22.8 C
Dar es Salaam
Saturday, June 3, 2023

Contact us: [email protected]

Makala: Mwanafunzi anayetumia kichwa kuchora herufi na ndoto ya kuwa rubani

Na Nora Damian, Dar es Salaam

“Ndoto yangu ni kuja kuwa rubani na naamini itatimia, nawaomba wabunge na ninyi waandishi mtusaidie kuelimisha wazazi, walezi na jamii yote juu ya watu wenye ulemavu. Watoto wasifichwe majumbani wapewe elimu kama watoto wengine,” anasema Augustino Ilomo.

Ilomo anayesoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Kimanga jijini Dar es Salaam ana ulemavu wa viungo hawezi kuandika wala kuzungumza lakini anasikia hivyo, wakati wa kusoma hulazimika kutumia kichwa kuchora herufi pindi anapotaka kuuliza au kujibu kitu.

Mwandishi wa makala haya akizungumza na Augustino Ilomo. Kulia ni mwalimu wake, Joshua Kitale.

Ni mmoja wa wanafunzi wenye uwezo wa juu darasani ambapo katika mtihani wa kidato cha pili alifaulu kwa kupata daraja la kwanza ambapo masomo yote alipata alama A.

Anaweza kuzungusha kichwa akimaanisha herufi O au kutaja namba mbalimbali kwa mfumo huo wakati akijifunza.

Alipokuwa akijibu maswali mbalimbali ya mwandishi wa makala haya alikuwa akionyesha herufi moja moja kwa kichwa kisha mwalimu wake, Joshua Kitale aliandika kwenye daftari na kuunganisha sentensi.

Baada ya kuunganisha sentensi mwalimu aliisoma na kumuuliza Ilomo kama kilichoandikwa ndicho alichomaanisha.

Kuna wakati Ilomo alikuwa anatamka herufi nne kati ya saba na kabla hajamaliza kuzitaja mwalimu wake aliweza kubaini alichomaanisha.

Mfano alipotamka neno ‘wabunge’ alianza kutaja herufi moja moja na liliposomeka ‘wabu’ mwalimu alimuuliza kama anamaamisha wabunge na Ilomo aliitikia kwa kichwa.

TAALUMA

“Kitaaluma yuko vizuri katika masomo yote, katika uelewa anatumia kichwa kuchora herufi lakini kusikia anasikia kama kawaida ila kuzungumza anatamka A na U,” anasema Mwalimu Kitale.

Mwalimu Kitale anasema kutokana na changamoto alizonazo Ilomo wakati wa mitihani amekuwa akifanya kwa mtindo huo yaani wa kutumia kichwa kwa kuchora herufi kisha mwalimu huandika.  

Anasema pia kuna haja ya kupata walimu wengi wa sayansi watakaosomea elimu maalumu ili kukidhi mahitaji ya watoto katika fani tarajiwa. 

Anawaasa wazazi na walezi kutowatenga watoto wenye ulemavu badala yake wahakikishe wanawapatia haki zao kama watoto wengine kwani wanao uwezo.

“Watoto hawa wana uwezo mkubwa wakati mwingine kuliko hata sisi, Augustino amepata A katika masomo yake yote lakini ni wanafunzi wangapi wanapata A katika masomo yao, wana changamoto lakini wana uwezo kama wengine na wanaweza kutimiza ndoto zao,” anasema Mwalimu Kitale.

MZAZI

Mzazi wa Ilomo, Faraja Kambanyuma, anasema Ilomo ambaye ni mwanawe wa kwanza tangu akiwa shule ya msingi alikuwa akifanya vizuri kitaaluma.

“Kuanzia msingi alikuwa anafanya vizuri, wakati wa mtihani alitakiwa apatikane mwanafunzi badala yake, lakini kutokana na kukua kwa teknolojia kuna kifaa (had pointer) tumemnunulia anavaa kichwani huku akitumia ‘laptop’ ambacho kinamrahishia kujifunza,” anasema Kambanyuma.

UZOEFU UHURU MCHANGANYIKO

Katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko wanafunzi sita wasioona ndio wanaoshika namba za mwanzo kwenye darasa la saba.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, Christina Wambura, anasema shule hiyo yenye wanafunzi 133 wenye mahitaji maalumu wengi wanafanya vizuri zaidi hasa wasioona.

“Kwa mfano darasa la saba wako watoto sita ambao hawaoni katika namba za mwanzo ndio wanaoshika, jamii ielewe kwamba kila mmoja anayo haki ya kupata elimu. Shule zipo, wataalamu wapo, watoto wanaweza na wanafanya vizuri,” anasema Mwalimu Wambura.

Anasema pia watoto hao wanahitaji kupendwa, kuthaminiwa na kwamba wakisimamiwa wanafanya vizuri zaidi kitaaluma.

MIKAKATI YA SERIKALI

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetengeneza mkakati wa kusaidia watoto wenye mahitaji maalumu ili waweze kupata elimu bila vikwazo. 

Kupitia mkakati huo mwaka wa fedha 2019/20 Serikali ilitenga Sh bilioni 2.3 zilizowezesha kununua vifaa saidizi ili kuboresha ujifunzaji na ufundishaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Mkurugenzi wa Elimu Maalumu, Magreth Matonya, anasema shule za msingi na sekondari zinazopokea wanafunzi wenye mahitaji maalumu zimegawiwa vifaa hivyo.

Anavitaja baadhi ya vifaa hivyo kuwa ni mashine kubwa ya kuchapia maandishi ya wasioona itakayotumika katika kiwanda cha kuchapia maandishi nukta nundu, karatasi za kuchapia maandishi ya wasioona, mashine 27 za kurudufishia maandishi ya nukta, mashine 60 za kupimia kiwango cha usikivu na vifaa 60 vya kufundishia matamshi kwa watoto wenye changamoto ya matamshi.

Vingine ni miwani 5,167 ya kuzuia mionzi ya jua, vioo 2067 vya kukuzia maandishi kwa watoto wenye ualbino na uoni hafifu, viti mwendo kwa wanafunzi wenye ulemavu wa viungo, kompyuta mpakato 20, kompyuta za mezani 65, televisheni 30 na printa 30. 

Maboresho mengine yaliyofanywa katika elimu maalumu ni kutengeneza mtaala wa walimu tarajali wa elimu maalumu pamoja na kamusi ya lugha ya alama ya kufundishia ambayo ilizinduliwa mwishoni mwa mwaka jana.

Aidha Serikali imejenga shule ya mfano ya msingi katika Chuo cha Ualimu Patandi ili wakurufunzi wawe na darasa la vitendo kwa ukaribu zaidi.

Takwimu za Elimu (BEST) za mwaka 2020 zinazotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) zinaonyesha idadi ya wanafunzi wenye ulemavu katika shule za serikali na zisizo za serikali kwenye mikoa 26 ya Tanzania Bara ni 4,178.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,270FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles