23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Viboko shuleni sio ‘Mwalimu’

*Unahitajika utafiti kuhusu adhabu ya viboko

*Walimu washauriwa kufikiria nje ya viboko

Na Samwel Mwanga, Mtanzania Digital

ADHABU ya viboko bado inaendelea kutumika katika shule za Msingi na Sekondari nchini Tanzania.

Kuendelea kutumika kwa adhabu hiyo kunatokana na kuwa ni miongoni mwa kanuni zilizotungwa na Serikali ambayo inajulikana kama The Education (Corporal Punishment) Regulation G. N. 294 ya mwaka 2002.

Kanuni hizi zinatoa mwongozo ni wakati gani adhabu ya viboko inatakiwa kutolewa na kwa kiwango gani.

Wanafunzi wakiadhibiwa kwa viboko,

Kanuni ya 3 (1) inasema “Adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhamu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima. Kanuni ndogo ya (2) inasema adhabu ya Viboko itatolewa kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi na isizidi viboko vinne (4) kwa tukio lolote”.

Sheria hiyo imempa Mwalimu Mkuu wa shule husika mamlaka ya kutoa adhabu ya viboko au kukasimisha mamlaka yake kwa umakini mkubwa kwa mwalimu yeyote kutoa adhabu hiyo.

Mwalimu anayechaguliwa kutoa adhabu atakuwa na mamlaka ya kutoa adhabu pale tu atakapopata idhini ya mwalimu mkuu katika tukio husika.

Aidha, kanuni ya (5) inataka kila adhabu ya kiboko inayotolewa kwa mwanafunzi kumbukumbu ya kutolewa kwa adhabu hiyo sharti iwekwe kwenye kitabu, ikitaja jina la mwanafunzi, kosa alilolifanya, idadi ya viboko na jina la mwalimu aliyetoa adhabu na kumbukumbu hizo lazima zisainiwe na mkuu wa shule.

Kwa sasa adhabu hiyo imekuwa ikipigiwa kelele na wadau wengi wakiwemo wa ambao wanasimamia haki za watoto wakidai kuwa ni adhabu ya kikatili ambayo haisaidii kumwadabisha mtoto.

Walimu na wazazi au walezi wanapaswa kujua kuwa kumfunza adabu mtoto siyo kutumia viboko bali kumuelimisha lipi la kufanya na lipi la kuacha.

Kwa mfano shuleni kuna kazi nyingi ambazo unaweza kumpa mtoto kama adhabu, kazi kama kumwagilia maji bustani ya  maua, kufagia darasa, kusafisha choo au ofisi za walimu ni adhabu tosha kwa wanafunzi, hii ni kwa sababu kwanza unakuwa umemwadhibu na hivyo kumuadabisha na pili unamfundisha kufanya kazi.

Hali hii hufanya mwanafunzi kujitahidi kusoma kwa bidii ili kuepuka adhabu toka kwa walimu wake.

Chanzo cha Utoro…

Njile Masunga(13) ni mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya Msingi Ng’hami wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu amekuwa mtoro kutokana na kukimbia adhabu ya viboko inayotolewa na walimu shuleni kwao.

Mwanafunzi huyo hajimudu vizuri katika somo la Hisabati, hivyo mara nyingi kila likitokea zoezi la somo hilo darasani daftari lake huwa na makosa mengi hali ambayo husababisha mwalimu wa somo hilo kumchapa viboko na matokeo yake ameamua kuacha shule na kusisitiza iwapo viboko shuleni vitafutwa atarejea shuleni.

“Mimi somo la hisabati kwa kweli uwezo wangu ni mdogo sasa kila zoezi likitolewa nakosa hesabu nyingi, mfano katika ya hesabu 10 nakosa nane na hapo mwalimu kila kosa unachapwa kiboko kimoja, kwa msingi huo niliona siwezi kuvumilia nikaona bora niache shule labda viboko shuleni vikifutwa naweza kurudi shuleni,”a nasema Mwanafunzi huyu.

Mwanafunzi huyu kutokuwepo shuleni ni matokeo ya adhabu za viboko ambazo sio tu humjengea mtoto chuki dhidi ya walimu wake au walezi wake bali pia humnyima haki yake ya elimu na malezi bora.

Wazazi/Walimu

Baadhi ya wazazi na walimu walikuwa na maoni  juu ya jambo hili ambapo wengi wao wanasema kuwa viboko shuleni havimjengi mtoto bali vinamfanya kuwa sugu.

Paulina Paul ni Mwalimu wa shule ya msingi Mwaliga katika wilaya ya Maswa mkoani Simiyu ambapo anasema kuwa haoni sababu ya kumchapa viboko mtoto kama njia ya kumuadabisha, kwanza kwa kile anachoamini kwamba kwanza mtoto anakuwa sugu kwa kuwa kila atakapofanya kosa anajua atachapwa tu na hivyo ataendelea kurudia kosa lilelile.

Vile vile mwalimu huyo ameendelea kueleza kuwa baadhi ya walimu wana hasira, hivyo huweza kumchapa mtoto katika hali ya hasira na hatua inayoweza kumsababishia maumivu makali au hata majeraha makubwa.

“Lengo la adhabu ni kumkanya au kumfunza mtoto aone kuwa yale aliyoyafanya siyo mazuri hivyo basi nashauri kuwa mtoto apewe adhabu kama za kusafisha darasa, kumwagilia na kadhalika,” anasema Mwalimu Paulina.

Upande wake, Jesca Michael ambaye ni Mzazi wa Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Mwanyahina iliyoko wilayani Meatu mkoani Simiyu anasema kuwa kama mtoto hamudu somo au masomo fulani, atafutiwe mwalimu wa kumsaidia pia kuwepo mawasiliano ya mara kwa mara kati ya walimu na wazazi au walezi wa watoto ili kuweza kutatua tatizo hilo.

Ushauri…

Aidha, Mwalimu Paulina anashauri kuwa kama mwanafunzi amechelewa kufika shule asubuhi basi anaweza kuadhibiwa kwa namna nyingine na si kwa viboko.

“Mfano mwanafunzi kama amechelewa kufika shule basi anaweza kuadhibiwa kwa kupewa adhabu ya kubaki shuleni na afanye adhabu aliyopewa, kesho yake lazima atawahi tu shuleni na atafanya vizuri zaidi,”anashauri Mwalimu Paulina.

Jesca anashauri kwa kusema kuwa, mtoto kwanza apewe mapenzi na malezi bora kutoka kwa wazazi wake, anapofanya kosa, wazazi waangalie na waupime uzito wa kosa, kabla ya kutoa adhabu kali.

“Badala ya kumchapa viboko mtoto, mwambie sitakununulia nguo ya sikukuu au mwambie ukiwa wa kwanza darasani nitakununulia nguo nzuri, viatu vizuri au hata baiskeli, mtoto akishafikiria vitu vyote hivyo vizuri, atajihidi asifanye makosa kuanzia nyumbani mpaka shuleni,”anashauri mzazi huyo.

Sylvester Kasulumbayi ambaye ni mlezi wa wanafunzi katika shule ya sekondari Ipililo iliyoko wilayani Maswa anasema kuwa kwa sasa tunarudi nyuma miaka 60 badala ya kwenda mbele.

Anafafanua zaidi kuwa kuna watu wengi akiwemo yeye ambao hawaamini kuwa kumchapa mwanafunzi kiboko ni kumsaidia kujenga nidhamu na kujituma.

“Tunarudi nyuma miaka 60 badala ya kwenda mbele kuna watu wengi kama mimi tusio amini, kuwa kumchapa mwanafunzi kiboko au viboko shuleni ni kumsaidia kujenga nidhamu na kujituma.

“Kinyume chake, kama ni nidhamu, utamjengea nidhamu ya woga na kufanya yale ambayo anadhani unataka ayafanye na si kuwa ayafanye kwa faida yake na jamii hapo baadae.

“Viboko vinamfanya mwanafunzi asijiamini na hata akose uwezo wa kudadisi, mimi nakumbuka nikiwa shule ya msingi miaka ya nyuma ilinitokea nikachapwa fimbo darasani kwa kosa la kumdadisi sana mwalimu wangu wa Jiografia sababu nilitaka kupata ufahamu zaidi lakini mwalimu aliniona nimekosa nidhamu,” anasema Sylvester.

Kipi kifanyike…

Ikumbukwe kwa mwanafunzi au wanafunzi kukosa nidhamu na kutokufanya vizuri kwenye masomo inachangiwa na mambo mengi tuanze kuyaangalia hayo kwanza kabla hatujawahamasisha walimu wakate fimbo na kuwachapa watoto wetu.

Kwani kama tunavyofahamu kwamba viboko havifundishi zaidi ya kumpatia mwanafunzi maumivu na kusababisha aichukie shule. Waelimishwe kwa kuelekezwa lakini wakiendelea kukiuka, wapewe adhabu za kufanya kazi mbalimbali.

Hivyo, ni vizuri kwa walimu kuwa karibu zaidi na watoto au wanafunzi wao ili wajue tatizo ni nini hasa ambalo linawafanya wasizingatie masomo yao vizuri au kutokuwa na nidhamu huenda tatizo ni la Kisaikolojia kutokana na malezi anayoyapata nyumbani, labda kulelewa na mama wa kambo au mtu baki.

Kama matatizo yanatokana na malezi ya nyumbani jaribu kuwasiliana na wazazi/ walezi wake ili ujue ni jinsi gani utamsaidia mtoto huyu badala ya kutumia viboko.

Na kwa upande wa nyumbani, wazazi na walezi wajaribu kuwa karibu na watoto wao na wanapofanya makosa wawaonye kwanza kwa maneno usitangulize viboko, kwani ataona hakuna tofauti kati ya nyumbani na shuleni.

Jamii yoyote ambayo walezi wake wamebobea katika kuelekeza watoto kupima athari za matendo yao kabla ya kutenda na kufundisha maadili ya akili kuliko maadili ya kuachana na ngono: mfano kufundisha matumizi bora ya muda, matumizi ya pesa, umuhimu wa kufanya mambo kwa tija, umuhimu wa kusikiliza sauti za nafsi zao na wenzao pamoja na Mungu itaweza kufanikiwa sana bila viboko.

Lakini Kwa hali tuliyofikia viboko siyo suluhisho hivyo ni vizuri kwa serikali kufanya utafiti upya juu ya adhabu ya utoaji wa viboko shuleni kwani kumekuwa na kesi nyingi ambapo adhabu hiyo inayotolewa shuleni imesababisha vifo au majeraha makubwa yasiyofutika kwa mtoto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles