26.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Maafisa elimu Kata waaswa kusimamia uboreshwaji elimu

Veronica Simba – TSC

Maafisa Elimu Kata kote nchini wametakiwa kutimiza wajibu wao wa kutoa msaada wa kitaaluma ili kuwawezesha walimu katika maeneo yao kufundisha kwa ufanisi na hivyo kuboresha kiwango cha elimu.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) David Silinde, alipokuwa akifungua Mkutano wa Viongozi wa Maafisa Elimu Kata, leo Aprili 8, 2021 jijini Dodoma.

Aidha, Naibu Waziri Silinde, amewataka Maafisa Elimu Kata kusimamia kikamilifu ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari huku akieleza kuwa imebainika baadhi ya Maafisa hao hawasimamii shule za sekondari.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Moses Chitama (kulia-mbele) na Mkurugenzi Msaidizi, Ajira na Maendeleo ya Walimu Mectildis Kapinga (wa tatu kutoka kushoto – mbele), wakiwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali katika siku ya kwanza ya Mkutano wa Viongozi wa Maafisa Elimu Kata, Aprili 8, 2021 jijini Dodoma.

“Mnajikita zaidi katika shule za msingi na kujisahau kusimamia shule za sekondari. Kote ni wajibu wenu na hakuna mtu anayepaswa kuwazuia. Akijitokeza wa kuwazuia tupeni taarifa tutamchukulia hatua,” amesisitiza.

Akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya Tume ya Utumishi wa Walimu katika Mkutano huo, Mkurugenzi Msaidizi, Maadili na Nidhamu, Mwalimu Robert Lwikolela amewataka Maafisa Elimu hao kushughulikia makosa yanayofanywa na walimu, ambayo hayapewi umuhimu kwa kudhaniwa ni madogo.

Akifafanua, Mwl. Lwikolela ametoa mfano wa kosa la utoro kwa walimu kuwa pamoja na kuathiri utoaji elimu lakini limekuwa halitiliwi maanani kwa kuchukuliwa kama halina uzito.

“Wako baadhi ya Walimu hata hawaandai Mpango wa Somo (Lesson Plan) na wanafundisha vipindi vichache tofauti na walivyopangiwa lakini wanaachwa tu. Ni wajibu wenu kuwafuatilia hao na kushirikiana na Wakuu wa Shule katika kuwarudisha kwenye mstari.”

Hata hivyo, akitoa ufafanuzi zaidi katika masuala ya nidhamu kwa walimu, Mkurugenzi Msaidizi, Ajira na Maendeleo ya Walimu, Mectildis Kapinga, amesema endapo Mwalimu atabainika kutenda kosa, anayepaswa kutoa adhabu kwake kwa mujibu wa sheria ni Mamlaka yake ya Nidhamu ambayo ni Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), na siyo vinginevyo.

Hivyo amewatahadharisha Maafisa Elimu Kata kutojichukulia sheria mkononi badala yake, ikitokea wamebaini Mwalimu anakiuka maadili ya kazi yake, washirikiane na Mkuu wa Shule kumkanya ili abadili mwenendo wake na asipojirekebisha wamripoti kwa Mamlaka yake ya Nidhamu ili imchukulie hatua.

Kwa upande wake, akitilia mkazo suala la uwajibishaji walimu wanaokiuka maadili ya kazi, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu kutoka TSC, Moses Chitama, ameshauri kabla ya muhusika kuripotiwa kwa Tume, zifanyike jitihada katika ngazi ya shule na kata, kukaa na kuzungumza naye ili kumkanya, hususan kwa makosa madogomadogo ambayo yanarekebishika.

Mkutano huo wa Maafisa Elimu Kata unatarajiwa kuhitimishwa rasmi kesho Aprili 9, 2021 ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles