32.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 5, 2024

Contact us: [email protected]

Kutumbuliwa Balozi Kidata pasua kichwa

Na Mwandishi Wetu-Dar es salaam

Kitendo cha Rais Dk. John Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada, Alphayo Kidata pamoja na kumwondolea hadhi ya ubalozi kimezua maswali na kuacha hisia tofauti.

Hisia hizo na maswali zimetokana na taarifa iliyotolewa juzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Faraji Mnyepe, kwa kuwa haikuweka wazi sababu za Rais Magufuli kufikia uamuzi huo.

Katika mtiririko wa maswali hayo, kuu ambalo wengi wanajiuliza, ni nini kikubwa alichokifanya Kidata hadi Rais Magufuli kufikia hatua ya kumwondolea hadhi ya ubalozi?

Baadhi ya wadadisi wa mambo wanadai kuwa, bila shaka Rais Magufuli atakuwa na sababu nzito ya kufanya hivyo, ambayo kwa sasa imebaki kuwa siri.

Wapo pia waliokwenda mbali zaidi na hata kujenga hisia kwamba huenda kuna jambo pengine la kimaamuzi alilofanya Kidata ambalo limeigharimu nchi.

Kutokana na uamuzi huo, Kidata anaandika rekodi ya kuwa mtu wa kwanza katika Serikali ya Rais Magufuli na wa pili kuanzia serikali iliyokuwa ikiongozwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuondolewa hadhi ya ubalozi.

Wakati wa utawala wa Kikwete mwaka 2007, Profesa Costa Mahalu, aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Italia, alisimamishwa kazi na kuvuliwa hadhi ya ubalozi, kisha alifunguliwa mashtaka ya jinai na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, mwaka 2012 mahakama ilitoa hukumu kwamba Profesa Mahalu hakuwa na hatia, hivyo Machi mwaka huu, Rais Dk. Magufuli alimrudishia hadhi ya ubalozi Profesa Mahalu.

Tayari baadhi ya wadadisi wamekwisha jenga hisia kwamba iwapo Kidata ametenda kosa la jinai ambalo limesababisha kuvuliwa hadhi ya ubalozi, huenda naye akakabiliana na mkono wa sheria katika vyumba vya mahakama ndani ya siku chache zijazo.

Ili kufahamu kilichomsibu Kidata, ambaye aliteuliwa kuwa balozi wa Tanzania nchini Canada Januari 10, mwaka huu, MTANZANIA Jumamosi liliwasiliana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, ambaye alilitaka gazeti hili kuwatafuta Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa kuwa ndio waliotoa taarifa hiyo.

Gazeti hili lilimtafuta Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga, ambaye alisema kuwa yuko likizo.

“Kama ni masuala ya kiofisi, siko ofisini, watafute watu wizarani, mimi niko likizo,” alisema Mindi.

Jitihada za MTANZANIA Jumamosi kuwapata wahusika hazikuzaa matunda, kwani namba ya simu ya Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Augustine Mahiga, haikupatikana.

Alipotafutwa Naibu wake, Damas Ndumbaro kupitia simu yake ya kiganjani, alijibu kwa ujumbe mfupi kuwa kwa mujibu wa Katiba na Mkataba wa Vienna, mamlaka ya uteuzi na utenguzi yako kwa Rais.

“Kwa mujibu wa Katiba na Mkataba wa Vienna, mamlaka ya uteuzi na utenguzi ni Rais,” alisema Dk. Ndumbaro.

Kabla ya kuteuliwa kuwa balozi, Kidata aliwahi kushika nafasi tofauti. Machi 2016, Rais Magufuli alimteua kuwa Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) na baadaye kumthibitisha kuwa Kamishna Mkuu.

Kabla ya uteuzi huo, Kidata alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, nafasi aliyoishika tangu Agosti, 2013, alipoteuliwa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, akitokea Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), alikokuwa Naibu Katibu Mkuu.

Machi 23, 2017, kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi nchini Canada, alikuwa Katibu Mkuu (Ikulu), akichukua nafasi ya Peter Ilomo ambaye alistaafu.

 

Mchambuzi wa masuala ya kidiplomasia achambua

 

Mchambuzi wa Masuala ya Kimataifa ya Diplomasia, Abbas Mwalimu, amechambua sababu mbalimbali ambazo husababisha balozi kurejeshwa nyumbani, kutenguliwa na hata kuvuliwa hadhi ya ubalozi.

 

Sababu, mazingira ya balozi kuweza kuitwa nchini mwake

Kwa mujibu wa Mwalimu, sababu ya kwanza ni kuharibika kwa hali ya usalama wa nchi husika, Balozi kumaliza muda wake au kupangiwa majukumu mengine na nchi yake.

Kuzorota/kuharibika kwa uhusiano baina ya nchi na nchi, lakini pia balozi kushindwa kufikia matarajio ya nchi au taasisi.

Kuhusu sababu zinazoweza kutumika kumvua balozi hadhi hiyo, Mwalimu anaeleza mojawapo ni mashtaka.

Huku akitumia mfano wa kile kilichowahi kumkabili Balozi Mahalu, Mwalimu alieleza katika andiko hilo kuwa, kilichosababisha Profesa Mahalu kuvuliwa hadhi yake ya ubalozi mwaka 2007 ni kuruhusu taratibu za kimahakama kufuata mkondo wake.

Anasema mabalozi huwa na kinga dhidi ya mashitaka katika zile nchi zilizowapokea na ambazo wanazofanyia majukumu yao.

Anasema hiyo ni kwa mujibu wa Ibara ya 31 ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961.

Watu wanaofuatilia mwenendo wa mambo mbalimbali watakuwa wanakumbuka jinsi Profesa Mahalu, ambaye  aliteuliwa kuwa balozi na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kati ya mwaka 1999 na 2000 na baadaye Kikwete kati ya mwaka 2000 hadi 2006, alivyorudishwa nchini na kufunguliwa mashitaka ya jinai na uhujumu uchumi, sambamba na mfanyakazi mwingine wa ubalozi, Grace Martin.

Kesi hiyo ilikuwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, mwaka 2007, ikitokana na manunuzi ya Ofisi ya Balozi ya Oktoba 1, 2002.

Ilidaiwa Balozi Mahalu na Grace walituhumiwa kula njama na hatimaye kutumia nyaraka feki ili kuidanganya mamlaka na kuiingizia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60, sawa na zaidi ya Sh bilioni 2.5 za Tanzania.

Balozi Mahalu na Grace walifunguliwa mashitaka sita tofauti kwa kile kilichoelezwa kuwa walikiuka Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2002 [Cap.329. R.E.2002], Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 [Cap. 16.R.E.2002] na Sheria ya Kupambana na Uhujumu Uchumi ya mwaka 2002 [Cap. 200.R.E.2002].

Hata hivyo, mahakama iliwaachia huru baada ya kubainika kuwa hawakuwa na hatia.

Je, kinga za mabalozi zina mipaka?

Mwalimu anasema, kwa mujibu wa Ibara ya 37, ibara ndogo ya 4 ya Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, inaeleza kuwa kinga ya mashitaka ndani ya mamlaka iliyompokea hazimfanyi balozi kutoshitakiwa na mamlaka iliyomtuma.

Nani mwenye mamlaka ya kumvua balozi hadhi yake?

Mwalimu anachambua kuwa mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 umetoa mwongozo wa nani mwenye mamlaka ya kumvua balozi hadhi yake.

Ibara ya 32, ibara ndogo ya kwanza ya mkataba huu inaeleza kuwa kinga ya mashitaka ambayo balozi hupewa huweza kuondolewa na nchi iliyomtuma tu.

Sasa swali hapa linakuja kuwa ni nani katika nchi iliyomtuma balozi ana mamlaka ya kumvua hadhi?

Kwa mujibu wa Ibara ya 36 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inaeleza ifuatavyo…

 

36 (2) Rais atakuwa na madaraka ya kuteua watu kushika nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za idara na taasisi za Serikali, na watendaji wakuu wanaowajibika kusimamia utekelezaji wa sera za idara na taasisi hizo katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, nafasi ambazo zimetajwa katika sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge kwamba zitajazwa na uteuzi unaofanywa na Rais.

 

Kutokana na ibara hii ya 36 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunaona kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye mwenye Mamlaka ya kumteua mtu yeyote kuwa Balozi kuiwakilisha nchi na pia kama mwakilishi wa Rais katika nchi na vivyo hivyo ana haki ya kumvua hadhi ya ubalozi na hata kutengua uteuzi wa mtu yeyote endapo kutakuwa na hitaji la kufanya hivyo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles