24.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 8, 2021

Madai tume huru ya uchaguzi yanavyopata msukumo mpya

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

KUMEKUWAPO na kilio cha muda mrefu cha vyama vya upinzani nchini juu ya tume huru ya uchaguzi huku suala kubwa linalolalamikiwa likiwa ni muundo wa tume hiyo.

Suala hilo sasa ni miongoni mwa ajenda zinazopigiwa chapuo na vyama vya upinzani wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadaye Oktoba.

Muundo wa tume hiyo kwamba wasimamizi wa uchaguzi wanakuwa wakurugenzi wa halmashauri za miji, manispaa na wilaya ndiyo unaolalamikiwa.  

Historia inaonyesha kumekuwapo na mapendekezo kwa miaka kadhaa sasa ya kuundwa tume huru ya uchaguzi kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na kutenda haki kwa kila upande. 

Mathalani Tume ya Jaji Fransic Nyalali iliyoundwa mwaka 1991 ilipendekeza mfumo wa vyama vingi na tume huru ya uchaguzi.

Aidha Tume ya Jaji Ropbert Kisanga iliyoundwa mwaka 1999 ilisema hatua ya wajumbe wa tume kuteuliwa na rais ambaye anaweza kuwa kiongozi wa chama kinachotawala katika utendaji wao ama watakuwa na upendeleo kwa chama husika ama watalipa fadhila kwa aliyewateua.

Mapendekezo mengine ni yale ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba ambayo iliona umuhimu wa kubadili muundo wa tume ya uchaguzi na kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi.

Katika kitabu chake cha My Life, My Purpose, Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, anashauri kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi ili kuimarisha demokrasia barani Afrika.

Anasema muundo wa tume umekuwa ukilalamikiwa kutokana na upatikanaji wa viongozi wake hivyo, kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi itakayokubalika na vyama vyote vya siasa ndiyo chachu ya kulea na kukuza demokrasia nchini.

Anasema mamlaka ya nchi inaweza kubaki na jukumu la kuteua mwenyekiti wa tume lakini lazima vyama vya upinzani vishirikishwe kwa uwazi katika suala zima la kuhesabu kura na kutangaza matokeo.

VYAMA VYA SIASA

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, anasema kunahitajika mabadiliko madogo ya katiba ili kutengeneza mazingira ya kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.

“Tunahitaji tume huru ambayo mwenyekiti na mkurugenzi wake hawatateuliwa na rais bila kuwa na chombo maalumu cha kuwathibitisha, watendaji wake wakuu katika ngazi za halmashauri hawatakuwa wakurugenzi, tunahitaji mchakato wa uchaguzi ambao utatoa mazingira kwa wagombea binafsi tunahitaji mazingira ya kiuchaguzi ambayo yatakuwa ‘fair’.

“Haya yanaweza kuwekwakatika katiba kwa mabadiliko madogo halafu masuala ya kupigania katiba mpya yanaweza yakafuata baada ya uchaguzi mkuu,” anasema Ado.

Anasema zipo hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa za kujenga muafaka wa kitaifa na kwamba mtu yeyote ambaye anataka kujenga maridhiano, kujenga muafaka wa kitaifa, kusababisha maelewano miongoni mwa wadau wa kisiasa na wananchi kwa ujumla, anapaswa kuungwa mkono.

“Hatua zote za kimaridhiano zinazochukuliwa sisi tunaziunga mkono, ndiyo maana baada ya Chadema kuanza jitihada za kimaridhiano kwa kumuandikia rais kumtaka akutane na vyama vya upinzani na kuchukua hatua kuleta tume huru na kadhalika, chama chetu kilitoa kauli rasmi ya kuunga hatua hizo.

“Mwenyekiti wetu mpya wa chama baada ya kuombwa na rais afanye naye mazungumzo bila kusita wakati akiwa mshauri mkuu wa chama chetu, alikwenda Ikulu na kufanya naye mazungumzo ambayo nayo unaweza kuyatia katika mkondo wa maridhiano.

“Kwa hiyo ACT Wazalendo tunakubaliana na maridhiano ili mradi yatawaliwe na nia njema, dola kwa upande wake iwe na nia njema, CCM kiwe na nia njema na sisi vyama vya upinzani daima tumekuwa na nia njema. Tukiwa katika hali kama hiyo mnufaika daima atakuwa ni Mtanzania,” anasema Ado.

Naye Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad, anamuomba Rais Magufuli kukutana na viongozi wakuu wa vyama vya upinzani ili kupata muafaka juu ya tume huru ya uchaguzi kutenda haki kwa kila upande.

“Sisi wapinzani tunalia kwamba mwenyekiti wa tume anateuliwa na rais ambaye ndiye anakuwa mgombea wa chama, wajumbe wote wanateuliwa na rais sasa kuna ile kuona hivi mimi nimuangushe huyu na kunifadhili…nitamsaidia saidia.

“Kama una tume ambayo haiko huru huwezi kusema utakuwa na uchaguzi huru na wa haki, kwa sababu huyu ‘refaree’ lazima awe afungamani na upande wowote,” anasema.

Maalim Seif anatoa mfano wa muundo wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na kudai kuwa licha ya kuwa na wajumbe wengi ambao ni wakereketwa lakini wapinzani walipewa nafasi ya kuteua wajumbe wawili.

“Tukienda kwenye mchakato wa katiba ulioongozwa na jaji warioba walitoa mapendekezo mazuri ya kupata tume huru ya uchaguzi. Wakati wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, marekebisho ya katiba hayakwua ‘perfect’ lakini upinzani walipewa nafasi ya kuteua watu wawili na rais kazi yake ni kuwatangaza tu.

“Jaji wa mahakama kuu au mahakama ya rufaa na mjumbe wengine anayeteuliwa na rais, ‘at least’ mnaona wenzenu wanawa – brief nini kinatokea huko, lakini tume iliyoteuliwa na mtu mmoja hata wakisema watakuwa free hoja ni dhaifu sana,” anasema Maalim Seif.

Nacho Chadema kupitia Mwenyekiti wake Taifa, Freeman Mbowe, kilimuandikia barua Rais Dk. John Magufuli kikimuomba afanye mabadiliko ya sheria yatakayowezesha kuundwa kwa tume huru kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu.

Mbowe anasema kuna ulazima Rais Magufuli akaunda tume ya maridhiano ili kuepusha malalamiko kutoka kwa wananchi na kuwa na taifa lenye umoja na mshikamano.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, John Shibuda, anavishauri vyama vya siasa ambavyo bado havijapata nafasi ya kukutana na Rais Magufuli kuendelea kuvuta subira.

“Tukitoa CCM kuna vyama 18 na vyote ni wadau wa tasnia ya siasa, nashauri viongozi wa vyama vya siasa wasubiri waone matokeo ya maamuzi yake kwa sababu rais ana matakwa binafsi anayoweza kuamua kuyafanya kwa hiyo tusubiri matakwa yake binafsi…ana malengo gani yatajulikana kwa vyama vya siasa vingine,” anasema Shibuda.

DHAMIRA YA JPM

Januari 21 Rais Dk. John Magufuli katika hotuba yake kwenye hafla ya kukaribisha mwaka mpya aliyoiandaa kwa ajili ya mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa Ikulu jijini Dar es Salaam, aliwaeleza viongozi hao kuwa wakati ukifika watakaribishwa kuja kushuhudia demokrasia Tanzania.

“Kama nilivyoeleza awali mwaka huu nchi yetu itafanya uhaguzi mkuu, zoezi la uchaguzi ni muhimu kwa nchi yoyote inayofuata misingi ya kidemokrasia kama yetu.

“Kwa hiyo basi Serikali imejipanga kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 utafanyika katika mazingira ya amani, uhuru na haki na kama ilivyo kawaida yetu wakati ukifika tutazikaribisha nchi na taasisi mbalimbali kuja kuangalia uchaguzi wetu ili kujionea jinsi nchi yetu inavyokomaa katika nyanja ya demokrasia,” alisema Rais Magufuli.

UBALOZI WA MAREKANI

Ubalozi wa Marekani ulimpongeza Rais Magufuli kwa ahadi yake hiyo huku ukipendekeza kuharakishwa kwa tume huru ya uchaguzi.

Ubalozi huo pia ulieleza matarajio yao ya kuwepo kwa uchaguzi wa amani ambao wagombea wote watakutana kwa amani wakieleza mawazo yao na kampeni zitakazofanyka katika misingi ya usawa.

“Tumetiwa moyo sana na hakikisho lililotolewa na Rais Magufuli la Januari mwaka huu, kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 utakuwa huru wa haki na wenye uwazi pamoja na mwaliko wake kwa waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa. 

“Tunatarajia uchaguzi ambao raia wote na wagombea wa vyama vyote wanaweza kukutana kwa amani, wakielezea mawazo yao na kampeni zitakazofanyika katika misingi ya usawa.  

“Tunatoa wito wa kuharakishwa kwa zoezi la uandikishaji wapigakura lenye uwazi, kuanzishwa kwa tume huru za uchaguzi na kuteuliwa mapema kwa waangalizi wa uchaguzi wa kitaifa na kimataifa wa kuaminika watakaofuatilia uchaguzi kwa kipindi kirefu na kipindi kifupi,”ilisema taarifa ya Ubalozi wa Marekani.

ILICHOKIFANYA NEC

Hadi sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeendesha mikutano na makundi mbalimbali ya wadau kwa lengo la kuwajengea uwezo na kupata maoni na mapendekezo yao wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.

Mikutano ya hivi karibuni ilihusisha viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, watu wenye ulemavu, asasi za kiraia, waandishi wa habari, wanawake, vijana na makundi mengine.

Baadhi ya hoja zilizotolewa na viongozi wa dini ni kuwepo kwa uwazi na uhuru bila kujali itikadi za vyama.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage, anasema manung’uniko mengi yanayojitokeza yamewekewa utaratibu kwa kufuata sheria, kanuni, katiba na maelekezo ya tume hiyo.

“Tumekuwa tukisisitiza chaguzi zitafanyika vizuri ikiwa kila mmoja atazingatia kanuni, katiba na sheria kwa sababu majibu ya manung’uniko hayo unakuta yameelekezwa vizuri kwenye sheria,” anasema Jaji Kaijage.

Anasema sheria za uchaguzi hazijaiweka tume au watendaji wake juu ya sheria au katiba ya nchi na kwamba ziko adhabu kwa yeyote atakayebainika kwenda kinyume.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, kifungu cha 89 (A) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kinaweka masharti kwamba ofisa yeyote wa uchaguzi kwa kujua na kwa makusudi akikiuka taratibu za uchaguzi na kusababisha kutenguliwa kwa matokeo ya uchaguzi, atakuwa ametenda kosa la jinai na adhabu yake ni faini kati ya Sh 500,000 hadi milioni moja au kifungo kati ya mwaka mmoja hadi miwili jela.

“Suala la siku ya kupiga kura tutaliangalia kwa macho mazuri na hatuna shaka kwamba yatatokea matokeo mazuri. Uwezekano wa kuwa na kitambulisho kimoja tumeliona hilo, lakini si katika uchaguzi huu. Tunakokwenda kuna uwezekano wa kuwa na kitambulisho kimoja,” anasema.

Kuhusu suala la maandishi ya nukta nundu, anasema wenye ulemavu wa macho wanatakiwa kuwa na watu watakaowasindikiza vituoni wakati wa zoezi la kujiandikisha na kupiga kura.

Kamishna wa tume hiyo, Jaji Mary Longway, anawaomba viongozi wa dini kuelimisha waumini wao pindi zinapotokea fikra potofu wakati wa uchaguzi.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,538FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles