22.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Waliosoma Tanga School wanavyoimulika shule yao

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Historia ya shule za sekondari Tanzania haiwezi kukamilika bila kuitaja Shule ya Sekondari ya kwanza Tanganyika maarufu Tanga School.

Shule hiyo ilijengwa na Wajerumani mwaka 1895 eneo la Mkwakwani jijini Tanga ikiwa ni kituo cha elimu kwa vijana wa kiume na mafunzo ya ualimu na baadaye mwaka 1905 iliidhinishwa rasmi kuwa shule ya sekondari.

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Umoja wa Wanafunzi waliosoma Tanga School (TSAA).

Mwalimu na mwanafunzi wa zamani wa Tanga School, Zuberi Mohamed, anasema mwaka 1966 Serikali ya Tanganyika ilijenga shule kubwa zaidi eneo la Makokora mjini Tanga na kuhamishia wanafunzi wote toka Mkwakwani kwenda Makorora na kuendelea na elimu ya sekondari kwa wavulana pekee.

“Mwaka 1968 ndipo Tanga School ilianzisha elimu ya kidato cha tano na sita kwa wavulana pekee, mwaka 1972 shule ilibadilishwa na kuwa seondari ya ufundi kwa wavulana pekee.

“Mwaka 1988 Serikali ya Tanzania ilianzisha masomo ya sekondari ya ufundi kwa wasichana na kuifanya shule kuwa ya jinsia mchanganyiko baada ya ujenzi wa mabweni mapya ya wasichana…mpaka sasa imekuwa shule ya wanafunzi mchanganyiko,” anasema Mwalimu Mohamed.

Shule hiyo imekuwa na umaarufu mkubwa nchini kwani mihimili yote ya nchi imewahi kuongozwa na Watanzania waliosoma Tanga School akiwemo Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete ambaye alisoma kati ya mwaka 1970 – 1971.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Tanga, MacMaster Luzilo, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Umoja wa Wanafunzi waliosoma Tanga School (TSAA).

Wengine waliosoma shule hiyo na nafasi walizoshika kwenye mabano ni Chifu Erasto Mang’enya (Spika wa Bunge la Tanzania), Amir Manento (Jaji Kiongozi mstaafu), Fakihi Jundu (Jaji Kiongozi mstaafu), January Msofe (Jaji wa Mahakama ya Rufaa mstaafu), Hamisi Semfuko (Meja Jenerali mstaafu), Injia Ramadhani Mwikalo (Mtaalamu aliyekuwa akiongoza mitambo ya Satelite Marekani), Haroun Madofe (Mkuu wa Chuo cha IFM mstaafu) na Mwanariadha mkongwe, Juma Ikangaa.

Oktoba 29,2023 wanafunzi hao waliungana na kuzindua Umoja wa Wanafunzi Waliosoma Tanga School (TSAA) ambao unawaunganisha waliosoma kuanzia miaka ya 1960 mpaka sasa.

Mwenyekiti wa TSAA, Meja Jenerali mstaafu, Hamisi Semfuko, anasema wanalenga kuieneza historia ya elimu ya sekondari nchini kupitia shule hiyo ya kihistoria iliyoasisiwa enzi za utawala wa Wajerumani.

“Umoja huu umelenga kuunganisha nguvu na kuweka jitihada za pamoja katika kuboresha kiwango cha taaluma kwenye shule hiyo ikiwa ni dhamira ya kuifanya shule kuendelea kutoa wanafunzi bora kitaaluma ili watoe mchango mkubwa katika kulijenga taifa.

“Mafanikio ya jambo hili ni zawadi kubwa kwa kizazi kijacho na taifa letu na sio kwa Tanga School pekee. Dhamira yetu ya kwenda kuanzisha maktaba ya kimtandao inalenga kuboresha kiwango ha ufaulu na ni chachu ya mageuzi makubwa ya maboresho ya miundombinu kulingana na kasi ya teknolojia ya sasa,” anasema Meja Jenerali Semfuko.

Anasema maktaba hiyo itawaondolea wazazi gharama ya kutafuta vitabu na kupanua wigo wa wanafunzi kupata taarifa mbalimbali za kitaaluma.

Mlezi wa umoja huo, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete anasema wamedhamiria kuboresha kiwango cha elimu na mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule hiyo ili iwe miongoni mwa shule bora kitaifa.

“Tunaamini sisi ambao tumebahatika kupata elimu pale tunao mchango kwa ajili ya maendeleo ya shule yetu, hatuna uwezo mkubwa lakini kuna ambacho tunaweza kuchangia.

“Focus yetu kubwa tunataka Tanga School iingie kwenye hesabu ya shule bora zenye ufaulu wa hali ya juu, kama wenzetu wanatajwa na sisi tunaweza kutajwa…haiwezekani shule ya kwanza nchini lakini imepotea kabisa watu hawaijui,” anasema Kikwete.

Baadhi ya viongozi waliowahi kusoma Tanga School.

Mkuu wa Shule hiyo, MacMaster Luzilo, anasema wameweka mikakati ya kuhakikisha shule hiyo inaingia kumi bora kitaifa.

Anasema shule hiyo kwa sasa ina wanafunzi 1,126 wakiwemo 163 wenye mahitaji maalumu.

Hata hivyo anasema inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa walimu wa ufundi, sayansi, hisabati na elimu maalumu.

“Karakana zimechoka na zingine zilibadilishwa matumizi, pia nyumba za walimu zimechakaa na tuna upungufu wa kompyuta,” anasema Mwalimu Luzilo.

Katibu wa umoja huo Godwin Mbaga, anasema wanatarajia kuwaunganisha watu wote waliosoma Tanga School kuanzia miaka ya 1960 mpaka 2022 kwa lengo la kuieneza historia ya elimu ya sekondari nchini kupitia shule hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles