27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Malagashimba apongezwa kwa kuubadilisha Mtaa wa Amani

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Amani uliopo Kata ya Kipunguni Wilaya ya Ilala wamempongeza mwenyekiti wao Daniel Malagashimba, kutokana na juhudi anazofanya za kukarabati barabara ambazo kwa muda mrefu zilikuwa kero.

Miongoni mwa barabara zinazokarabatiwa kwa ushirikiano wa mwenyekiti huyo na wadau wa maendeleo ni ile inayoanzia Kwa Mkolemba – Kwachimwene – Mwakapungu – Bombambili ambazo zinawekwa vifusi katika sehemu korofi.

Barabara za Mtaa wa Amani uliopo Kata ya Kipunguni zikiendelea kukarabatiwa.

Wakizungumza na Mtanzania Digital kwa nyakati tofauti leo Aprili 8, 2022 wananchi hao wamesema ukarabati huo utawezesha barabara hizo kupitika nyakati zote tofauti na ilivyokuwa awali hasa wakati wa masika.

“Huyu mwenyekiti anaacha alama kubwa kwetu kwa sababu barabara zilikuwa mbovu sana na kama ungekuja wakati wa mvua ungejionea mwenyewe jinsi tulivyokuwa tunateseka,” amesema Joseph Simon mmoja wa wakazi wa mtaa huo.

Mkazi mwingine wa mtaa huo Rahma Athumani, licha ya kushukuru kwa ukarabati huo ameiomba Serikali kuingilia kati suala la nauli za pikipiki za miguu mitatu (bajaji) kwani wamekuwa wakitozwa kati ya Sh 500 hadi Sh 700 kutoka Gongolamboto hadi Kwamkolemba.

Naye Malagashimba amesema kero kubwa katika mtaa huo ni barabara na kwamba licha ya ukarabati huo kuleta nafuu lakini bado wanahitaji lami.

“Nimekuwa nikifanya juhudi binafsi kufukia mashimo ili kuisaidia Serikali, natafuta wadau wa maendeleo wanaotuzunguka na mpaka sasa hivi nimemwaga zaidi ya roli 10 kubwa, wadau wananipa vifusi na mimi nanunua mpaka Songas nao wamevutiwa na kuniletea vifusi.

“Viongozi tunatakiwa tuwe wabunifu sio unalalamikia Serikali jiulize wewe umewajibika kwa kiwango gani, kama leo nimekesha usiku nasimamia umwagaji vifusi,” amesema Malagashimba.

Aidha amesema barabara ya Kwadiwani hadi Kwamkolemba Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) wameanza kuikarabati.

Amesema pia wamekarabati kivuko cha Shule ya Msingi Kipunguni na hivi sasa kinapitika vizuri.

Mbali na miundombinu ya barabara mwenyekiti huyo pia amefanikiwa kujenga ofisi kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo akiwemo mzee Dankan Mwaisumo aliyetoa kiwanja.

Amesema walianza kazi bila kuwa na ofisi ambapo walifadhiliwa na mmoja wa wananchi aliyewapa vyumba viwili.

“Ofisi hii imepatikana kutokana na biashara yangu ya utalii na kushirikiana na wadau wangu wa maendeleo na wananchi ambao walishiriki kwa kuchimba msingi, kubeba tofali na wengine kumsaidia fundi kuchota maji. Tuna mitaa 159 na mingi haina ofisi hivyo, kwa kujenga ofisi nimeipunguzia mzigo Serikali wa kulipa kodi,” amesema Malagashimba.

Mwenyekiti huyo pia ameajiri mgambo ambaye anamlipa mwenyewe ili kuimarisha ulinzi na usalama huku huduma za barua za utambulisho wa makazi na dhamana zikitolewa bure bila kuwatoza wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles