27.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Lissu azua kizaazaa mahakamani

Kulwa Mzee, Dar es Salaam

Mdhamini wa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Robert Katula ameiambia mahakama kuwa wakati anamdhamini mshtakiwa huyo hakujua kama atapigwa risasi.

Katula ametoa madai hayo leo Jumatatu Januari 20, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipokuwa ikitajwa.

Amesema Desemba 19 mwaka jana, mahakama iliamuru Lissu afike leo mahakamani lakini amefanya juhudi za kuwasiliana naye akawafahamisha kwamba atawasiliana na wakili wa chama lakini hadi leo kimya.

Mdhamini huyo ameomba apewe muda zaidi wa kuhakikisha anamfikisha mshtakiwa huyo mahakamani.

“Mheshimiwa wakati natoa ahadi kwamba nitahakikisha anafika mahakamani sikujua kama atapigwa risasi, tumemuandikia Mwenyekiti Freeman Mbowe barua atusaidie kumfikisha mshtakiwa nchini,” amedai Katula.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hadi Februari 20 mwaka huu na kuamuru kwamba mshtakiwa ni lazima afike mahakamani tarehe hiyo kabla mahakama haijatoa amri nyingine zenye nguvu zaidi dhidi ya wadhamini.

Mdhamini wa mwingine wa Lissu ni Ibrahim Ahmed.
Kesi hiyo ilifunguliwa Juni 14 mwaka 2016 baada ya muda mshtakiwa wa nne, Lissu akapata matatizo yaliyomfanya ashindwe kufika mahakamani.

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Lissu na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Inadaiwa kuwa Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa watatu, Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 jijini Dar es Salaam, walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13, 2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokua na taarifa za uchochezi.

Alidai mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Mbali na mashtaka hayo washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016, Dar es Salaam, bila ya kuwa na mamlaka yoyote, waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar wasiweze kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,903FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles