24 C
Dar es Salaam
Thursday, July 25, 2024

Contact us: [email protected]

Makala| Umasikini unachochea ndoa za utotoni

Na Samwel Mwanga, Simiyu

NDOA za Utotoni zimeonekana kushamiri sana katika Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu na moja ya sababu kubwa inayochochea kuwepo kwa ndoa hizo inatajwa kuwa ni umasikini.

Tafsiri mbalimbali zilizoko kweny maandiko na machapisho mbalimbali yanaeleza kuwa ndoa za utotoni ni pale msichana au mvulana wanapoingia katika ndoa wakiwa chini ya umri wa miaka 18.

Kwa kawaida, ndoa hiyo huwa kati ya msichana na mwanaume aliyemzidi umri, yawezekana pia ikawa ndoa kati ya msichana na mvulana.

Wakati mwingine wasichana huolewa kwa kuwa wamepata mimba au kwa sababu ya shinikizo kutoka kwenye familia kuwataka waolewe kabla hawajapata mimba.

Wazazi pia wanaweza kuweka shinikizo kwa vijana kuingia katika ndoa kutokana na mila au kwa vile wao ni maskini.

Mmoja ya wahanga wa ndoa za Utotoni ni ambaye tunampatia jina la Anna John(si jina lake halisi) miaka 25 mzaliwa wa kijiji cha Likungulyakoma katika Kata ya Senani wilayani Maswa anaeleza jinsi hali ya Umasikini nyumbani kwao iliyomfanya aingie kwenye mtego huo wa ndoa za utotoni.

“Sina furaha kabisa na ndoa hii natamani kutoka lakini kinachonibakisha ni watoto wangu wawili sitaki tena kuzaa mtoto mwingine nasubiri watoto wangu wakifikisha umri mkubwa wa kuanza shule ya msingi niachane kabisa na huyu mwanaume.

“Kwani nilifanya kazi kwa uadilifu nyumbani kwetu kama vile shughuli za nyumbani zikiwemo kupika nikajua baba yangu Mzazi ataniendeleza kielimu kumbe nilikuwa naenda kuangukia kwenye ndoa licha ya umri wangu kuwa mdogo,” anasema.

Hiyo ni sehemu ndogo tu ya safari aliyoipitia binti huyo ambaye kwa sasa ni mama wa watoto wawili ambao anaendelea kuwalea.

Awali ilikuwaje

Anna ambaye anaonekana kutokuwa na furaha dhidi ya maisha anayoishi na mume wake ni wa tano kuzaliwa katika familia ya watoto sita ambao kati yao wanne ni wavulana na wawili ni wasichana na wote wako hai.

Kwa mujibu wa Anna, baba yake anafahamika kwa jina la Mbusule Matulanya ambaye ni mkulima na mfugaji alianza machungu ya maisha yake yalianza wakati akiwa na umri wa miaka minne tu kwani alianza shughuli za kuchunga ng’ombe akiwa kwa shangazi yake.

“Hapo tayari na mimi nilikuwa na mdogo wangu wa miaka miwili huku mama yangu akiwa ni mkulima anakwenda shambani na kutuacha sisi wawili huku hatujui la kufanya wakati huo Kaka zetu wote ambao ni wanne walikwisha ondoka nyumbani kwenda kutafuta maisha yao ya kuchunga mifugo ya matajiri huko Sumbawanga mkoani Rukwa hivyo hawakuwa na mawasiliano tena nyumbani,” anasema Anna.

Kwa ujumla hali ya maisha yetu haikuwa ya kuridhisha sana kwani tulikuwa tunaishi na mama tu muda mwingi na baba yetu muda mrefu tulikuwa hatumuoni kutokana na kwenda sentani pale Senani na kulewa pombe na kukaa huko hadi siku tano au sita huku wakati mwingine tukilala na njaa,” anasema Anna.

Anasema ili kutoa nafasi ya matunzo kwa mdogo wake alilazimika kwenda kuishi na shangazi yake anayemtaja kwa jina la  Hollo Mitanda katika kijiji cha Ipililo.

“Nilienda kwa shangazi ambaye pia alikuwa akiishi peke yake kwani alikuwa hajawahi kubahatika  kupata mtoto kwani alikimbiwa na mme wake baada ya kukaa muda mrefu bila kuzaa  hivyo mimi nikawa ndiyo mtoto pekee katika nyumba hiyo.

“Maisha yaliendelea kwa siku za mwanzo ambapo nilikuwa nikipatiwa mahitaji muhimu kulingana kwamba nilikuwa tayari nimeshaandikishwa kuanza elimu ya msingi katika shule ya Msingi Ipililo B,” anasema Anna.

Changamoto zikaanza

Ana anasema kuwa changamoto zilianza wakati akiwa darasa la tatu
ambapo hapo alinza kwenda shamba pamoja na kushughulika na mifugo
ambayo ni ng’ombe na mbuzi na kufanya vibarua vya kusomba maji kwa
wafyatuaji wa matofali..

“Hiyo ilikuwa ni baada ya shangazi kuniambia kuwa nilitakiwa nijifunze kujitegemea kwa kufanya kazi mbalimbali kutokana kwamba kwetu tulikuwa maskini, hivyo nilivumilia changamoto hizo nikamaliza darasa la saba.

“Bahati nzuri matokeo yalipotoka nilichaguliwa kujiunga na shule ya Sekondari ya Ipililo,” anasema Anna.

Hata hivyo, safari ya masomo yake haikudumu kutokana na kushindwa kumudu ada shuleni.

“Wakati huo serikali ilikuwa bado haijaondoa ada shuleni, hivyo tulikuwa tukilipa Sh 20,000 hivyo muhula wa kwanza shangazi alinilipia Sh 10,000 lakini mhula wa pili alikataa kwa kile alichosema kwamba sikufanya kazi kwa bidii wakati wa likizo, hivyo akanitaka nitafute
fedha ili nijilipie pamoja na michango mingine.

“Nilienda shuleni bila ada lakini nikarudishwa, nilivorudi kumwambia Shangazi akaniambia natakiwa kufanya kazi kwa bidii mara mbili zaidi ili niweze kupata hiyo fedha, jambo ambalo lilinishinda,” anasema .

Afanya maamuzi magumu

Anasema kutokana na changamoto hiyo aliamua kuchukua uamuzi mgumu wa kutoroka na kurudi nyumbani kwao kwa lengo lakutaka kuwauliza wazazi wake walipo kaka zake.

“Baada ya kufika na kuwauliza walipo kaka zangu ili niweze kwenda hata kama ni mbali nilichotarajia sikukipata  kwani baba ndiye ilikuwa mwanzo wa mimi kuolewa kabla ya umri wangu.

“Kwanza baba alinikubali  kunirejesha shule iliyokuwa jirani kwa ajili ya kuendelea na masomo lakini haikuwa hivyo ni kutokana na kushindwa naye kuzimidu gharama za shule,”anasema.

Anasema kutokana na hali hiyo alifikia hatua ya kuamua kuacha shule kabisa akiwa  kidato cha kwanza.

“Nilitoroka na kwenda mjini Maswa kwani nilikuwa na kiasi cha Sh 4,000 ambazo ziliniwezesha kufika katika mji huo ambao ndio ni mara yangu ya kwanza kufika kwa kipindi hicho.

Safari ya ndoa ilianzia hapa

Anasema akiwa hapo aliingia kwenye moja ya nyumba zilizokuwa wilayani hapo akiomba kazi za ndani na kwa bahati nzuri alikubaliwa ila hakulipwa mshahara badala yake nikawa napewa chakula na zawadi ndogo ndogo kutokana kwamba nami sikuwa na sehemu ya kwenda alafu umri wangu mdogo sikujua kama nilikuwa nanyima stahiki zangu.

“Nilifanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja, baadaye yule mama ambaye ni bosi wangu akatokea kunipenda kutokana na ufanyaji kazi wangu, hivyo akanitaka niolewe na kijana wake, namimi nilikuwa sijui mambo ya ndoa nikijua nikuishi tu vizuri, nikakubali,” anasema Rehema ambaye kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 15.

Anasema baada yakukubali ombi hilo, mabosi wake hao walimwambia kuwa walihitaji kufika kwa wazazi wake ambapo aliwapeleka kwa Wazazi wake kijijini.

“Baada ya kufika waliwapatia wazazi wangu zawadi na wao wakaeleza hitaji lao na wakakubali niolewe kwa mahari ya Sh 1,000,000 fedha ambayo walilipa siku hiyohiyo na baadae tulirejea nyumbani na nikaanza kuandaliwa kama mke wakati huo nikiwa na umri  wa miaka 15.

“Kwa sasa nina watoto wawili ambao mmoja nilijifungua kawaida nikiwa na miaka 16 na mwingine kwa njia ya upasuaji, hivyo nimelazimika kukubaliana na hali halisi licha ya ukweli kwamba inaniuma sana kuona ndoto zangu hazijatumia za kuwa mwalimu,” anasema Anna ambaye kwa sasa anaishi Mjini Maswa na Mume wake huyo.

Athari za ndoa za utotoni

Ndoa za utotoni huathiri afya ya msichana, elimu, usalama na furaha. Wasichana waolewapo wakiwa chini ya umristahiki tafsiri yake ni kwamba huacha kwenda shule na kama tunavyofahamu kwamba bila elimu nzuri, wasichana hawawezi kupata kazi nzuri itakayomuwezesha kuendesha maisha na kujimudu kwa ujumla.

Aidha, wasichana hupata mimba wakiwa katika umri mdogo, kabla miili yao kuwa tayari. Hii huongeza hatari matatizo ya hatari, maradhi na hata kusababisha kifo.

Ni wajibu wa nani kukomesha hili?

Ni wazi kwamba hakuna mbinu rahisi yakuweza kutokomeza ndoa za utotoni iwapo kila mmoja atafanya kazi peke yake.

Hii ina maana kwamba lazima tufanye kazi pamoja kwani kila mmoja anayo nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko iwapo tutaungana pamoja.

Ni wajibu wetu kupaza sauti katika jamii dhidi ya ndoa za utotoni nchini na kuwasaidia wasichana kubaki shuleni na kutimiza ndoto zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles