25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

MAJAMBAZI YAVAMIA MGODI, YAUA WAWILI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa.

Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA

WATU wawili wamefariki dunia na wengine wanne wamejeruhiwa katika Kijiji cha Nholi, Kata ya Mpalanga, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, baada ya majambazi kuvamia mgodi wa Nholi juzi na kupora madini, fedha na vitu vingine.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. James Kiologwe, aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Lukumale Membo na mwingine aliyejulika kwa jina moja la Hamisi.

Dk. Kiologwe aliwataja majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ni Sofia Sayuni (37), Sunday Undi (49), Laurence Mhagama(35) na Maila Mchele (44).

“Wagonjwa hawa waliletwa saa sita usiku, huku Maila Mchele akiwa katika hali mbaya na hadi sasa hivi hajaweza kuzungumza,” alisema.

Akizungumzia mkasa huo akiwa katika wodi namba moja hospitalini hapo, mmoja wa majeruhi, Mhagama ambaye anafanya shughuli za uchimbaji wa madini katika mgodi wa Nholi, alisema  juzi majira ya saa mbili usiku, majambazi yaliwavamia na kuwavua nguo na kuwapora fedha, simu, nguo na madini waliyokuwa nayo.

Alisema majambazi hayo yalipowavamia, alikuwa ndani na alipotoka nje kuangalia kinachoendelea, alipigwa risasi ya mguuni na kuanguka.

Majeruhi mwingine, Undi, alisema yeye ameporwa Sh milioni 2.

“Nilikuwa na marafiki zangu tunapiga ‘story’, nilishangaa tunazingirwa na kikundi cha watu kisha kutakiwa kuvua nguo na kuwapatia kila kitu tulichonacho,” alisema.

Alisema kuwa majambazi hao walipofika walipiga risasi juu na wao iliwabidi wakimbilie nyumba ya jirani na kisha kulala chini, lakini waliendelea kupiga risasi hivyo kumpata yeye ubavuni na mwenzake Mchele tumboni.

“Walipotufikia walituvua nguo na kuchukua kila kitu tulichokuwa nacho; vitambulisho, simu, nguo na madini… Walikuwa wamevaa soksi usoni,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, hakuweza kuzungumzia suala hilo akisema yuko mbali na Dodoma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,750FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles