23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

KESI ZA KISIASA, DAWA ZA KULEVYA, UJANGILI KUENDESHWA HARAKA

Na JANETH MUSHI

-ARUSHA

MAJAJI wafawidhi na mahakimu wafawidhi wa mahakama zote nchini, wametakiwa kuzipa msukumo kesi zenye mvuto katika jamii zikiwemo za kisiasa kwa kuzisikiliza haraka ili kutoa fursa kwa chombo hicho kufanya kazi bila shinikizo na kwa uhuru bila kuingiliwa na mhimili mwingine.

Agizo hilo lilitolewa jana na Kaimu Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim Juma, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mafunzo ya siku tatu na mkutano wa siku mbili kwa Majaji wa Mahakama ya Rufaa, Majaji Wafawidhi na Majaji wa Mahakama Kuu kutoka mikoa yote  nchini.

Prof. Juma alizungumzia umuhimu wa mahakama kuisoma na kuielewa jamii na kusisitiza kuwa licha ya mhimili huo kuwa huru kikatiba, lakini kuna aina ya mashauri yanayopewa umuhimu na jamii ambayo yasipoweza kushughulikiwa mapema yanaweza kuzua maswali kuhusu uhuru wa chombo hicho.

Alitoa mifano ya baadhi ya mashauri ambayo alisema yakicheleweshwa mhimili mwingine utapiga kelele kuwa ni mapambano ya rushwa, dawa za kulevya, mapigano ya wakulima na wafugaji, ujangili, ugaidi, masuala ya kiuchumi na uwekezaji mkubwa.

“Ingawa tunasema mahakama ni huru kikatiba, lakini kuna mashauri fulani ambayo yamepewa umuhimu na jamii, tukichelewesha mashauri kwenye mambo hayo mhimili mwingine utapiga kelele na hatutaki kuwa katika ‘pressure’ yoyote kutoka katika mhimili mwingine,” alisema.

Kuhusu suala la maadili, Prof. Juma, alisema vitendo vya rushwa, lugha isiyofaa haviwezi kumalizwa na mahakama pekee kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) na mawakili wasipokuwa tayari kushirikiana.

Katika hilo alisema wataangalia namna ya kuwashirikisha ili kufikia malengo na wananchi kupata haki.

Kuhusu utekelezaji wa mpango mkakati wa mahakama ulioanza Septemba mwaka jana ambao una nguzo mbili ambazo ni utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali, majaji walipata nafasi kujadiliana namna ya kutumia rasilimali kuhakikisha kazi ya utoaji haki inafanyika na utoaji wa haki kwa wakati.

MLUNDIKANO WA KESI

Prof. Juma pia alisema wamejadiliana changamoto mbalimbali ikiwamo ya mlundikano mkubwa wa kesi unaochangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo upungufu wa majaji, mahakimu na watendaji wa mahakama.

Kuhusu upungufu wa majaji ambapo kwa mujibu wa ripoti ya taarifa ya mahakama Mwaka 2014/15 Majaji wa Mahakama Kuu walikuwa 98, mwishoni mwa mwaka jana idadi hiyo ilipungua hadi kufikia 75 baada ya majaji kustaafu na kwa sasa wako 69.

Alisema ukigawanya kesi zote  kila Jaji anabeba majalada 478 na kwa wastani jaji ana uwezo wa kusikiliza kesi 178 kwa mwaka na kuwa wamelazimisha jaji kumaliza kesi 220 kwa mwaka.

“Upungufu wa majaji unachangia kushindwa kumalizika kwa mashauri, Mahakama ya Rufaa uwezo wao ni kusikiliza mashauri 200 kwa mwaka ila kutokana na mlundikano kutahitajika kuwepo na majaji wengine watano wa Mahakama ya Rufaa, ili kuondosha hayo majalada na kutoa haki kwa wakati,” alisema na kuongeza: 

Akitolea mfano wa matokeo ya changamoto hiyo alisema Kanda ya Dar es Salaam ndiyo inaongoza kwa kuwa na mashauri mengi ya zamani mengine yakiwa yana miaka 10.

Kaimu Jaji huyo alisema suala lingine linalochangia kesi kulundikana ni masilahi kwa watumishi hasa wa ngazi za chini ambao wengi wao hufanya kazi zaidi ya muda wa kazi uliopangwa bila malipo yoyote.

Zaidi aliitaja changamoto nyingine kuwa ni majengo ambako kunahitajika Mahakama za Mwanzo zaidi ya 2,000 ili wananchi wapate haki.

 Pamoja na hilo, alisema mikoa 12 haina Mahakama Kuu.

“Upatikanaji wa haki unategemea mashauri yanavyofunguliwa na muda yanapokuwa mahakamani na tumejiwekea muda, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa tumejiwekea lengo kesi zisikae miaka miwili, Mahakama za wilaya mwaka mmoja na miezi 6 kwa mahakama za mwanzo.

“Mpango mkakati wa mwaka huu ni kuhakikisha mashauri yote ambayo ni mlundikano katika ngazi zote za mahakama, kuhakikisha hukumu zinasomwa ndani ya siku 90, majaji na mahakimu wanazingatia hatua za uendeshaji wa mashauri, kusikiliza mashauri kwa wakati, kuongeza uwajibikaji na uwazi,” alisema Prof. Juma.

Akizungumzia mafunzo hayo, alisema yamefanyika ya aina tatu kwa makundi tofauti ya majaji likianziwa na Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji Wafawidhi na Majaji wa Mahakama Kuu, ambapo baada ya mafunzo ya kila kundi kulifanyika mafunzo ya siku mbili yaliyojumuisha makundi yote.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, majaji wafawidhi walijifunza juu ya usimamizi wa mashauri na majaji wengine walijifunza juu ya uongozi na usimamizi wa mabadiliko, lengo likiwa ni kutazama taratibu zilizopo na kuona namna zinavyoweza kutumika kuharakisha usikilizaji wa mashauri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles