23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

KISA CHA MTOTO MNYWA MAFUTA NA MGANGA WA KIENYEJI

Dk. Rwezaula akimsaidia Shukuru kukaa vema kwenye kiti anachotumia kutembelea, kulia ni mama wa mtoto huyo

 

Na Veronica Romwald – Dar es Salaam

SI jambo la kawaida hata kidogo, mtu kuishi akila mafuta lita moja, maziwa lita tatu na sukari robo tatu tena kila siku. Lakini hayo ndiyo yalikuwa maisha yake Shukuru Kisonga kwa miaka 16.

Shukuru alizaliwa Aprili 2, 2001 ni mtoto wa mwisho katika familia yenye watoto watano ya Mzee Kisonga na Mwanabibi Mtenje, makazi yao yakiwa wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.

Amekuwa akilazimika kula vitu hivyo ili kuondokana na maumivu makali aliyokuwa akiyapata kutokana na ugonjwa ambao awali haukugundulika.

Mwanabibi ambaye ni mama mzazi wa mtoto huyo anasema alishauriwa kumpatia mtoto wake vitu hivyo na mganga wa kienyeji.

“Ilipofika Novemba, 2001 mwanangu akiwa na miezi sita, alianza kuugua homa za mara kwa mara na malaria, tulilazwa kila wakati hospitalini kwa matibabu,” anasema.

Anasema hali ilizidi kuwa mbaya kadri muda ulivyosonga mbele.

“Wakati huo baba yake alikuwa bado yupo hai, Shukuru alikuwa anabadilika badilika rangi ya ngozi yake, alikuwa wa bluu, njano na wakati mwingine mweupe hasa asipobwia sukari,” anasema.

Huku akitokwa machozi, mama huyo anasimulia; “baba yake alifariki nikabaki mwenyewe nikimuhudumia mwanangu, alipokosa kula vitu hivyo alikuwa anaumia mno, mwili wake ulikata kata mfano wa gari lililoishiwa mafuta.

Anasema ilifika hatua ikamlazimu kuuza ng’ombe zake 10 na fedha zote alizitumia kutafuta matibabu ya mtoto wake huyo.

“Nimehangaika mno, nimefika hadi Msumbiji, Malawi, Maputo, nimelala njiani mara nyingi, nikitafuta tiba ya mwanangu,” anasema.

Anasema ndipo alikutana na mganga mmoja ambaye alimueleza kuwa mwanawe ana tatizo kubwa tumboni mwake, kwamba nyama za ndani zimekuwa ngumu, hivyo matibabu yake ni kumpatia vitu hivyo.

Mwanabibi anasema Shukuru alipokosa vitu hivyo aliumwa zaidi, nyama zilikuwa zikijikata kata ndani ya tumbo kiasi cha mtu kusikia sauti kwa nje.

“Nilinyong’onyea, niliposhindwa kumpatia vitu hivyo, mimi ni mjane, maisha sasa ni magumu, vitu hivyo ni ghali, alipokosa alikuwa anabadika na kuwa wa bluu hadi nywele.

“Kila alipopata maumivu ya kichwa, jicho la kushoto nalo lilivimba na kuzingirwa na damu ambayo huganda na kuwa donge la damu, nilimsaidia kulitoa,” anasema kwa huzuni.

Anasema; “Wakati mwingine aliniambia anahisi kuna kitu kinaanguka mgongoni, ghafla anaanza kutapika damu, ambayo hutoka mabonge mabonge (imeganda) kama kinyesi cha mbuzi na mwisho hutoka mbichi, namsaidia kuitoa.

Anasema Shukuru sasa yupo kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Mgomba, kutokana na hali hiyo hushindwa kuhudhuria vema masomo yake.

“Ninalazimika kumsindikiza kila anapopata nafuu, nabeba begi lake nampeleka shuleni, kila wanapofanya mtihani matokeo yake huwa mazuri sawa na wale wanaohudhuria kila siku, inanishangaza,” anasema.

Tatizo ni nini?

Uchunguzi wa awali aliofanyiwa Shukuru katika Hospitali ya Taifa Muhimbili umeonesha kuwa anaugua ugonjwa wa selimundu (sickle cell).

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu wa hospitali hiyo, Stella Rwezaula ambaye amemfanyia uchunguzi huo amebaini mtoto huyo pia ana upungufu mkubwa wa madini chuma mwilini mwake.

“Ripoti ya awali niliyokabidhiwa inaonesha Shukuru aliwahi kulazwa Muhimbili Machi, mwaka jana, alikuwa analalamika kupata maumivu makali ya kichwa, lakini kabla ya matibabu kaka yake aliomba apewe ruhusa ya kuondoka, wakarudi nyumbani,” anasema.

Anasema hakubahatika kumuona, hadi waliporudi hospitalini hapo Mei 26, mwaka huu na kuanza kumfanyia uchunguzi.

 “Bahati nzuri nilikuwa zamu wiki hiyo, baada ya uchunguzi, nimegundua ana tatizo la selimundu, ni ugonjwa ambao amezaliwa nao,” anasema.

Jinsi inavyotokea

Dk. Rwezaula anasema ni ugonjwa wa kurithi ambao mtu huzaliwa nao iwapo baba na mama yake wana vinasaba vya ugonjwa huo.

“Chembechembe nyekundu za damu huwa zinashambuliwa, zinaharibika pindi tu zinapotengenewa,” anasema.

Anaongeza; “badala ya kuwa na umbo la mviringo ambalo linatakiwa, huwa zina umbo la nusu duara (mundu), hivyo bandama na viungo vingine vinavyohusika na kusaga zile chembe chembe zisizofaa mwilini, huziharibu.

Anasema dalili alizokuwa nazo Shukuru tangu utotoni ni za selimundu lakini bahati mbaya hakuweza kufanyiwa vipimo mapema kubaini.

Kwanini hubadilika rangi

Dk. Rwezaula anasema mwili wa Shukuru ulibadilika rangi na kuwa mweupe kwa sababu ya kule kuharibiwa haraka kwa chembe chembe nyekundu za damu.

“Chembe chembe hizo zinapoharibiwa anapata upungufu wa damu, mtu yeyote akipatwa na hali hiyo mwili wake huwa mweupe.

 “Chembe chembe hizo zikishasagwa husababisha nyongo kutengenezwa kwa wingi mno na kushindwa kutosheleza, kukaa katika mfuko wake.

“Nyongo hiyo hutoka nje na kusambaa mwilini,  hapo mtu huwa na rangi ya njano hasa kwenye macho,” anasema Daktari huyo.

Anasema watu wanaougua selimundu kwa kawaida huvimba kichwa hasa wakati ambao chembe chembe nyekundu zinapovimba na kubadilika umbo kutoka katika umbo lake la kawaida.

“Huwa zinakwenda kuziba kwenye mishipa ya damu hasa ile midogo midogo, hivyo damu hushindwa kupita kirahisi, anapata maumivu makali,” anasema.

Anasema anatakiwa kunywa maji mengi ambayo huenda kusafisha katika maeneo yaliyoziba na damu kupita kirahisi.

Sababu ya kula vitu hivyo

Dk. Rwezaula anasema ni kutokana na mwili kukosa virutubisho muhimu vinavyohitaji hasa madini ya chuma.

“Mwili unapokosa madini hayo, mtu hula vitu vya ajabu, kwa mfano wajawazito utawaona wakila udongo, mkaa, mchele na hata magodoro,” anasema.

Anasema hiyo ni kwa sababu mwili hulazimika kutafuta madini hayo kwa namna yoyote.

“Ndivyo ilivyokuwa kwa Shukuru, kwa kuwa alikuwa hapati vyakula vyenye wanga na vitamin, mwili wake ulipungukiwa madini chuma,  alipokuwa akila sukari, mafuta na maziwa alipata madini hayo ndiyo maana alipata unafuu,” anasema.

Si matibabu sahihi

Daktari huyo anasema wagonjwa wa selimundu hutakiwa kumeza vidonge vya folic acid kila siku ambavyo huwasaidia kutengeneza damu.

“Tayari ameanza kutumia vidonge hivyo, ni malighafi inayomsaidia mgonjwa wa selimundu, mwili wake kutengeneza damu,” anasema.

Anafafanua; “kwa kawaida, chembechembe nyekundu za mtu asiye na ugonjwa huishi siku 90 hadi 120 kisha huzeeka na kufa. Lakini mgonjwa wa selimundu, zake huishi siku 10 na kufa, damu yao inaharibiwa haraka, hivyo folic acid huusaidia mwili wake kutengeneza damu,” anasema.

Daktari huyo anasema Shukuru atatumia dawa hizo maisha yake yote kuanzia sasa.

“Nimemshauri mama yake, huu ni ugonjwa wa kurithi ni vema awalete watoto wake wanne nao wachunguzwe afya zao, inawezekana sasa  hawaugui lakini kumbe wamebeba vinasaba hivyo,” anasema.

Anasema amempa elimu sahihi mama huyo kuhusu ugonjwa huo ili imsaidie akirudi nyumbani, asipewe taarifa zisizo sahihi na watu wengine akashindwa kumuhudumia vema mwanawe.

Uchunguzi zaidi

Dk. Rwezaula anasema wataendelea kumfanyi uchunguzi zaidi mtoto huyo kwani ugonjwa huo huathiri ubongo, figo, ini na viungo vingine vya mwili.

“Hasa wale wanaougua selimundu kali, ni rahisi kuathirika, hivyo tutaendelea kumwangalia kwa ukaribu afya yake,” anasema.

Ndoto ya udaktari

Shukuru sasa anaendelea vizuri tangu alipoanza kupewa matibabu sahihi dhidi ya ugonjwa huo.

Anasema ameanza kula vyakula vya kawaida, anamshukuru Mungu na madaktari waliomsaidia kwani ameteseka kwa muda mrefu.

“Nimeteseka sana, lakini tangu nimefika hapa Muhimbili nimepata tiba nzuri, nashukuru sana wametupokea vizuri, wamenitibu vizuri na sasa naendelea vizuri,” anasema.

Anasema atakapojaaliwa kurudi nyumbani ataongeza juhudi kwenye masomo yake ili aje kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya damu.

“Nataka nisome fani hiyo ili siku moja niweze  kuwasaidia watu wengine wanaoteseka kama mimi, nataka niwasaidie kama mimi nilivyosaidiwa,” anasema.

Furaha ya mama

Mama yake anasema anawashukuru mno madaktari kwa kumsaidia mtoto wake.

“Sina cha kuwalipa, tangu nimekuja Muhimbili hadi sasa mwanangu hajatumia tena sukari, maziwa wala mafuta.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles