29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mafuriko yaathiri watu 1404 Kilosa

Na Mwandishi wetu, Morogoro

Jumla ya watu 1404 wameathirika na mafuriko ya mvua zinazoendelea kunyesha katika Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, huku nyumba 351 zikiingia maji na vyoo 368 kubomoka.

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, amesema nyumba 17 zimebomoka ambapo katika kitongoji cha Kampala jumla ya kaya 161 na watu 624 wameathirika, Kitongoji cha Madizi kaya 137 zimeathirika na watu 531, Kitongoji cha Estate kaya zilizoathirika 57 na watu 196 wameathirika.

“Kitongoji kingine ni cha Lugunga kata nane na watu 32 wameathirika, Kitongoji cha PWD kaya tano na watu 20 wameathirika,” amesema Shaka.

Amesema nyumba 17 zilizobomoko tano zinatoka kitongoji cha Kampala, nyumba nane kitongoji cha Estate na nyumba nne kitongoji cha Madizini.

Amesema jumla ya vyoo 368 vimeathirika kutokana na mafuriko, hivyo kufanya maji kuwa machafu baada ya vyoo hivyo kutapishwa na mafuriko.

Aidha, Shaka amesema jumla ya visima 30 vya maji vinavyotumika vimeathirika na mafuriko hayo kwa kuingiliwa na maji machafu.

Akizungumzia kuhusu hali ya miundombinu ya barabara, Shaka amesema zaidi kilometa 170 za barabara zimeathirika kwa maji na kusababisha kukatika kwa mawasiliano baina ya Kilosa na Mikumi, maeneo mengine ya yanayounganisha vijiji, hali iliyosababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi na shughuli za usafirishaji bidhaa.

Amesema Machi 17, 2024 maji mengi yalijaa katika mto Miyombo unaopita katika vijiji vya Ulaya, Zombo na Changarawe baada ya mvua kubwa kunyesha katika vijiji vya Kisanga, Madizini na Kitunduweta.

Amefafanua kuwa mvua hiyo ilisababisha athari katika makazi, mashamba na miundombinu ya maji na barabara katika maeneo hayo na kijiji cha Changarawe kimekuwa na matukio ya kupatwa na mafuriko mara kwa mara tangu mwaka 2016 na msimu huu wa mvua tangu Desemba mwaka jana hadi sasa ni tukio la tisa la mafuriko.

“Mafuriko haya yamesababishwa na maji kujaa katika mto Miyombo nje ya kingo za mto baada ya ongezeko la kujaa mchanga katika mabwawa ya Nara na Kipera ambayo yalichimbwa kwa ajili ya kupunguza kasi ya maji kipindi cha mvua kubwa na kuruhusu maji machache kuingia katika mto huo,”amesema.

Amebainisha kuwa uharibifu wa tuta hilo lililojengwa pia kuzuia maji yasiingie katika mashamba ya mkonge enzi hizo kwa sasa yamekuwa ni makazi ya watu.

Ameongeza kuwa shughuli za kibinadamu katika kingo za mto huo ambapo wakazi wa eneo hilo za kulima na kuchunga katika tuta hilo wameathiriwa na mvua hizo.

Katika hatua nyingine Shaka amemshukuru Dk.Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoguswa na hali ya mafuriko katika Wilaya hiyo ambapo nyakati zote amekuwa akielekeza hatua mbali mbali za haraka na dharura ili kuokoa maisha ya wananchi lakini pia kurudi huduma za kibinadamu.

“Tangu Desemba hadi leo tumekuwa na mafuriko ya mara kwa mara Rais Dk.Samia amekuwa nasi nyakati zote, tumepokea msaada wa chakula cha dharura, matibabu, magodoro lakini pia fedha za mfuko wa dharura katika kurudisha miundo mbinu ya barabara. Wananchi wanamshkuru sana vyenginevyo hali ingalikuwa mbaya sana, majanga haya yanakuja kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu hakuna anaeyatarajia ila serikali imekuwa makini mno kuhakikisha tunakabiliana nayo,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles