25.1 C
Dar es Salaam
Saturday, December 9, 2023

Contact us: [email protected]

LWANDAMINA: SIENDESHWI NA PRESHA ZA MASHABIKI

IMG_7704

ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM NA SAADA AKIDA, ZANZIBAR

KOCHA mkuu wa timu ya Yanga, Mzambia George Lwandamina, amesema hawezi kuwa mtumwa wa kuendeshwa na presha za mashabiki wa timu hiyo, ambao wanataka ushindi katika kila mchezo bila kujali changamoto za mchezo wa soka.

Timu ya Yanga ambayo ilianza vema michuano ya Kombe la Mapinduzi, juzi ilitupwa nje ya michuano hiyo baada ya kuchapwa mikwaju ya penalti 4-2 katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa Uwanja wa Amaan.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Lwandamina alisema ni vugumu kuwaelewesha mashabiki maana halisi ya soka kutokana na kuegemea eneo moja ambalo ni ushindi pamoja na kulipa kisasi bila kujali kuna kufungwa au kutoa sare.

“Wachezaji wanatakiwa kufanya juhudi ili kufika katika mafanikio wanayoyataka wakiwa na mawazo chanya, hakuna anayejua nini kitatokea ndani ya dakika 90 za mchezo, kitu cha muhimu tunatakiwa kuwa na umoja na hamasa ya kutosha,” alisema Lwandamina.

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya nchi, Mzambia huyo alisema soka halitaendelea kutokana na  mawazo ya walio wengi kuyaelekeza katika kulipiza kisasi badala ya kutazama vitu vya msingi.

“Tutaendelea kupambana ili kutunza hadhi yetu kama Yanga, lakini tunashindwa kuelewa kuwa soka ni mchezo wa kisayansi, hivyo ni vigumu kuendelea kutokana na kutokuwa na mawazo mapana katika mchezo huo,” alisema Lwandamina.

Kauli ya kocha huyo ni kama kuwajibu mashabiki wa timu hiyo ambao wanaonekana kukerwa na timu hiyo kufungwa na timu za Azam na Simba, hali iliyoitupa nje ya mashindano.

Lwandamina alionyesha kukerwa na mashabiki hao zaidi pale alipoamua kuandika katika ukurasa wake wa facebook kuwa ili kupata ushindi kunahitajika uwekezaji wa kutosha na kujiandaa.

Katika hatua nyingine, kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, alisema kujiamini  kupita kiasi kwa wachezaji wao ndio sababu kubwa ya kupoteza michezo miwili mfululizo katika michuano hiyo.

Kabla ya kupokea kichapo kutoka Simba, Yanga ilikutana na Azam FC katika hatua ya makundi ambapo ilikubali kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa wanalambalamba hao.

“Simba na Azam tunazijua, hivyo wachezaji wetu wameingia kucheza nazo kwa kujiamini sana wakijua watashinda, tofauti na walivyocheza na timu nyingine ambazo hawazijui, tumeligundua hilo na tutalifanyia kazi,” alisema.

Mwambusi alisema baada ya kurejea jijini Dar es Salaam, wanayafanyia kazi mapungufu  yaliyojitokeza ili kujiandaa vyema na mechi yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Sasa tunarejea nyumbani kwa ajili ya kuendelea na michezo yetu ya ligi pamoja na maandalizi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa, ambayo inaanza mapema mwaka huu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles