25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

Makamba ajionea athari za bomoabomoa

makambajpg*Asema hakuna mwananchi atakaye nyanyasika

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano, Mazingira), January Makamba, amefanya ziara na kujionea namna wananchi waliobomolewa nyumba zao wanavyoishi kwa kukosa makazi.

Kutokana na hali hiyo, amesema  hakuna mwananchi anayeonewa au anayeteseka na kunyanyasika katika kazi ya kuwaondoa wakazi wanaoishi katika Bonde la Msimbazi ila kazi hiyo inafanyika kwa mujibu wa sheria.

Hayo aliyasema  jijini Dar es Salaam jana, baada ya kuwatembelea wananchi wa maeneo mbalimbali ambao nyumba zao zimebomolewa na nyingine kuwekewa alama ya X kwa ajili ya kubomolewa.

Katika ziara hiyo, Makamba alijionea hali mbali ya uchafuzi wa mazingira hasa katika maeneo ya Kigogo,Mburahati na na Kinondoni Mkwajuni.

Akizungumza na wananchi wa maeneo hayo, Makamba alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuendelea kuwaona wananchi wanakufa kila mwaka kutokana na mafuriko na wengine wanaishi katikati ya bonde na kwenye kingo za mito, huku wakielekeza majitaka yao kwenye mito na mifereji.

Alisema kazi ya kuondoa wakazi itazingatia misingi ya ubinadamu.

“Hakuna mtu atakayekurupushwa na kubomolewa nyumba anayoishi bila yeye na Serikali kuthibitisha kama hakumilikishwa kiwanja au nyumba, na kwamba anapoishi hapastahili kwa makazi na shughuli za binadamu.

“Mtu yeyote ambaye amemilikishwa eneo na Serikali na amepewa kibali cha ujenzi, hataondolewa hadi atakapopewa kiwanja mbadala, ila Serikali yetu inataka sheria zifuatwe lakini pia ina sura ya kibinadamu,” alisema January.

Akiwa katika eneo la Kinondoni Mkwajuni, Waziri Makamba alikagua uzoaji wa kifusi kilichotokana na ubomoaji wa nyumba zilizokuwa katika bonde hilo.

“Tunataka eneo hili liwe safi kabisa ili tuonyeshe mfano wa maendelezo bora na rafiki kwa mazingira ya maeneo ya mabondeni,” alisema .

Akiwa katika eneo hilo,alikutana na wananchi ambao waliomba ufafanuzi kuhusu kero mbalimbali wanazozipata.

Alisema Serikali imeomba taarifa kupitia mamlaka za Serikali za mitaa kuhusu watu wote wenye kuhitaji msaada maalumu wa kibinadamu na jitihada zitafanyika ili kuweza kuwasaidia watoto waliokuwa wanaishi mabondeni kuhamishiwa katika shule nyingine.

Kutokana na hali hiyo, January alitoa siku saba kwa viongozi hao kuhakikisha mito hiyo inakuwa safi kwa kuwashirikisha wananchi kufanya usafi na kuomba halmashauri husika zitoe magari.

Alisema iwapo viongozi hao watashindwa kutekeleza agizo hilo, basi kibarua chao kitakuwa shakani, ni pamoja na kuwawajibisha kwakuwa wamechangia uchafuzi wa mazingira.

Alisema Benki ya Dunia na serikali ya Marekani zimetoa Sh bilioni 100 kwa ajili ya kusafisha mito na kuijengea ili ipitishe maji kwa mtiririko ambao hautasababisha mafuriko.

“ Hali hii inatisha, haiwezekani kiongozi wa mtaa unaongoza wananchi katika eneo chafu hivi, ninaondoka leo (jana), Jumapili ijayo nakuja, kama nitakuta hivi, kazi utakuwa huna leo na kusamehe…itisha mkutano panga wananchi wako,mfanye usafi,” aliagiza Januari.

Bomoabomoa jijini Dar es Salaam ilianza Desemba 17, mwaka jana ambapo hadi sasa tayari nyumba kadhaa  zimebomolewa na nyingi zimewe kuwekewa alama ya X.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,750FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles