadi 80 mara baada ya kujifungua hupatwa na hali za kuwa na huzuni, wasiwasi, kukosa usingizi na kupungukiwa kwa hamu ya kula.
“Wanawake huweza pia kuwa na hali ya kubadilika badilika kwa hisia (mood swings). Kwa ujumla hali hii hujulikana kitaalamu maternal blues, dalili hizi huwa kwa kiasi kidogo na mara nyingi huisha ndani ya muda mfupi lakini zikiendelea kwa kipindi kisichozidi wiki mbili basi hiyo inaweza kuwa dalili za sonona,” anasema.
Anasema tatizo la sonona hutokea baada ya mama kujifungua, mara nyingi ndani ya miezi minne ya mwanzo lakini linaweza pia kutokea wakati wowote katika kipindi cha mwaka mmoja baada ya kujifungua.
“Tafiti zinaonyesha kuwa kati ya wanawake kumi wanaojifungua mmoja mpaka wawili yaani asilimia 10 hadi 15 hupatwa na tatizo la kukosa furaha kupindukia (sonona),” anasema.
DALILI ZIPOJE
Anataja dalili za tatizo hilo kuwa ni pamoja na kukosa furaha hata kwa vitu ambavyo mama alikuwa akivipenda.
“Wakati mwingine huwa na huzuni inayomfanya alie mara kwa mara na kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa, wapo ambao hukosa nguvu, usingizi, hamu ya kula na kupungua uzito,” anasema.
Anasema dalili nyingine ni kujiona mpweke, aliyetengwa na kuwa na shaka na wasiwasi juu ya usalama wa mtoto wake.
“Kujiona huna thamani na mwenye makosa, kutokuwa makini na kukosa uwezo wa kufanya uamuzi. Kuwa na fikra hasi zikiwamo za kutaka kujiua au kumdhuru mtoto ikiwamo kumuua (hata hivyo ni mara chache mno kina mama wenye tatizo hili huwadhuru watoto wao au wao wenyewe),” anasema.
ATHARI
Daktari huyo anasema dalili hizi zinapokuwapo kwa muda mrefu bila ya matibabu zinaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa mama kumhudumia mtoto au watoto wake.
“Matokeo yake mama anaweza kufikiria kumuua au kuwaua watoto wake na hata kujiua yeye mwenyewe. Fikra hizi husababishwa na hofu na hisia za kutokuwa na uwezo wa kuwahudumia watoto na si kwa sababu ya chuki,” anasema.
NINI HUSABABISHA TATIZO HILI
Anasema chanzo halisi cha tatizo hili hakijulikani ila vipo vitu ambavyo vinahusishwa na kutokea kwake.
Anasema vitu hivyo ni pamoja na mabadililiko ya homoni yanayotokea baada ya kujifungua.
“Kwa kawaida baada ya kujifungua hutokea mabadiliko ya homoni hususani oestrogen, progesterone na cortisol,” anasema.
Anataja sababu nyingine kuwa ni historia ya ugonjwa wa sonona (depression) kabla ya ujauzito, migogoro ndani ya ndoa, kupoteza kazi na kukosa msaada kutoka kwa ndugu na marafiki.
Anasema zipo pia sababu nyinginezo kama vile historia ya kuharibikiwa na mimba au kuzaa mtoto aliyefariki kipindi cha nyuma.
“Mabadiliko yanayotokea baada ya mama kujifungua yanaweza pia kuchangia kutokea kwa tatizo hili. Mabadiliko haya ni pamoja na ya kimwili ambayo humfanya mama ajione tofauti, aliyepoteza mvuto wa kimwili,” anasema.
Anasema sababu nyingine ni uchovu baada ya kujifungua, maumivu yanayotokea katika njia ya uzazi baada ya kujifungua, mawazo ya kukosa uhuru na kujiona aliyefungiwa nyumbani, hali ya kuelemewa na mzigo wa kuwa mama na msongo unaotokana na mabadiliko ya shughuli za nyumbani.
NINI CHA KUFANYA
Daktari huyo anasema mambo yatakamsaidia mama kukabiliana na tatizo hilo ni kukaa karibu na ndugu au marafiki.
“Waombe wakusaidie kumlea mtoto, angalia afya yako, pumzika kadri unavyoweza na ulale pindi mtoto anapokuwa amelala, kujitahidi kukaa na watu waliopo nyumbani, kuepuka kukaa peke yako chumbani na kutafuta muda wa kukaa mke na mume peke yao.
“Mhusika anapaswa pia kujitahidi kuoga na kuvaa nguo kila siku, kutoka nje kwa matembezi, kutembelea rafiki au kufanya kitu anachokipenda. kutafuta mtu wa kusaidia kukaa na mtoto pindi anapofanya yote hayo, ikishindikana kwenda na mtoto,” anasema.
Anaongeza; “Mhusika hatakiwi kujichosha kwa kazi za nyumbani bali kuomba ndugu au marafiki wamsaidie, aongee na mama wengine wenye watoto ili kujifunza kutokana na uzoefu wao.
“Kama tatizo hili litaendelea kwa zaidi ya wiki mbili baada ya kufanya yote hapo juu, ni vizuri kumuona mtaalamu wa afya ya akili au mwanasaikolojia,” anashauri Dk. Swai.
WAKATI GANI UNAFAA KUMUONA DAKTARI
Anasema iwapo mama akiwa na dalili hizo ni vema akaomba msaada wa ndugu aliye karibu au rafiki ili apate msaada wa awali na ikiwezekana apelekwe kuoanana na mtaalamu wa afya.
“Kama atajisikia huzuni kwa zaidi ya siku chache baada ya kujifungua, akiona anashindwa kumudu kazi zake za kila siku, ikiwa ni pamoja na kumhudumia mtoto wake, akishindwa kulala kwa zaidi ya saa mbili kwa siku, akiwa na mawazo ya kujidhuru, kujiua au kumdhuru mtoto, ni vema akaonana na wataalamu wa afya,” anashauri.
MATIBABU
Daktari huyo anasema matibabu ya tatizo hili hutegemea vitu kadhaa ikiwamo ukubwa wa tatizo na hali inayoweza kuchangia kwa tatizo kutokea.
Anasema mtaalamu wa afya ya akili au mwanasaikolojia anaweza kutoa aina mojawapo ya matibabu yafuatayo au kuyachanganya yote kwa pamoja.
“Anaweza kutoa ushauri tiba (psychological help), kupata msaada wa akina mama wengine wenye historia ya tatizo hilo (group therapy), ushauri wa ndoa, iwapo kuna migogoro ya kifamilia au matibabu ya dawa kadri mtaalamu husika atakavyoona inafaa,” anasema.
TATIZO LISIPOTIBIWA MAPEMA NINI HUTOKEA
Anataja athari za kushindwa kukabiliana na tatizo hilo kuwa ni mama kushindwa kumlea mtoto wake ipasavyo hivyo kumfanya ashindwe kukua vizuri kiakili na kimwili, kumuumiza au kumuua mtoto wake, kujiua mwenyewe, uhusiano wa ndani ya ndoa au familia kuvunjika.
“Wakati mwingine mama hushindwa kumudu majukumu yake ya kila siku katika familia au ya kikazi au hupatwa na hali ya kuchanganyikiwa,” anasema.
NJIA ZA KUEPUKA TATIZO HILO
“Kuzungumza na mtu wake wa karibu ili kupata utatuzi wa hali yoyote inayomletea msongo wa mawazo wakati wa ujauzito au mara baada ya kujifungua, kupata muda wa kutosha kupumzika baada ya kujifungua, kuomba msaada pale anapoona anazidiwa na majukumu ya kumlea mtoto au ya kifamilia,” anasema.
Anasema familia na hasa mwenza anapaswa kuwa karibu na mama aliyejifungua hasa katika kipindi cha mwanzoni kwa ajili ya kumpa msaada wowote atakaohitaji ili aweze kupumzika.
“Mama asiwe na mategemeo yasiyo halisia kuhusiana na malezi ya mtoto wake mchanga, ayakubali mabadiliko ya kimaumbile yanayotokea kipindi cha ujauzito na hata baada ya kujifungua na ajiandae na kuyakubali majukumu ya kuwa mama na kuomba msaada pale anapoona ameelemewa,” anasema daktari huyo.