24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Uzazi wa mpango siyo dhambi- Viongozi wa Dini

*Washauri wananchi kutopumbazwa na uzushi

Damian Masyenene, Mtanzania Digital

Baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mwanya wa maandiko matakatifu kupotosha wengine na kuamini kuwa dini haziruhusu uzazi wa mpango na wanaouhamasisha wanakwenda kinyume na maagizo ya Mwenyezi Mungu aliyeagiza wanadamu wazae na kuijaza nchi.

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke.

Imani za namna hiyo zimekuwa zikirudisha nyuma jitihada za serikali na wadau mbalimbali katika kuikomboa jamii kutoka kwenye tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi, umaskini uliokithiri, uharibifu wa mazingira na utegemezi mkubwa huku ikilenga kuleta ustawi wa familia na taifa.

Kufuatia upotoshaji huo na matumizi yasiyofaa ya imani za dini, baadhi ya viongozi wa dini waliozungumza na Mtanzania Digital jijini hapa wametoa ufafanuzi na kueleza umuhimu wa kupanga uzazi, malezi na uzazi salama huku wakiwataka wananchi kurejea kwenye maandiko matakatifu kujiridhisha vyema na maagizo ya Mwenyezi Mungu.

Mchungaji wa Kanisa la EAGT Mwanza, Dk. Jacob Mutashi ambaye pia ni mwalimu wa ndoa na vijana amesema kuwa hawapingani na uzazi wa mpango kwa sababu mtu akizaa watoto nje ya utaratibu wa kumzidi uwezo atasababisha wakose malezi mazuri, lishe bora, malezi, elimu na kucheza ambapo waumini wameaswa kutopuuzia jambo hilo na wazingatie kupata watoto kadri ya uwezo wao kiuchumi.

“Tunashukuru serikali inaboresha elimu ya afya na tunaunga mkono kukiwa na spacing (muda wa kupangilia uzazi) uwezo wa wazazi unakuwa mzuri kupangilia mambo yao vizuri, mtu akizaa kwa mpango siyo vibaya isipokuwa utaratibu unaotumika kwenye njia hizo za uzazi wa mpango uwe salama,” amesema Dk. Mutashi na kuongeza

“Ile lugha ya kwamba kila mtoto ana riziki yake hapa duniani siiungi mkono kwa sababu mzazi lazima ajipange hivyo kuzaa kwa mpango ni muhimu sana, Mwenyezi Mungu alipoagiza tuzae tukaijaze nchi hakumuambia mtu mmoja tuliambiwa wote siyo kufanya mashindano ya kuijaza mwenyewe unakuwa na mapato kiduchu wakati walaji wanaongezeka utaingia kwenye madeni na maisha mabaya,” alisisitiza Mchungaji huyo.

Kwa upande wake, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke amesema dini ya kiislam inafundisha malezi na uzazi salama kupitia elimu ya unyonyeshaji huku akibainisha kuwa uzazi salama na uliokamilika utaepusha mimba za mara kwa mara na kuwa na uwezo wa kumhudumia mtoto ambapo waumini wa dini wanapaswa kurejea kwenye maandiko matakatifu na kupata elimu kuliko kukubali kupofushwa macho na uzushi wa watu wengine.

“Mfano kwenye uislamu tumefundishwa utaratibu mzima wa mwanamke kubeba mimba mpaka kumzaa mtoto na elimu ya unyonyeshaji kwamba mtoto anapaswa kunyonya kwa miaka miwili kwahiyo tunaamini ndani ya kipindi hicho ndani yake kuna mambo mbalimbali ya manufaa na baraka kwa mtoto huyo.

“Kwahiyo ukiliangalia vizuri jambo hili la uzazi salama ndani yake liko hivyo, fikiria una mke kila mwaka ana mimba inamaana utakuwa umekiuka utaratibu wa kumwezesha mtoto kunyonya kwa kipindi cha miaka miwili na mzazi utakuwa umemdhulumu,” amesemaSheikh Kabeke ambaye pia Mwenyekiti mwenza kamati ya amani ya viongozi wa dini mkoani humo.

Kwa upande wake, muumini wa kanisa la Waadventista Wasabatho jijini hapa, Janeth Gakwandi alisema uzazi wa mpango hauna shida yoyote na wala hausiani na imani bali ustawi wa mtu, jamii na taifa kwani ni jambo lenye heri ambalo faida zake ni nyingi kuliko hasara.

“Huwezi kusema dini inakataza alafu baadaye unakuwa na utitiri wa watoto unakwenda kanisani kuomba msaada wa chakula na mavazi ya watoto, ukizaa bila mpangilio ni ngumu kwa mtu kupangilia kazi zake na kukosa ukaribu na watoto na kwa wafanyakazi watakakosa muda wa kutimiza majukumu yao na kujikuta wakipoteza ajira zao,” amesema Janeth.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles