25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Maandalizi sensa ya mwaka 2022 yaanza

MWANDISHI WETU-DODOMA

MTAKWIMU Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa, amesema matumizi ya teknolojia za kisasa yataleta ufanisi mkubwa katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, hivyo kuipatia nchi takwimu za uhakika zaidi na kwa wakati kuliko sensa zilizopita.

Hayo aliyasema jana alipotembelea wilayani Kondoa kukagua maendeleo na ubora wa kazi katika hatua ya awali ya utengaji wa maeneo Mtaa wa Mnarani, ikiwa ni sehemu ya matayarisho ya sensa ya mwaka 2022.

“Lengo letu ni kufanya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa ufanisi mkubwa na nimekuja hapa kukagua na kutathmini ubora wa kazi ya kutenga maeneo katika wilaya yenu,” alisema Dk. Chuwa.

Wakati wa ukaguzi huo, Dk. Chuwa alionyeshwa namna maeneo hayo yanavyopimwa na kuwekewa mipaka pamoja na namna taarifa zinavyohifadhiwa katika kishikwambi (tablet) ambazo zitatumika wakati wa kuhesabu watu tofauti na sensa zilizopita ambazo wadadisi walikuwa wakitumia ramani zilizochorwa kwenye karatasi.

Katika sensa ya mwaka 2012 kiwango cha watu waliosahaulika kuhesabiwa kilikuwa asilimia tano, ambacho hata hivyo ni cha chini ikilinganishwa na nchi nyingine barani Afrika.

“Tunataka kile kiwango cha asilimia tano cha waliosahauliwa kuhesabiwa mwaka 2012 kiondoke katika sensa ijayo ili tupate takwimu halisi na kuongeza ufanisi katika upangaji wa mipango yetu ya maendeleo,” alisema Dk. Chuwa.

Mkuu wa Kitengo cha Mifumo ya Taarifa za Kijiografia katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Benedict Mugambi, alisema kwa kutumia kishikwambi, mdadisi atafanya kazi yake ya kuhesabu watu katika eneo lake tu na hataweza kuingia eneo la mwenzake.

“Mdadisi akitoka nje ya eneo lake, kishikwambwi kitamuonyesha alama kuwa anaingia eneo silo, lakini zaidi dodoso halitaweza kufunguka, hivyo hataweza kufanya kazi,” alieleza Mugambi.

Awali, akitoa taarifa ya kazi, kiongozi wa timu hiyo, Mrasimu Ramani Jerve Gasto wa NBS, alieleza kuwa hadi sasa vijiji vyote 84 katika Halmashauri ya Kondoa Vijijini tayari vimetengewa maeneo ya kuhesabia watu na taarifa zote muhimu zimeshachukuliwa na kuweka katika ramani.

Kazi ya kutenga maeneo ya kuhesabia watu wilayani Kondoa ilianza Septemba 16, mwaka huuna kushirikisha warasimu ramani kutoka NBS, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) na wataalamu wa mipango miji kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles