26.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Magufuli adai anawindwa

Waziri John Magufuli
Waziri John Magufuli

NA JOHN MADUHU, MWANZA

WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ameibuka na kusema kuwa anawindwa na mahasimu wake kwa kumbeza baada ya Mahakama Kuu kuwaachia huru watuhumiwa wa kesi ya kuvua samaki katika Ukanda wa Uchumi wa Tanzania.

Amesema watu hao wanaongozwa na ajenda za siri kisiasa na si wazalendo.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, Dk. Magufuli alisema ameshangazwa na namna suala hilo linavyofanywa kisiasa zaidi, na kudai wapo baadhi ya watu wana malengo maalumu na kesi hiyo.

Alisema operesheni iliyofanyika ya kuwasaka wavuvi haramu waliokuwa wakivua samaki katika Ukanda wa Uchumi wa Tanzania katika Bahari ya Hindi, ilikuwa chini ya ushirikiano wa nchi za kusini mwa Afrika, ikiratibiwa na SADC na kuongozwa na Afrika Kusini.

“Nilipofanikiwa kukamata meli hii na wavuvi wake nilipongezwa, lakini leo nabezwa…, wakati nakamata nilikuwa Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, nilikuwa natimiza wajibu wangu kama msimamizi wa wizara,” alisema.

Alisema baada ya Wachina hao kukamatwa, suala lao lilipelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kisha kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kama taratibu zilivyo na watuhumiwa kufikishwa mahakamani.

“Awali walipofikishwa mahakamani walihukumiwa miaka 23 na mahakama iliagiza meli yao itaifishwe. Sikuwashtaki kama Magufuli, ni Jamhuri ndiyo iliyoshtaki na kushinda.

“Baada ya Wachina hao kuhukumiwa kutokana na kazi nzuri niliyoifanya, ambayo hata ninyi waandishi wa habari hamkunipongeza, ilikuwa kimya, leo hii watu wanaibuka na kuelekeza lawama kwangu baada ya Wachina kuachiwa huru na mahakama, mara Magufuli afukuzwe mara hivi, hizo ni siasa,” alisema.

Alisema kuwa awali Mwanasheria Mkuu wa Serikali alipopeleka kesi mahakamani Wachina hao walipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka 23, lakini hakuonekana mbaya.

Akizungumzia meli ya MV Tawaliq 1, alisema ilitoka chini ya Wizara ya Uvuvi na kuwa katika uangalizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Alisema ikiwa chini ya uangalizi huo, iliibwa vifaa muhimu kabla ya kuzama, lakini hakuna ambaye amewahi kumuuliza Waziri wa Mambo ya Ndani kuhusu suala hilo.

“Mie kwa sasa si Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, nilitimiza wajibu wangu, na sasa hivi niko Wizara ya Ujenzi nikiendelea kuwatumikia Watanzania, malumbano ya kisiasa yasiyo na tija hayana nafasi kwangu, sitaki kuzungumza kwa undani hukumu ya kuachiwa hawa, watafuteni viongozi wa mahakama au ofisi ya AG na si Magufuli,” alisema.

Wiki iliyopita, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwaachia huru Wachina wa ‘samaki wa Magufuli’ na kuamuru Jamhuri iwarejeshee vitu vyao, ikiwamo meli ya Tawaliq 1.

Wachina hao waliachiwa kwa mara ya pili, kwani mara ya kwanza waliachiwa na Mahakama ya Rufaa Machi 28, mwaka huu, kabla ya kukamatwa tena na kushtakiwa upya kwa mashtaka hayo hayo yaliyofutwa.

Washtakiwa hao ni nahodha wa meli, Hsu Chin Tai na wakala wa meli hiyo ya Tawaliq 1, Zhao Hanquing, waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya uvuvi haramu katika Ukanda wa Uchumi wa Tanzania.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Prosper Mwangamila, aliwasilisha maombi ya kuifuta kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Isaya Harufani.

“Mheshimiwa hakimu, Jamhuri tunaifahamisha mahakama kwamba hatuna haja ya kuendelea na kesi dhidi ya washtakiwa, maombi yetu tunawasilisha chini ya kifungu cha sheria namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ya mwaka 2002,” alidai Mwangamila na kuwasilisha.

Wakili wa washtakiwa, Kapteni Ibrahimu Bendera, alikubaliana na maombi hayo na kuiomba mahakama iwarudishie hati zao za kusafiria, meli iliyokamatwa pamoja na samaki waliokuwamo ikiwezekana.

- Advertisement -

Related Articles

6 COMMENTS

  1. Ni jambo ambalo kwangu mimi nisiyejua sheria na vifungu vyake nashindwa kuelewa hukumu ya mwanzo waliopewa hawa Wachina ina maana kifungu cha sheria kilichowaachia sasa hivi hakikuwepo? ama hakimu aliyetoa hukumu hiyo hakusomea sheria na kulijua hilo? Ni jabo la kuhuzunisha na kumkatisha bidii ya kazi Mheshimiwa Waziri Magufuli kwani kama jitihada ya ukamataji huo kama usingefanyika hawa ndugu wa Kichina wangevuna kiasi gani cha pesa kwa samaki hao toka katika Tanzania? Ni vyema maamuzi ambayo yametolewa na mahakama yakazingatiwa vema kwani inaonyesha udhaifu fulani ambao unaweza ukajengea hoja zisizostahili katika kuamuru mambo ambayo yanaingiliana na maamuzi ya serikali. Mheshimiwa Magufuli wewe ulitenda kazi yako kama serikali ilivyokubainisha katika wajibu wako wa kazi lawama nyingine zisielekezwe kwako kwani hivyo vyombo vya sheria ndiyo vinajikanyaga vyenyewe na ndio watakaojibu kuhusu lawama za maamuzi ya awali na ya sasa yametokana na nini na hasara yake hiyo atalipa nani kama siyo hao hao mahakimu kwa kodi zao wanazolipa na kurejesha mali za hao Wachina? na kukwamisha maendeleo mengine ya taifa kwa kupoteza fedha isiyokuwa na mpangilio? Watanzania wale tunaopewa madaraka ya kazi tuangalie vema tusije tukaliingiza hasara serikali kwa jambbo linaloonekana dhahiri kama lilikuwa ni makosa kwa Wachina hawa kwa kazi waliokuwa wanaifanya tofauti na sheria za vyombo katika mwambao wa bahari yetu

  2. MH.JOHN MAGUFULI huna haja ya kukwazwa na poropoganda za wana
    siasa uchwala juuu ya hilo.ulitimiza wajiibu wako-“HONGERA KWA HILO’-wana sheria wa nchi hususan wahusika wayamalize kwa
    taratibu,zilizopo.TUJENGEE MABARABARA YETU MAKUU-USIOGOPE MUNGU YUKO NAWE.

  3. ukiona hivyo ujue kuna wanasiasa wamepanga mpango wa fedha watazolipwa wachina sehemu yake iingie mifukoni mwao,majaji hawako huru hata kidogo ndo ujue siasa ni uuwaji,kukosesha haki,kupindisha ukweli,ubakaji,na uchafu mwingine kama huo unasababishwa na siasa.EE MUNGU TUSAIDIE watu kama hawa wafe kabla ya siku zao.

  4. muheshimiwa magufuli kwa hakika huna kosa lolote kwa kukamata hio meli, ukiangalia hii kesi sababu ya kuachiwa huru hawa watu kwa mara ya kwanza sio kwamba ilithibitishwa kua hawakutenda kosa bali nimesoma kua taratibu za kisheria hazikufuatwa katika uendeshaji kesi kwasababu hio basi ndio ilipolekea kukamatwa tena kwa hawa watuhumiwa, ni jambo la kushangaza sana kuja kusikia mwanasheria wa serekali hana nia ya kuendelea na kesi hii inaonyesha dhahiri kua wameshindwa kuwa na ushahidi wa kuwatia hatiani hawa watuhumiwa kwa kufuata taratibu zilizo sahihi, kwa hio basi hapa wenye makosa ni hao watu washeriana hasa wapelelezi maana wangekua makini wangeifuta hii kesi mapema sana kabla hata samaki hawajagaiwa. hii ni uzembe wa wanasheria wetu na mpango wa kumchafua mheshimiwa Magufulu aonekane kaitia serekali na watanzania hasara. Big up muhishimiwa ila punguza kukimbilia vyombo vya habari kila tukio mengine yanaweza kua yanaandaliwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles