25.5 C
Dar es Salaam
Friday, May 3, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa: Serikali inaboresha kwanza maeneo ya utawala

Na Mwandishi wetu-Dodoma


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kuboresha maeneo ya utawala lengo likiwa ni kutekeleza miradi ya maendeleo na kuongeza uwezo wa halmashauri iziweze kujiendesha.

Majaliwa alisema hayo   Dodoma jana  alipofungua Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli.

Aliwataka viongozi hao kujitathmini na kuainisha mikakati mizuri  kuhakikisha lengo la kusogeza huduma kwa wananchi linatimia.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2014/15, halmashauri 66 na mkoa mmoja wa Songwe vilianzishwa pamoja na vijiji 1,949, mitaa 1,379 na vitongoji 8,777.

Hadi sasa maeneo hayo hayajaweza kuwa na miundombinu, vifaa na watumishi wa kutosha kuwezesha wananchi kupata huduma iliyokusudiwa, alisema.

“Mathalani, mkoa wa Songwe halmashauri zake zote, hata halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ambako ndiyo makao makuu ya mkoa, bado haujafikia vigezo vya kuwa manispaa.

“Baadhi ya halmashauri zinaendelea na ujenzi wa ofisi wakati nyingine kama Mafia, Rufiji, Handeni na Ludewa zipo kwenye magofu na huwezi kuamini kama ni ofisi za halmashauri.

“Taarifa nilizonazo hadi sasa ni kwamba tayari Sh bilioni 120.7 zimepokelewa kwenye halmashauri mbalimbali kati ya Sh bilioni 238.8 zinazohitajika kukamilisha ujenzi wa majengo ya halmashauri sawa na asilimia 50.54 ya fedha zote.

Alisema kiasi kilichobaki kitaendelea kutolewa kupitia bajeti ya Serikali na mapato ya ndani ya halmashauri, na  baadhi yake zitapewa fedha za kukamilisha ujenzi baada ya uhakiki.

Majaliwa aliwaagiza viongozi wa halmashauri hizo kujenga ofisi za Serikali za vijiji, mitaa na vitongoji badala ya kuendelea kuanzisha Serikali hizo huku zikiwa hazina hata ofisi.

 

Kuhusu uhaba wa watumishi wa kada mbalimbali katika mamlaka za serikali za mitaa, Majaliwa alisema Serikali inaendelea kuajiri watumishi hususan wa kada za afya na elimu.

Alisema  kati ya mwaka 2015/2016 na 2017/2018 Serikali imeajiri watumishi wa kada ya elimu 13,472 na afya 8,238.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles