27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

KTO yawawezesha wasimamizi wa vituo vya kulelea watoto chini ya miaka mitano

Na Clara Matimo, Mwanza

Ili kuhakikisha  kwamba watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanajengewa  mazingira ya kuweza kuchangamsha akili, kuwa wadadisi, kukua kisaikolojia  na kufurahia masomo  walimu wa watoto hao wamewezeshwa  mbinu mbalimbali za ufundishaji zitakazowafanya watoto kukuwa wakiwa na maadili mazuri.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya malezi, makuzi na maendeleoa ya awali ya mtoto chini ya miaka mitano wakisilikiza maelezo yanayotolewa na mwezeshaji Laurent Manyono(hayupo pichani).

Uwezeshaji huo umefanywa na Shirika lisilo la serikali la Karibu Tanzania Organization(KTO) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo jumla ya wasimamizi wa vituo vya kulelea watoto kutoka vyuo 14 vya maendeleo ya wananchi nchini wamepewa elimu ya  malezi, makuzi na maendeleoa ya awali ya mtoto chini ya miaka mitano.

Mafunzo hayo ya siku 10 yalifanyika katika  Chuo cha Maendeleo ya Wananchi(FDC) Sengerema kilichopo Mkoani Mwanza kuanzia Januari 25 hadi Februari 3, 2023.  

Akizungumza  Februari 3, 2023 wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mkurugenzi wa KTO, Maggid Mjengwa, alisema wameamua kutoa mafunzo hayo baada ya kubaini watoto wengi wanaosoma chekechea wanajifunza kusoma na kuhesabu jambo ambalo wanadhani si sahihi kwani  watoto chini ya miaka mitano wanahitaji kucheza na  kujengewa mazingira ya kuweza  kuchangamsha akili zao ili waweze kuwa wadadisi.

“Ukitaka kujua ustawi wa kesho wa nchi  angalia watoto  na vijana wake leo wako katika hali gani pia wazazi na walezi wa leo tunapoangalia wazazi na walezi  wa leo hawana maarifa mengi juu ya malezi na makuzi ya watoto wanahitaji kuwezeshwa kupata  maarifa hayo ikiwemo mbinu na nyenzo zitakazowasaidia kuwalea watoto wetu vizuri.

Watoto wengi leo wanajilea wenyewe wakati mwingine au wanalelewa na simu na televisheni sasa tukiacha jukumu la malezi kwa televisheni na simu tunakuwa tunaandaa mazingira ya watoto kukosa uadilifu maana wanachokiangalia mzazi au mlezi hukifahamu vitu vingi wanavyoangalia vinaweza vikawa havina tij,” alisema Mjengwa na kuongeza.

Katika kutatua changamoto hiyo tunadhani watoto kucheza kwenye vituo vya kulelea watoto ni mahali salama zaidi maana vinahusika pia na ulinzi wa mtoto ndiyo maana tumeona kuna umuhimu wa kutoa mafunzo haya kwa wasimamizi wa watoto hao ili kujua saikolojia ya mtoto na hata kwenye vituo vya kulelea watoto mara nyingi tunakosa watu wenye utaalamu huo,” alisema Mkurugenzi wa Shirika la KTO ambalo linajishughulisha na masuala ya elimu.

Afisa kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Idara ya Ufundi, Henry Adriano, alisema mafunzo hayo yataleta chachu katika jamii kuhusu malezi ya watoto kwani ingawa washiriki waliishasoma vyuoni lakini dunia inabadilika kila siku hasa kwenye makuzi ya watoto.

“Kuwapa washiriki mafunzo haya ni kuwa update ili waweze kwenda na wakati tunaamini yatawasaidia kukabiliana na mazingira yaliyopo sasa hivi ya utandawazi, hivyo nawasihi sana washiriki wote waende kuitumia elimu waliyoipata hapa kwa siku 10 kuwalea vizuri watoto naamini wakifanya hivyo tutapunguza vibaka mitaani.

“Ndiyo maana wizara ya elimu tunapambana kuwapa walimu wetu mbinu mbalimbali za kukabiliana na utandawazi ambao unaathiri malezi ya watoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu likiwemo shirika hili la KTO,” alisema Adriano.

Akizungumza wakati akifunga mafunzo hayo mgeni rasmi ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Sengerema, Consolata Magaka, alisema matukio ya kupigwa, kubakwa na unyanyasaji wa kisaikolojia ndiyo yanayoripotiwa kuwakumba watoto ambapo aliwashauri wazazi na walezi kutumia vyuo vya maendeleo ya wananchi vyenye vituo vya kulelea watoto mchana (day care centre) ili wapate malezi bora yatakayowajenga kisaikolojia badala ya kuwaacha na wasaidizi wa kazi nyumbani ambao hawana utaalamu wa kulea watoto.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Beatrice Chaula ambaye ni Mkufunzi kutoka chuo cha Maendeleo ya Wananchi Bariadi Mkoani Simiyu  alisema” Tunamshukuru sana mzazi wetu Wizara ya elimu ambaye  ametambua kwamba akituunganisha na KTO ufanisi wetu katika kutekeleza majukumu yetu utaongezeka.

“Tutafanya kazi kwa kujiamini zaidi, elimu  mliyotupatia haitaishia kwenye maeneo yetu ya kazi tu bali pia tutaitumia majumbani kwetu hivyo tutazidi kuwa mama bora kuanzia ngazi ya familia hadi kwenye jamii hasa mkizingatia kwamba mmetupatia vifaa vya kutoa mafunzo kwa watoto wanaopata elimu ya awali pamoja na kutujengea uwezo jinsi ya kutengeneza zana za kufundishia  zinazotumia gharama nafuu kwa kutumia vifaa vinavyopatikana kwenye mazingira yetu tunashukuru sana,” alisema Beatrice.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa KTO, Mjengwa, Kati ya vyuo 54 vya FDC vilivyopo nchini 10 vinaendesha moja ya programu ambazo zinaratibiwa na Shirika lake ikiwemo elimu haina mwisho  inayotoa fursa kwa watoto wa kike waliokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali kujiendeleza katika fani mbalimbali, mpira fursa inayolenga kukuza vipaji kwa watoto wa kike mashuleni pamoja na elimu ya malezi, makuzi na maendeleoa ya awali ya mtoto chini ya miaka mitano.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi(FDC)  Sengerema, Ramadhani Yakubu, aliwaasa washiriki wa mafunzo hayo kwenda kuitumia elimu waliyoipata kwa manufaa ya kuboresha vituo vya watoto ili lengo lililokusudiwa na serikali pamoja na KTO liweze kufikiwa.

Washiriki wa mafunzo hayo wametoka mikoa mnalimbali ikiwemo Mara, Iringa, Morogoro, Dodoma Singida na Mwanza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles