Erick Mugisha Na Saidi Ibada (TUDACO) -Dar es salaam
MKAZI wa Manzese, Dar es Salaam, Amiri Shekhe (25), amepandishwa kizimbani Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kwa tuhuma za kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha tatu.
Akimsomea mashtaka jana mbele ya Hakimu Anifa Mwingira, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Hilda Kato alidai kuwa Novemba 10, mwaka huu eneo la Mvuleni Manzese wilayani Ubungo, mshatakiwa alimpa mimba mwanafunzi wa kidato cha tatu mwenye umri wa miaka wa 17.
Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na Kato alisema upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba mahakama ipange tarehe nyingine.
Hakimu Mwingira alisema dhamana ipo wazi kwa mshtakiwa kwa kutakiwa kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh 500,000.
Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurudishwa rumande hadi Agosti 19, mwaka huu kesi hiyo itakapokuja kutajwa tena.