25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

KINGUNGE AWATAJA VIGOGO WATATU WASALITI CCM

Mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru, akizungumza na Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda (katikati) na mwandishi Evance Magege, wakati wa mahojiano maalumu nyumbani kwake Kijitonyama, Dar es Salaam juzi.

NA EVANS MAGEGE –Dar es Salaam

MWANASIASA mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru, amesema hatua ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwaadhibu makada wake hivi karibuni ni mwendelezo wa makosa yaliyoongozwa na kuratibiwa na viongozi wakuu watatu wa chama hicho wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais takribani miaka miwili iliyopita.

Kingunge mmoja wa waasisi wa CCM aliwataja viongozi hao ambao alisema kimsingi ndio wanapaswa kubeba dhamana ya usaliti ndani ya chama hicho kuwa ni Mwenyekiti mstaafu, Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu,  Abdulrahman Kinana.

Kingunge aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na MTANZANIA Jumapili yaliyofanyika  wiki hii katika makazi yake yaliyoko eneo la Victoria, Dar es Salaam.

Katika mahojiano hayo ambayo yalidumu kwa saa moja na dakika 22,  Kingunge ambaye amepata kufanya kazi na serikali za awamu zote nne, alizungumzia demokrasia, haki, utendaji wa Serikali ya awamu ya tano na hali ya siasa, ikiwamo uamuzi wa hivi karibuni uliochukuliwa na CCM.

Kuhusu yaliyotokea wiki iliyopita ndani ya CCM, ikiwa ni pamoja na kuwaadhibu wanachama wake kwa makosa ya usaliti, Kingunge alisema si mapya bali ni mwendelezo wa makosa yaliyotokea wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais kupitia chama hicho mwaka 2015.

Aliyataja makosa yenyewe kuwa ni yale ya ukiukwaji wa taratibu na kanuni za kumpitisha mgombea wa urais.

Alisema uongozi wa CCM wa wakati huo chini ya uenyekiti wa Kikwete, Makamu Mwenyekiti Bara, Mangula na Katibu Mkuu Kinana, kwa pamoja walifanikiwa kushawishi Kamati Kuu (CC) kuvunja Katiba na kanuni za chama hicho.

Kingunge ambaye hii si mara yake ya kwanza kueleza kile alichokiona ni ukakasi wa mfumo uliotumika na vikao vya juu vya CCM kumpata mgombea wa kiti cha urais, alihoji katika mazingira ya leo ya kuwashuku fulani ni wasaliti wakati unajua kuna watu walikiuka taratibu na kanuni za chama, ni nani anayepaswa kuitwa msaliti?
Kwa muktadha huo, alisema CC ilishindwa kufanya kazi yake kama inavyoelekezwa na katiba na kanuni zake, hivyo ikajikuta imekataa kuwasikiliza, kuwaona na kuwahoji wagombea 38 wa urais, badala yake wakakubaliana na mapendekezo ya majina yaliyotoka kwa Kikwete.

“Huko kwenye NEC baada ya vurumai kubwa ndiko wakapatikana hao wagombea watatu ambao walipelekwa kwenye mkutano mkuu na mwisho wake akapatikana Bwana Magufuli,” alisema.

Kingunge alisema kuwa imekuwa kama alivyosema Mwalimu Nyerere, kwamba ukishakula nyama ya binadamu hutakoma, utaendelea tu.

KUFUKUZA WANACHAMA

Akizungumzia hatua ya CCM kuwafuta uanachama baadhi ya viongozi, kuwapa onyo na kuwasamehe wengine kwa sababu ya kile kinachoitwa usaliti, mwanasiasa huyo alisema anastaajabu adhabu hiyo kuwagusa baadhi wakati msingi wake ni mchakato wa kumpata mgombea urais 2015.

“Kwa hawa waliohukumiwa, wamehukumiwa kwa usaliti wa kuendana na mchakato kumpata mgombea wa urais, sasa swali linakuja, hapo katika mchakato wa kumpata mgombea urais, aliyesalitiwa ni nani? Ni CCM ndiyo iliyosalitiwa ama kuna mgombea fulani maalumu ambaye ndiye aliyesalitiwa?

“Kwa ninavyoijua Katiba ya CCM na kanuni zake, hadi wakati ule wa kumtafuta mgombea, mazingira yalikuwa ya ushindani huria (huru),” alisema.

Kwa mtazamo wake, alisema wagombea wote walifuata taratibu za kuchukua fomu hadi kutafuta wadhamini na kuhoji hadi katika hatua hiyo nani ni msaliti na alimsaliti nani?

“Kwa sababu huo ulikuwa ni utaratibu ndani ya CCM… wadhamini waliomuunga mkono mmoja hawakuruhusiwa kwa mwingine. Sasa wadhamini waliomuunga mkono ‘A’ ndio walikuwa wasaliti kwa sababu hawakuwaunga mkono wengine waliobaki?” alihoji Kingunge.

Kwa mujibu wa Kingunge, vikao vya juu vya CCM wajumbe walikuwa na haki ya kujadili sababu za baadhi ya wagombea kuwamo na wengine kutokuwamo.

 “Sophia Simba alimsaliti nani, Madabida alimsaliti nani na katika ngazi gani? Ndiyo maana nasema hili suala lote hili ni mwendelezo wa yaliyotokea 2015, Agosti 10 kule Dodoma, pale ambapo uongozi wa chama, kundi la watu watatu likiongozwa na Kikwete ndilo lilifanya CC na jopo la wazee wastaafu washirikiane na wakubaliane kuvunja katiba na kanuni na wao kuchukua jukumu la kuteua watu watano nje ya utaratibu uliowekwa na chama,” alisema.

Alihoji wanachama waliofukuzwa wamemsaliti nani kwa sababu wakati wa mchakato kila mwanachama alikuwa na mgombea wake anayemuunga mkono.

MAAMUZI YA KAMATI YA MAADILI

MTANZANIA Jumapili lilimkumbusha kwamba majina hayo yalipitishwa katika Kamati ya Maadili ya chama.

Lakini katika maelezo yake Kingunge alifafanua kwamba Kamati ya Maadili wakati wa kipindi hicho ilikuwa ni kitengo ndani ya Ofisi ya Katibu Mkuu, hivyo haitambuliwi ndani ya Katiba ya CCM.

Alisema kwa sasa anaona kuna jitihada za kutaka kuibadili Kamati ya Maadili kiwe kikao rasmi.

“Katika suala la maadili ndani ya chama, mkuu wa maadili ni NEC na katika ngazi zote za chama kuanzia taifa hadi matawi,” alisema.

Kwa mujibu wa Kingunge, kuanzia mwaka 1982 wakati ulipoanzishwa mfumo mpya wa chama, ilikuwapo Tume ya Udhibiti na Nidhamu.

Alisema tume hiyo ilikuwa na hadhi ya idara ya chama, lakini baadaye yakafanyika marekebisho, hivyo suala la maadili halikujumuishwa katika hadhi ya idara ya chama na badala yake likawa ndani ya kitengo ambacho kipo chini ya Ofisi ya Katibu Mkuu.

“Kwa hiyo, Kamati ya Maadili haina majukumu ya kikatiba ya kuwa na kauli juu ya nani awe au asiwe mgombea, lakini inaweza kuishauri CC na NEC na kamati hiyo haiwezi kutoa ushauri wa kuvunja katiba na anayeshauriwa ndiye mwamuzi,” alisema.

MADARAKA YA KIIMLA

Akiendelea kufafanua hoja hiyo, Kingunge alisema madaraka yanatakiwa kujengeka kwa misingi ya hoja na si misingi ya kiimla.

Alisema pamoja na kwamba yeye si mwanachama wa CCM kwa sasa, lakini ana haki za kutoa maoni juu ya uamuzi huo kama raia wa Tanzania.

Kwamba kama raia wa nchi hii, anataka vyama vya siasa vilivyopo vijengeke katika misingi ya demokrasia.

“Hatuwezi kuwa na vyama feki feki tu, kwa hiyo inavyotokea kwamba chama cha siasa hapa nchini kinafanya vitabia ivitakavyo bila kusimamia misingi ya demokrasia, sisi kama raia tuna haki ya kukihoji na kama kimekosea tutawaambia wamekosea na katika hili CCM imekosea,” alisema.

Alisema pamoja na kwamba ameachana na CCM, lakini ana historia na chama hicho. Alitanabaisha kuwa yeye ni miongoni mwa waasisi wa CCM na alikuwa kwenye jopo la watu 20 waliounda kamati ya kuandaa rasimu ya katiba ya chama hicho (1976-1977).

Alisema kuwa ndani ya CCM amehusika na utangulizi na yaliyomo katika katiba ya chama hicho.

“Watu waliomo CCM waelewe, ile katiba ni kitu kikubwa sana na tuliiunda ili ibebe mema yote ya TANU na ASP, ibebe misingi iliyotuongoza kufanya mambo makubwa sana katika TANU na ASP, misingi hiyo ni demokrasia, haki, usawa na utu.

“Sasa wanaodai kwamba wanaongoza CCM wakifanya mambo ambayo hayafanani na ile tuliyoiunda, mimi inanipa tabu na katika hilo siwezi kunyamaza nitasema tu… naweza nikasema nyinyi CCM yenu mliyoiunda ni nyingine, siyo yetu ya akina Kingunge na wenzake,” alisema.

CCM INAINGIA PAGUMU

Kingunge alisema CCM inajiingiza katika hali ngumu, kwa sababu ya baadhi ya viongozi ndani ya chama hicho kujiaminisha kuwa wanajua kila kitu.

“Hii inatokana na jambo moja, lazima niliseme. Binadamu sisi tumepewa vichwa na ndani ya vichwa kuna akili ambayo imepewa kazi ya kufikiri, lakini hakuna binadamu anayejitosheleza katika masuala ya kufikiri, sasa ukifika mahala kwamba baadhi ya binadamu wanajiaminisha kwamba wao wanajua kila kitu, ndio chanzo cha matatizo,” alisema.

CCM HAITAKI MIJADALA

Kingunge alisema kwa yanayofanywa sasa ndani ya CCM, ni wazi inaonekana haitaki mijadala.

 “Mkutano Mkuu wa Taifa ulifanyika kwa saa tatu, mkutano ambao ulikuwa na jukumu la kujadili mabadiliko ya katiba… saa tatu umwekwisha kila kitu… sasa nasema tunalo tatizo katika nchi hii, kwanza mijadala nje ya chama haitakiwi, sasa hawa wenye nchi yao kwahiyo itakuwa ada yao ni kupewa amri tu?

“Wanapewa amri na watawala na ada yao itakuwa ni kutii amri za watawala? Hakuna kuhoji. masuala yanayotokea katika nchi yao, hawa raia hawana haki ya kuyajadili,” alisema.

Akithibitisha kauli yake hiyo, Kingunge alitolea mfano jinsi wale wanaotangaza baa la njaa wanavyopewa adhabu.

NCHI IENDESHWE AU IONGOZWE?

Alisema nchi imefika mahali sio pazuri kwa sababu ya viongozi na alitoa mifano ya njia mbili za kufuatwa.

“Kuna njia mbili, ama nchi iendeshwe au nchi iongozwe, kama mnataka nchi iongozwe maana lazima mkubali wananchi wenyewe watoe maoni yao halafu mnakwenda, lakini mnataka kuiendesha nchi na mnajua matokeo ya nchi kuiendesha,” alisema.

Aliongeza kwa kusema kuwa ni lazima kila Mtanzania, kuanzia viongozi, wote kujitahidi kuondoa munkari na hasira.

“Hamuwezi kuwa na nchi viongozi wanaonekana wana hasira tu na raia nao wataonekana kuwa na hasira, tukifika hapo nchi haiendi. Nasema tuwe watulivu sote, wakubwa kwa wadogo ili tuwe wanyenyekevu kwa sababu sisi ni watu tu, ukiwa mkubwa ni mtu, ukiwa mdogo wewe ni mtu.

“Mkubwa mambo yake ya msingi anayoyafanya ni yale yale anayoyafanya mtu mdogo, kwahiyo sisi wote ni watu ndiyo maana Katiba ya CCM inasema binadamu wote ni sawa na kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa utu wake,” alisema.

Aliongeza kwa kusema kama Watanzania wote wanataka kuijenga nchi, wanaweza kuijenga, lakini kama wanataka kuibomoa wataibomoa.

CCM IMECHOKA

Kingunge alikwenda mbali na kusema kwamba CCM si kwamba imeishiwa pumzi tu, bali imechoka.

Alisema mazingira hayo yanakifanya chama hicho kukosa nguvu ya kwenda mbele kwa sababu ndani yake kumekosekana umoja.

“Hakuna suala kubwa katika ‘organization’ (taasisi) yoyote kama umoja, muundo wowote wa watu wanaotaka kufanya jambo kwanza kabisa ni umoja, Mwalimu Nyerere alitufundisha wakati ameanzisha TANU na wenzake 17. Alisema suala la kwanza ni umoja, Waafrika tuungane kumtoa mkoloni.

“Na katika harakati za kujenga umoja kunatokea vitu vingi, zinatokea nguvu nyingine zinazotaka kuwaweka pembeni ili mtengane… uongozi unatakiwa kuelewa masilahi ya chama ni nini… kuna kuelewa masilahi yako na vikija vishawishi vya kujitenganisha na wenzako, unajiuliza kama linafifisha harakati au linaendeleza, hivyo unajirudi na kuendelea na mapambano,” alisema.

WALIFUKUZWA CCM

Katika hatua nyingine, Kingunge aliwatia moyo watu waliovuliwa uanachama wa CCM na wale waliopewa onyo.

Aliwataka wasibabaike kwa sababu kama bado wanaipenda CCM waombe warudishwe.

Lakini akasema: “Dunia si CCM, kwa sababu kabla yake kulikuwa na TANU. Kwani binadamu hawakuishi?”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles