27.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

Makamba, Kinana, Membe njiapanda

Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

HATUA ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekeza makatibu wakuu wawili wa zamani wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na Mzee Yusuf Makamba lakini pia Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani, Bernard Membe waitwe na Kamati ya Usalama na Maadili ya Taifa ya chama hicho ili wajibu tuhuma za kimaadili zinazowakabili ni wazi sasa inawaweka mtegoni.

Wafuatiliaji wa masuala ya siasa wanasema hatua ya makada hao kufikishwa kwenye kamati hiyo inawaweka kwenye hatari ya ama kulazimishwa kuomba radhi  baada ya kushindwa kufanya hivyo mapema au kupewa adhabu yeyote na adhabu ya juu kabisa ni kuondolewa ndani ya chama hicho kikongwe. 

Lakini wanasema hayo yote yatategemea na namna wao wenyewe watakavyoweza kujitetea.

Akizungumza na Mtanzania Jumapili  Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)  Dk Muhidin Shangwe alisema kuwa makada hao wana wakati mgumu ingawa wanachoiitiwa kuhojiwa bado ni tuhuma.

“Wameitwa kwa tuhuma za kimaadili, hatua hiyo inaweka katika wakati mgumu, hata wakihojiwa na wasikutwe na hatia lakini bado umma umefahamu kuwa waliitwa katika kamati ya maadili.

“Lakini pia watakuwa na wakati mgumu wakikutwa na hatia kwani CCM ni taasisi ambayo wameitumikia kwa muda mrefu, lakini yote kwa yote tunasubiri matokeo ya  baada ya kuhojiwa, kwa kuwa kila taasisi ina namna yake ya kutoa adhabu kwa wanachama wake” alisema.

Rais Dk. John Magufuli mwenyewe wakati akizungumzia alivyoombwa radhi na Mbunge wa Bumbuli January Makamba  na William Ngeleja wa Sengerema kabla ya Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye naye hajajitokeza  alitamka bayana kwamba iwapo wangepelekwa kwenye Kamati ya Siasa ya Kamati Kuu wangepewa adhabu kubwa taswira ambayo sasa inaonekana kwa Makamba, Kinana na Membe.

Kwa maneno yake mwenyewe Dk. Magufuli wakati akitoa kauli ya kuwasamehe January na Ngeleja alikaririwa akisema;

“Kuna watu fulani walinitukana wee na ‘nika-prove’ (nikathibitisha) kwamba sauti zile ni zao ‘more than one hundred percent’ (zaidi ya asilimia 100), nikawa nakaa nafikiria, nikasema hawa wakipelekwa kwenye Kamati ya Siasa ya Central Committee adhabu itakuwa kubwa”.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari juzi jioni na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, ilieleza kuwa azimio la kuwaita Kinana, Mzee Makamba na Membe lilifikiwa kwa kauli moja na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichoketi Ijumaa Jijini Mwanza chini Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli.

Ingawa taarifa hiyo haikubainisha tuhuma za kimaadili zinazowakabili makada wake hao zaidi ya kuelekeza waitwe na kuhojiwa kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho na Kanuni ya Maadili na Uongozi, msingi wa yote unaweza kuwa ni sakata la waraka wa makatibu hao kwenda kwa Baraza la Wazee wa CCM na sauti zao za simu kuvuja. 

Kumekuwa na maneno mengi na hata sintofahamu ya uanachama wa Kinana, Mzee Makamba na Membe tangu lizuke sakata la kusambaa kwa sauti zinazosemekana kurekodiwa kupitia mazungumzo ya simu wakidaiwa kumsema vibaya Rais Magufuli na kabla ya hapo waraka waliouandika makatibu wakuu hao wawili wa zamani.

Takribani miezi miwili iyopita, Rais Magufuli alitangaza kuwasamehe baadhi ya waliomsema vibaya kupitia mazungumzo hayo baada ya kumwomba radhi.

Aliotangaza kuwasamehe ambao pia ni wabunge na majimbo yao kwenye mabano ni January Makamba (Bumbuli),  William Ngeleja (Sengerema) na baadae Nape Nnauye (Mtama) ambaye alimfuata Ikulu, Dar es Salaam.

Jana katika taarifa yake Polepole alisema Halmashauri Kuu ya Taifa pia ilipokea, kujadili na kuridhia kwa kauli moja taarifa ya Kamati ya Usalama na Maadili juu ya uamuzi wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli  wa kuwasamehe January, Nape na Ngeleja walioomba radhi kwake baada ya kukiri mbele yake kufanya makosa ya kimaadili yaliyokidhalilisha chama na viongozi wake mbele ya umma.

Aidha Polepole alisema kikao hicho kimewataka wanachama hao kujirekebisha na kutorudia makosa yao ama sivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao kwa mujibu wa katiba, kanuni na taratibu za CCM ikiwamo kufukuzwa uanachama

HAWAJAWAHI KUOMBA RADHI

Wakati January, Nape na Ngeleja wakiomba radhi na hata Halamshauri Kuu ya CCM kutangaza kwa kauli moja  kuridhia msamaha wao sasa, Kinana, Mzee Makamba na Membe hawajawahi kumwomba radhi Rais Magufuli licha ya sauti zao kudaiwa kusikika katika mazungumzo hayo.

Wakati Membe akiwa amepata kuzungumza na gazeti hili la MTANZANIA Jumapili kuhusu msimamo wake wa kuomba radhi akihoji kosa lake, na Mzee Makamba akikataa kuzungumza lolote, Kinana kwa upande wake hajapata kusikika akizungumza lolote kuhusu sakata hilo.

Baada ya Halmashauri Kuu  kuelekeza makada hao waitwe kuhojiwa na Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM, jana Membe alikaririwa na baadhi ya magazeti akisema kuwa;

 “Nimepata habari hiyo ninasubiri kwa hamu kubwa sana barua ya wito wa kikao hicho”.

Kwa upande wake Mzee Makamba naye alikaririwa akisema kuwa; “Sijapata huo wito nikipata nitazungumza.  

KUSAMBAA KWA SAUTI 

Itakumbukwa kuwa Julai mwaka huu sauti zinazodaiwa kuwa ni za January, Nape na makatibu wakuu wastaafu hao wa CCM, Makamba na Kinana zilisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ambapo pamoja na mambo mengine walisikika wakizungumzia kuandaa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwa makatibu wakuu hao wastaafu.

Siku chache baadaye ikasambaa sauti nyingine ya mawasiliano kati ya Nape na Ngeleja kisha kufuatiwa sauti inayodaiwa kuwa ni ya Membe na Katibu Kata wa Kijiji cha Rondo mkoani Lindi.

TAARIFA YA KINANA, MAKAMBA

Kusambaa kwa sauti hizo kulitanguliwa na tukio la Julai 14 mwaka huu ambapo wazee hao waliandika taarifa kwa Baraza la Wazee wa CCM wakilalamikia mambo mbalimbali ikiwamo kudhalilishwa kwa mambo ya uongo na mtu anayejitambulisha kama mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.

Waraka huo unaodaiwa kuandaliwa kwa ushirikiano wa Nape na Januari pia ulisambazwa katika mitandao ya kijamii.

Katika taarifa hiyo viongozi hao walidai kuwa wamezingatia Katiba ya CCM toleo la mwaka 2017 ibara ya 122, na mwaka waliwasilisha maombi yao wakiwasihi wazee hao wa chama watumie busara zao kushughulikia jambo hilo ambalo walidai kuwa linaelekea kuhatarisha umoja, mshikamano na utulivu ndani na nje ya chama.

Pia walidai kuwa wametafakari kwa kina kabla ya kutoa taarifa kuhusu kile walichodai kuwa ni uzushi na kwamba mara kwa mara Watanzania wamekuwa wakijiuliza kwamba mtu huyo anatumwa na nani.

“Pili anakingiwa kifua na nani? Tatu anatumika kwa malengo gani? Na nne nini hatima ya mikakati yote hii.

“Tafakari yetu inatupeleka kupata majibu yafuatayo; kwanza kwa ushahidi wa kimazingira mtu huyu anatumwa na kutumiwa na watu wenye uwezo wa kumlinda na kumkingia kifua bila kuhojiwa na taasisi yoyote wala mtu yeyote.

“Pili zipo ishara kwamba watu hawa wanaomkingia kifua wana mamlaka, baraka na kinga ambazo wamepewa ili kutekeleza majukumu maalumu kwa watu maalumu na kwa malengo maovu,”  ilieleza taarifa yao hiyo.

Katika hoja nyingine walidai kuwa mtu huyo anatumika kwa malengo ya kuwazushia, kuwakejeli, kuwavunjia heshima, kuwatia hofu na kuwanyamazisha viongozi, taasisi na watu ambao ni walengwa waliokusudiwa.

Jingine ni kwamba kuna kila dalili kuwa lengo na hatima ya mkakati huo ni kuandaa tufani ya kuwahusisha walengwa, wastaafu na walio kazini katika nafasi mbalimbali na matendo ya kihalifu, kimaadili na kihaini ili kuhalalisha hayo wanayokusudia kuyafanya.

“Tumeamua kutochukua hatua za kisheria kwa sasa kwa sababu kwanza jambo hili lina taswira ya kimkakati na lina mtandao wenye malengo ya kisiasa. Kwa hiyo linapaswa kushughulikiwa kisiasa. Pili, unapochafuliwa, unachokwenda kudai mahakamani ni fidia. Kwetu sisi, heshima yetu haiwezi kuthaminishwa na fidia,” walieleza kupitia taarifa hiyo.

Kuhusu tuhuma zilizokuwa zikielekezwa kwao na mwanaharakati huyo walisema wanaamini kuna sehemu zinatoka na kwamba anatumwa kutekeleza maagizo na kutumika kama kipaza sauti tu. 

Taarifa hiyo ilidai kuwa mara ya kwanza walizushiwa kuwa wanamkwamisha Rais Dk. Magufuli kutekeleza majukumu yake jambo ambalo walilipuuza kwa imani kwamba viongozi wao watayaona kwa namna yalivyo kuwa haiwezekani washiriki kuihujumu Serikali ya chama walichokitumikia maisha yao yote.

Iliongeza kuwa mara ya pili walizushiwa kuwa wanataka kumhujumu Rais ili asipitishwe na CCM kutetea urais mwaka 2020.

“Katika utumishi wetu, tumesimamia michakato ya kupitisha wagombea wa nafasi ya urais na nyinginezo tuhuma hizo ni uzushi uliosukwa kwa malengo maalumu na kwamba msingi wa tuhuma zote mbili ni hofu.

Kauli ya Msekwa

Hata hivyo Katibu wa Baraza la Wazee wa CCM, Spika Mstaafu Pius Msekwa alijibu hoja hizo  na kusema kwamba  Katiba ya CCM imekipangia kila kikao cha chama kazi za kufanya, na kwamba kazi za baraza hilo zimetajwa na kuainishwa katika Ibara ya 127 (3), Toleo la 2012, kuwa ni kutoa ushauri kwa chama na kwa Serikali zinazoongozwa na chama hicho.

 Msekwa alisema kikatiba baraza halikupewa mamlaka ya kutenda kazi hizo ambazo ni za kiuendeshaji badala yake jukumu hilo limetolewa kwa vikao vingine ambavyo ni vya viongozi walioko madarakani.

Hata hivyo Msekwa aliwatahadharisha Kinana na Makamba kutoruhusu machungu ya tuhuma hizo yakawasahaulisha misingi ya chama hicho, wakashawishika kutafuta njia za mkato za kuyashughulikia ambazo zinakiuka katiba yake.

Kutenguliwa uteuzi wa January

Ikiwa ni siku chache baada ya sauti hizo kusambaa, Julai 21 mwaka huu Rais Dk. Magufuli alitengua uteuzi wa January kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na nafasi yake hiyo kuchukuliwa na Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene.

Wakati akimwapisha Simbachawene Dk. Magufuli alizitaja sababu za kutengua uteuzi wa January kuwa ni pamoja na kutotekelezwa kwa wakati kwa katazo la mifuko ya plastiki na kutotumika vizuri kwa fedha zinazotolewa na wafadhili kwa miradi ya mazingira.

Hata hivyo baada ya mabadiliko hayo January kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter alieleza kuwa ameupokea kwa moyo mweupe uamuzi huo ambapo alimshukuru Rais kwa kumwamini kushika nafasi hiyo.

“Neno la mwisho kwenye hili; Namshukuru Rais kwa kuniamini, Makamu wa Rais kwa kunielekeza, PM (Waziri Mkuu) kwa kunisimamia na timu ya Ofisi ya Makamu wa Rais, NEMC na mawaziri wote kwa ushirikiano,” aliandika January.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles