25.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Mahakama yaelezwa mshtakiwa alivyomiliki meno ya tembo

PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM

UPANDE wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Robert Mwaipyana na wenzake saba, umedai vipande 154 vya meno ya tembo kati ya 161 ni mali ya mshtakiwa huyo na alijaribu kuwarubuni polisi ili wasimkamate.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Ramadhani Mnekea, Mohamed Mboweto, Exavery Sylvester, Frank Sadick, Issah Pilla, Ramadhani Matimbwa na Cliford Maivaja.

Wakili wa Serikali, Candid Nasua aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi wakati washtakiwa hao walipokuja kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

Wakili Nasua alieleza kuwa washtakiwa wote wanakabiliwa na mashtaka ya kujihusisha na biashara haramu ya nyara za Serikali bila ya kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Alieleza kuwa Desemba 21, 2015 eneo la Temeke Sudani, mshtakiwa Mnekea alikamatwa na polisi akiwa na vipande 156 vya meno ya tembo.

Alieleza kuwa alipohojiwa na polisi alimtaja Mwaipyana kuwa ndiye mmiliki wa vipande hivyo na kwamba hakuwa na kibali cha kumliki nyara hizo za Serikali.

Wakili Candid alieleza kuwa Mwaipyana naye alikamatwa tarehe hiyohiyo baada ya jitihada zake za kurubuni polisi ili wasimkamate kushindikana.

Alieleza kuwa Desemba 23, 2015 eneo la Temeke, Miburani vilikamatwa vipande vingine vitano nyumbani kwa Mnekea baada ya kupatikana kwa taarifa kutoka kwa Mwaipyana.

Wakati wa mahojiano na polisi, washtakiwa hao walikiri kutenda makosa hayo na kuwataja wenzao ambao ni Mboweto, Sylvester, Sadick, Pilla, Matimbwa na Maivaji.

Wakili Candid alieleza kuwa washtakiwa hao walipokamatwa na kuhojiwa, kila mmoja alieleza nafasi yake katika tukio hilo  na baadaye walifikishwa mahakamani kusomewa mashtaka yanayowakabili.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, washtakiwa wote waliyakana isipokuwa majina yao.

Upande wa mashtaka umesema wataleta mashahidi 10 na vielelezo 10 wakati wa usikilizwaji kesi hiyo na kuahirishwa hadi Mei 27, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,213FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles