27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 4, 2023

Contact us: [email protected]

Makala| Matundu ya vyoo yatesa shule 72 Morogoro, walimu wajisaidia Loji

*Hata yale machache yaliyopo nayo yamejaa

Na Ashura Kazinja, Morogoro

SHULE za msingi 72 za Manispaa ya Morogoro zenye takribani wanafunzi 64,362 zinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa matundu ya vyoo kwa wanafunzi na walimu, ambapo yapo matundu 892 badala ya mahitaji halisi ya matundu 2,574. 

Takwimu ya idadi ya matundu ya vyoo kutoka Idara ya Elimu ya Msingi Manispaa inaonyesha ukiukwaji wa Mwongozo wa Wizara ya Elimu ambao unaelekeza tundu moja linapaswa kutumiwa na wanafunzi kati ya 20 na 25. 

Idadi ya matundu 892 kwa wanafunzi 64,362 waliopo shuleni kwa mwaka huu wa masomo unafanya uwiano wa tundu kwa wanafunzi kuwa 71, ikiwa ni wanafunzi 46 zaidi ya kiwango kinachoelekezwa na mwongozo wa elimu, jambo ambalo ni kero na hatari kwa afya ya wanafunzi na hata walimu.

Takwimu za Idara ya Elimu ya Msingi manispaa ya Morogoro zinaonesha kuwa kuna matundu ya vyoo 892 wakati mahitaji halisi ni matundu 2,574, ambayo yanafanya uwiano wa tundu kuwa ni wanafunzi 71 tofauti na Mwongozo wa wizara wa tundu moja kwa wanafunzi kati ya 20 na 25.

Kulingana na sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 na sheria ya elimu  ya mwaka 2016, pamoja na sheria ya afya ya msingi ya mwaka 2017 zinaelekeza kuwa shule zinapaswa pamoja na mambo mengine kuwa na vyoo bora na vya kutosha kwa walimu na wanafunzi. 

Aidha, kwa upande wa miundombinu ya vyoo shuleni, sera ya afya inaelekeza kuwa shule zinapaswa kuwa na vyoo salama, safi na vya kutosha, ikiwa na lengo la kulinda haki za wanafunzi na wafanyakazi wa shule ya kufanya kazi katika mazingira safi na salama.

Upungufu wa matundu ya vyoo upo karibu katika shule zote 72 za Manispaa ya Morogoro jambo linalo sababisha msongamano mkubwa wakati wa mapumziko na hivyo baadhi ya wanafunzi kulazimika kujisaidia nje ya vyoo. 

Tatizo la uhaba wa mashimo ya vyoo katika shule za msingi pia linawagusa walimu ambao katika baadhi ya shule ndani ya Manispaa wanalazimika kuchangia vyoo na wanafunzi, ambapo utaratbu huu wa kuchangia vyoo ni kinyume cha maadili

Mwalimu Mkuu shule ya msingi Mafisa A, Mdaku Rajabu akizungumzia changamoto ya matundu ya vyoo shuleni hapo anasema kuna matundu saba ambapo matatu ni ya wavulana na tundu moja kati ya hayo matatu ni kwa ajili ya walimu wa kiume na manne ya wasichana pia tundu moja kwa ajili ya walimu wa kike.

Mwalimu Mdaku anasema shule hiyo ina walimu 23 na kati yao sita ni walimu wa kike, na kwamba ili kutumia choo inabidi kusubiriana kwa zamu na kwamba kama itatokea dharula ya kutaka kutumia choo kwa pamoja huwalazimu baadhi yao kwenda kujisaidia kwenye nyumba ya wageni iliyopo karibu na shule hiyo hali inayowafanya kuwa na wasiwasi wa kuonekana eneo hilo wakati wa kazi.

“Walimu hatuna choo, inabidi kusubiriana, kuna wakati inabidi kwenye dharula tukimbilie loji ya jirani na shule inayoitwa Maraha kujisaidia, inatuathiri kisaikolojia kwani inaleta shida kuonekana loji hususani muda wa kazi,” anaeleza Mwalimu Mdaku na kuongeza:

“Hali halisi kwa sasa nina matundu yaliyoko vizuri saba ambacho ndio choo kipya,  wanafunzi tunao zaidi ya 850 ukifanya uwiano huo wa watoto 850 tulionao na vyoo saba vilivyopo unaona kuna shida kidogo,” ameeleza.

Naye Mwalimu Mkuu msaidizi shule ya Msingi Mafiga B, Semeni Kapera, anaeleza kwamba hali ya mazingira shuleni hapo ni ngumu sana, kutokana na kuwa na matundu sita tu ya vyoo, matatu kwa wavulana na mengine matatu kwa wasichana, huku shule ikiwa na jumla ya wanafunzi 1005, pamoja na matundu mawili kwa walimu 30.

Anaeleza kuwa wakati wa mapumziko wanafunzi huwalazimu kupanga foleni ili kutumia vyoo, huku wengine wakikimbilia vyoo vya nyumba jirani, na kwamba hali ni sawa na kwa walimu ambao huwalazimu kupanga foleni pia.

“Mahitaji ya matundu ya vyoo ni 45 wakati yaliyopo ni sita, matatu kwa wasichana na matatu kwa wavulana, hivyo mapungufu ni matundu 39, hali ya vyoo ni mbaya kutokana na shida ya maji, unatoka huko ukajisaidie unakuta mzigo wa mwenzio huu hapa, maji yamekata, kwakweli mazingira ni magumu mno”  anasema Mwalimu Kapera.

“Wazazi wanajua kama kuna changamoto ya vyoo, kwani nao wanakuja kwenye mikutano na wanapanga foleni pia, wazazi wanashirikishwa, walisimamisha boma la darasa halmashauri ikaja kumalizia ujenzi,  hivyo kwa sasa wanatarajia kuanza kujenga choo, sisi tunaomba sana nguvu ielekezwe kwenye vyoo, kuna watoto wanakisukari wanakwenda chooni mara kwa mara huku hali ya vyoo hairidhishi na hawawezi kupanga foleni” anaeleza Mwalimu Kapera.

“Wanafunzi wanaathiriwa na kichocho, sasa hivi hata hizo dawa zenyewe hawatuletei kwa wakati, huwa wanaleta dawa kila mwaka za kichocho na minyoo lakini sasa hivi idara ya afya inaenda inatikisika, kama mwaka jana walileta za kichocho tupu za minyoo hakuna, kwakweli hata mtoto kumbana inakuwa shida, ukimuuliza ulikuwa wapi anakwambia nilizidiwa nikakimbia jirani au nyumbani, inabidi uwe mpole umuache,” anafafanua zaidi Mwalimu Kapera.

Aidha, anasema kwa upande wa walimu ambao wana matundu mawili tu ya choo imewalazimisha kuunda urafiki na majirani ili hata dharula ikitokea ikiwemo ya kuumwa tumbo ghafla wasikose sehemu ya kwenda kujisaidia.

“Tunaiomba Serikali ituangalie sana kwa mazingira ya chooni, kwa sababu afya ni choo, kama wanavyopigania mtaani huko watujali na sisi mashuleni, na hivi tunapika chakula hapa tunaweza kumlaumu mpishi bure kumbe tatizo ni vyoo kukosa maji, hivyo mtoto akitoka chooni akaja kula bila kunawa lazima magonjwa ya mlipuko yatokee,” amesisitiza Kapera.

Kwa upande wao wanafunzi shule za msingi Manispaa ya Morogoro akiwemo, Shalom Kise darasa la nne na Magreth Kise darasa la tatu wote shule ya msingi Muungano, Baraka Anakti na Amina Selemani wa darasa la saba shule ya msingi Msamvu B wanasema changamoto ya vyoo inayowakabili katika shule zao ni pamoja na uchache wa matundu ya vyoo, vyoo kuziba, mazingira yasiyo safi pamoja na kupanga foleni ndefu wakati wa  mapumziko ili kuweza kujisaidia.

“Changamoto ya matundu ya vyoo shuleni kwetu ni kwamba yameziba, ukiingia chooni unakuwa hauna raha ya kujisaidia tunaenda hivyo hivyo tu hatuna jinsi, muda wa mapumziko foleni ni kubwa, inatuathiri kisaikolojia kutokana na mazingira sio rafiki ya choo na uchafu wa mazingira,” anasema Baraka.

Diwani kata ya Mlimani, Zinduna Selemani anasema kuwa kwa zaidi ya miaka 10 hakuna choo cha walimu katika shule ya Msingi Mbete iliyopo katika kata yake na vilivyopo havitoshi, na kwamba kuna matundu sita ya wanafunzi kwa wavulana na wasichana na kwamba kati ya matundu kumi mapya yanayojengwa wataona namna ya kufanya ili kupata matundu kwa ajili ya walimu.

Hata hivyo, anasema wananchi wanajitolea kwa kuchimba mashimo na kugonga kokoto na wengine kusomba mawe ili kujenga choo, na kwamba bajeti iliyopendekezwa ni ya madarasa mawili tu.

“Tumeshaanza ujenzi tunajenga, vyoo vilikuwepo sema havitoshi lakini tumefanya mchakato halmashauri tumepatiwa bajeti ya matundu kumi, kwa kuanzia tutatenga kwa sababu kulikuwa na choo cha zamani chenye matundu kama sita hivi, kwahiyo matundu hayo kumi yakiisha tutaona namna sasa ya kufanya tupate ya walimu,” anasema Zinduna.

Hali ilivyo matundu ya vyoo shule ya msingi Mafiga A.

Naye Mwenyekiti mtaa wa Choma, Dismas Marco, anaeleza kuwa matundu ya vyoo yaliyopo katika shule ya msingi Mbete hayatoshi, na kwamba miundombinu ya vyoo ni mibovu, anasema shule iliomba kutoka halmashauri kiasi cha Sh milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 10, na kwamba jengo limeshajengwa ingawa bado halijakamilika na fedha zimeisha mpaka ziombwe fedha nyingine.

Wakizungumzia changamoto hiyo wazazi kwa upande wao akiwemo Witness Ally mkazi wa Milima ya Uluguru kata ya Mlimani, anasema kero yao ni uchache wa vyoo vya wanafunzi na walimu ambao hawana choo kabisa na hivyo kuwalazimu kujisaidia vyoo jirani au kuchangia choo kimoja na wanafunzi.

“Kero yangu kama mzazi katika shule yetu ya Mbete ni vyoo vya wanafunzi pamoja na kutokuwepo kabisa kwa choo cha walimu, walimu  walikuwa wanatumia choo cha msikitini lakini fununu zilizopo ni kwamba watu wa msikitini  wamekataza choo chao, hivyo walimu na wanafunzi wanachangia choo kimoja,” anaeleza Witness.

Mzazi, Severin Blasio mkazi wa kata ya Tungi anasema hali isiyoridhisha ya vyoo katika shule za msingi kwenye kata hiyo inapelekea magonjwa ya mlipuko kutokana na wengine kujisaidia ovyo, huku wengine wakiogopa kula ili kuepuka kwenda chooni au kurudi nyumbani kujisaidia.

“uhaba wa matundu ya vyoo unapelekea wengine kujisaidia ovyo, watoto wetu wanaathiriwa na magonjwa ya mlipuko, baadhi ya wanafunzi wanaogopa kula ili wasiende chooni au kukimbia nyumbani na hivyo kukosa masomo,” anaeleza Blasio. 

Afisa afya  kata ya Magadu, Elda Msigara, anasema kuwa hamna taarifa yoyote ya uwepo wa ugonjwa wa kichocho kwa shule za msingi zilizopo kata ya Magadu na kwamba mwezi wa nne mwaka huu zilitolewa dawa za kichocho na minyoo kwa shule zote na hata kwa watu wa majumbani. 

Akizungumzia swala hilo Afisa elimu Takwimu Manispaa ya Morogoro, Amna Kova anasema Manispaa inashirikisha wadau mbalimbali kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya shule ikiwemo ujenzi wa vyoo ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Amewataja baadhi ya wadau hao kuwa ni Alliance One ambao wamejenga vyoo 22, Swash na Umoja wa wanawake Mainjinia, na kwamba ingawa kuna changamoto katika shule nyingi lakini ipo shule moja ya Bungo ambayo haina changamoto ya vyoo.

Hata hivyo Mkurugenzi Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Ally Machela, anasema tatizo la uhaba wa matundu ya vyoo katika shule za msingi manispaa ya Morogoro lipo kwa kiasi, na kwamba sababu msingi ya uwepo wa tatizo hilo ni ongezeko kubwa la wanafunzi kutokana na elimu bure sambamba na wazazi kuelimika juu ya umuhimu wa elimu.

Anasema serikali imeanzisha mradi wa kuboresha elimu ya awali na msingi ‘Boost’ kwa ajili ya kuboresha shule za msingi ambao mpaka sasa umeshatoa shilingi bil. 1,401,200,000 fedha za maendeleo, na kwamba kuhusiana na halmashauri kutenga kiasi gani kwa ajili ya vyoo anasema bajeti za halmashauri zina vipaumbele vyake ambapo mwaka jana ilikuwa ni ujenzi wa madarasa kutokana na ongezeko la wanafunzi, na mwaka huu 2023/2024 ni madawati, na miaka inayo fuata itaweka kipaumbele katika vyoo pia.

“Huo mradi wa Boost utatekelezwa katika shule kumi, ikiwemo kujenga shule za msingi mbili mpya, moja Mwembesongo kata ya Mafisa na nyingine katika kata ya Mindu,” amesema Machela.

“Mradi wa lipa kulingana na matokeo unao simamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi (EP4R) wameleta Sh 110, 292, 255 kwa ajili ya ujenzi wa shule na mradi wa EP4R Covid shilingi mil. 350,000,000 kwa ajili ya shule mpya na ukarabati” ameeleza.

Ameongeza kuwa serikali kuu imeshapeleka fedha kiasi cha shilingi mil.180,000,000 kwa ajili ya ukarabati wa shule mbalimbali, Sh 181,000,000 kwa ajili ya umaliziaji, na Sh 400,000,000 kwa ajili ya shule mpya moja itakayokuwa na madarasa 16, vyoo 21 na jengo la utawala, na kwamba jumla ya fedha toka serikali kuu ni Sh 661,000,000.

“Shule za msingi nyingi zina changamoto ya matundu ya vyoo lakini hii miradi ukiwemo wa boost na EP4R utalimaliza kwa kiasi kikubwa kwa kuwa ni mradi wa miaka mitano,” ameeleza Machela.

Hata hivyo, kuna msemo unasema ‘nyumba ni choo’ ili kuonyesha umuhimu na ulazima wa choo kwa binadamu, hivyo ni vyema swala la ujenzi wa vyoo vya kutosha katika shule za msingi manispaa ya Morogoro likachukuliwa kwa umuhimu mkubwa ili kuondoa adha na kero wanayokumbana nayo wanafunzi na walimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles