24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kortini kwa kumuita Magufuli bwege

Tanzania's President elect Magufuli addresses members of the ruling CCM at the party's sub-head office on Lumumba road in Dar es Salaam ELIYA MBONEA NA JANETH MUSHI, ARUSHA

MKAZI wa Arusha, Isack Emiliy (40), amepandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka ya kusambaza lugha ya matusi na dhihaka kwa Rais John Magufuli.

Isack anakuwa mtu wa pili kushtakiwa katika kesi inayomhusu Magufuli baada ya hivi karibuni kondakta wa daladala, Hamimu Seif (42), kupandishwa kizimbani kwa kosa analodaiwa kulifanya Machi 10, mwaka huu alipotishia kumuua Rais Magufuli kwa maneno akiwa katika Baa ya Soweto iliyopo Makumbusho, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Kondakta huyo ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Ujiji, Mwananyamala jijini Dar es Salaam, alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Riwa na kusomewa shtaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kenneth Sekwao.

Wakili Sekwao alidai mahakamani hapo   kwamba kondakta huyo alitishia kumuua Magufuli kwa kutamka maneno kuwa: “Kwa mambo anayoyafanya Magufuli, nipo tayari kujilipua kwa kujitoa mhanga ili kumwangamiza.”

Kesi ya kondakta huyo iliahirishwa hadi Aprili 21, mwaka huu baada ya kukana kutenda kosa hilo alilosomewa mahakamani hapo na alikosa dhamana kutokana na kushindwa kutimiza masharti huku upande wa mashtaka ukiwa haujakamilisha upelelezi.

Kwa upande wa kesi ya Isack anayeishi Kata ya Olasite, anadaiwa kutoa lugha ya matusi na dhihaka kwa Magufuli kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook na alikamatwa Machi 23, mwaka huu mjini Arusha na kupelekwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam kisha alirejeshwa tena Arusha Aprili 14, mwaka huu kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka.

Akisoma mashtaka hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Augustine Rwizile wa Mahakama ya Hakimu Arusha, Wakili wa Serikali, Gaudensia Massanja, alidai kuwa Isack anakabiliwa na kosa moja.

Wakili Massanja alidai kuwa kwa kufahamu na kwa makusudi mtuhumiwa huyo alitumia mtandao wa Facebook kwa nia ya kumtukana Magufuli.

Alidai kwamba mtuhumiwa katika ukurasa wake wa Facebook alichangia maneno yanayosema: “Hizi ni siasa za maigizo halafu mnamfananisha huyu bwege na Nyerere wapi buana.”

Kwa upande wake, Isack, aliiomba mahakama hiyo kumpatia dhamana kwa kuwa ni haki yake.

Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa na Wakili Massanja aliyedai upepelezi wa shauri hilo haujakamilika hivyo kumpatia dhamana mtuhumiwa kunaweza kuharibu upelelezi.

“Hakimu tunaomba kuzuia kwa muda dhamana hii kwa sababu bado hatujakamilisha upelelezi. Lakini pia kwa ajili ya usalama wake mitaani anakoweza kudhurika kutokana na aina ya mashtaka yanayomkabili,” alidai Wakili Massanja.

Akitoa uamuzi mdogo wa hoja za pande mbili mahakamani hapo, Hakimu Rwizile, alisema kwamba uamuzi kamili wa dhamana ya mtuhumiwa huyo utatolewa Aprili 18, mwaka huu.

“Mtuhumiwa utaendelea kukaa ndani hadi Jumatatu nitakapotoa uamuzi wa dhamana yako,” alisema Hakimu Rwizile.

Awali, akizungumza ofisini kwake mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo katika Hoteli ya Annex iliyopo mjini hapa.

Mkumbo alisema kuwa Machi 17, mwaka huu, mtuhumiwa akiwa nyumbani kwake alipokea ujumbe katika akaunti yake ya Facebook uliosema: “Mnamlinganishaje Magufuli na Nyerere.”

Alisema ujumbe huo ulikuwa ni mjadala ulioanzishwa katika mitandao ya kijamii baada ya hatua ya Magufuli kupiga simu katika Kituo cha Clouds Tv kwenye kipindi cha Clouds 360.

Mkumbo alisema kupitia mjadala huo uliochangiwa na watu wengine, Isack kwa upande wake aliandika ujumbe uliojibu mada iliyoanzishwa akisema: “Hizi ni siasa za maigizo halafu mnamfananisha huyu bwege na Nyerere wapi buana.”

Alisema maneno hayo kutoka kwa Isack yaliwaudhi na kuwakwaza wachangiaji wengi waliousoma ujumbe huo na kusababisha malalamiko kufika ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo ilitoa taarifa kituo cha polisi na hatua kuchukuliwa.

“Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na TCRA tulifanikiwa kufanya uchunguzi wa kina na kumkamata mtuhumiwa akiwa na simu ya mkononi aina ya Tecno iliyotumika kutenda kosa hilo,” alisema Mkumbo na kuongeza:

“Polisi inatoa rai kwa wananchi watumie vizuri mitandao ya kijamii kujiletea maendeleo kubadilishana taarifa zenye tija na ufanisi na sio kuvunja sheria za nchi,” alisema Mkumbo.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles