28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

Kuogelea waahidi kutetea ubingwa Rwanda, Serikali yawapongeza

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

Timu ya Tanzania ya mchezo wa kuogelea, imeahidi kutetea ubingwa wao katika mashindano ya nane ya ‘Africa Aquatics’ kanda ya tatu yatakayofanyika Novemba 23-25, 2023, Kigali, Rwanda.

Jumla ya waogeleaji 30, wanaume 16, wanawake 14 wanaounda timu hiyo, wameagwa jana Novemba 20, 2023 kwa kukabidhiwa bendera ya Tanzania katika hafla iliyofanyika kwenye Shule ya Kimataifa ya Tanganyika(IST), Masaki, Dar es Salaam.

Tanzania inashiriki michuano hiyo inayoshirikisha timu 11 ikiwa bingwa mtetezi baada ya kutwaa ubingwa huo Novemba, 2022 katika mashindano yaliyofanyika hapa nchini ambapo jumla ya Mataifa 10 yalishiriki.

Akizungumza na waandishi wakati wa hafla hiyo ya kuagwa, Mwenyekiti wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Mhandisi David Mwasyoge, amesema ahadi yao kwa Serikali ni kwenda kutetea bendera ya nchi na kurejea na ubingwa.

“Tunachoahidi Serikali sisi tunakwenda kutetea bendera ya nchi, hatuwezi kumuangusha mama tunaahidi tunarudi na ubingwa.

“Kikubwa pia kuwashukuru wazazi ambao kwa asilimia 85 wamefanikisha hii safari na wadau wote ambao wamehakikisha hii timu Taifa inafanya mazoezi na inakwenda kushindana,” amesema Mhandishi Mwasyoge.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa(BMT), Neema Msitha ambaye ndiye aliyekabidhi bendera kwa timu hiyo, amesema Serikali ina imani na wachezaji hao kuwa watakwenda kufanya vizuri.

“Serikali imefurahishwa na kile mnachokifanya, mwaka jana mlifanya vizuri pale Gymkhana nyie ni mabingwa na hata sasa matarajio ya serikali ni kuona mnafanya vizuri na kutetea ubingwa wenu.

“Nina imani kubwa na nyie, mna kocha mzuri, kocha Alex anafanya kazi kubwa, alafu najua mnapata sapoti kubwa kutoka kwa wazazi na viongozi wa chama,” amesema Neema.

Aidha Neema amepongeza jitihada zinazofanywa na TSA ikiwemo ikifanya mashindano mengi na kuifanya timu ya Taifa kuwa imara, huku wakishirikisha wadau wanaochangia baadhi ya gharama.

Kocha wa timu hiyo Alex Mwaipasi, ameweka bayana kuwa kwa kushirikiana na wakufunzi wenzake, wamewaandaa wachezaji vizuri, bila shaka wataendeleza ushindi.

Naye nahodha wa timu hiyo, Collins Saliboko, amesema kila mtu yupo tayari na wamejiandaa kushinda na uwepo wa wachezaji wengi utasaidia kufanya vizuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles