22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Madiwani Kinondoni wampongeza meya wao

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni limewapongeza Meya Benjamini Sitta pamoja na Mkurugenzi Aron Kagurumjuli kwa kutekeleza miradi mikubwa katika kipindi cha miaka mitano ya utendaji wao wa kazi.

Pongezi hizo zimetolewa na madiwani hao wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani robo ya tatu ya mwaka ambapo wamesema kuwa katika kipindi ambacho wamekuwa madiwani, wameshuhudia miradi mikubwa ambayo imetekelezwa, ikiwa ni  juhudi kubwa zinazofanywa na viongozi hao pamoja na watendaji.

Akizungumza katika kikao hicho, Diwani wa Kata ya Mwananyamala, Songoro Mnyonge (CCM), alisema kuwa kupitia Meya Sitta na Mkurugenzi Kagurumjuli, Kinondoni imekuwa na mafanikio makubwa kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta ya elimu, afya, miundombinu, masoko na mazingira.

Aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni stendi ya kisasa ya daladala ya Mwenge, Ofisi ya kisasa ya manispaa, uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu, soko la kisasa la Magomeni na Tandale ambayo yote inatekelezwa na mapato ya ndani.

“Miradi iliyotekelezwa ni mingi na wote humu ndani ni mashahidi, hiyo tuliyotaja ni baadhi tu, lakini ukiangalia katika sekta ya elimu na afya huko nako pia meya na mkurugenzi wamefanya kazi kubwa sana ambayo wanastahili pongezi kubwa,” alisema Mnyonge.

Aidha aliongeza kuwa kwa upande wa fedha za asilimia 10 kwa mikopo ya vijana, wazee na walemavu, kupitia uongozi huo fedha hizo zimetumika vizuri na kwamba walengwa wamefikiwa.

Diwani wa Kata ya Wazo, Joel Mwakalebela alisema kuwa kata yake pia imenufaika na fedha za  halmashauri hiyo katika sekta ya elimu na afya kwani wananchi wamepata madarasa ya kisasa pamoja na vituo vya afya kazi kubwa ambayo imefanywa na Mkurugenzi Kagurumjuli na watendaji wake.

Diwani wa Viti Maalumu, Rose Mushi alisema kuwa manispaa hiyo inaongoza kwa kuwa na barabara nzuri za lami kwa kila mtaa sambamba na mifereji ambayo imeweza kujengwa maeneo mengi yaliyokuwa na changamoto hiyo.

“Ukipita kwenye mitaa huwezi kuona barabara ambazo hazipitiki, hata mvua ikinyesha ya namna gani, kwa hili kwakweli ninampongeza sana mkurugenzi na timu yako, halmashauri hii ina viongozi wachapakazi,” alisema Rose.

Kwa upande wake Mkurugenzi Kagurumjuli, alisema kuwa mafanikio ya utekelezaji wa miradi hiyo yametokana na ushirikiano mkubwa uliopo baina ya ofisi yake na meya pamoja na watendaji kwani kila mmoja amekuwa akitimiza majukumu yake pasipokuwa na migongano.

Alisema ushirikiano huo umewezesha halmashauri hiyo kuwa na maendeleo makubwa kwenye kila nyanja kama vile elimu msingi na elimu sekondari, afya, masoko, miundombinu sambamba na mazingira.

“Tangu tumeingia kwenye utawala huu, nikiwa na Meya Sitta hatujawahi kuwa na migogoro, watendaji wamekuwa na muda mwingi wa kufikiria mambo makubwa ya maendeleo jambo ambalo limetufikisha tulipo hapa kwenye mafanikio makubwa na ndio mana leo tunapongezana hapa,” alisema Kagurumjuli.

Katika hatua nyingine, baraza hizo limepitisha taarifa za kamati mbalimbali ambazo ni Kamati ya Fedha na Uongozi, Huduma za Uchumi, Kamati ya Kudhibiti  Ukimwi, Kamati ya Maadili pamoja na Kamati ya Mipango Miji na Mazingira.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,502FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles