29.6 C
Dar es Salaam
Saturday, May 21, 2022

Katibu Mkuu Wizara ya Maji atoa wiki sita wananchi kupata maji

Na Mohamed Saif-Iringa

KATIBU Mkuu mteule wa Wizara ya Maji, Anthony Sanga, ametoa wiki sita kwa Mamlaka ya Maji Iringa (Iruwasa) na Wakala ya Maji Vijijini (Ruwasa) kuhakikisha wananchi wa eneo la Ismani Tarafani Wilayani Iringa, wanapata huduma ya maji kupitia mfumo wa maji wa Iruwasa uliofika eneo la Kijiji cha Kising’a.

Sanga ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wizara hiyo, alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja kabla ya juzi Rais John Magufuli kumteua kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.

Akiwa katika ziara yake mkoani Iringa, alipofika Ismani kwenye mradi wa maji wa Ismani-Kilolo, Sanga hakukubaliana na taarifa ya wataalam wanaotekeleza mradi huo iliyobainisha kwamba wananchi wataanza kunufaika na huduma ya maji Juni, 2021 baada ya mradi kukamilika ikiwemo kukamilika kwa ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji.

“Sikubaliani na mapendekezo yenu kwamba wananchi waanze kupata maji mwakani baada ya mradi mzima kukamilika, nimejionea hali ya maji hapa Ismani si nzuri, hatuwezi kuendelea kusubiri hadi tenki la maji likamilike ndipo wananchi waanze kupata huduma wakati tunao uwezo wa kutumia utaalamu wetu kuhakikisha wanapata huduma kabla ya hilo tenki kukamilika,” alisema Sanga.

Alisema maelekezo ya Wizara ya Maji ni kwamba miradi yote inayopeleka huduma ya maji kwa wananchi ikamilike haraka kwani Serikali haipo tayari kuona wananchi wakitaabika kwa kukosa huduma ya maji.

“Maelekezo yangu ambayo ni maelekezo ya Waziri wa Maji ni kwamba miradi yote inayopelekea huduma kwa wananchi ijengwe kwa haraka. Hatuna sababu ya kuwacheleweshea huduma wananchi, Serikali ya Rais Magufuli haiwezi kuvumilia kuona wananchi wakiteseka kwa kukosa huduma ya maji,” alisema Sanga.

Alisema  ifikapo Julai 20 wataalam wa Ruwasa na Iruwasa wawe wameanza utekelezaji wa maelekezo ya kuhakikisha wananchi wa Ismani wanapata huduma haraka kwani fedha zipo tayari na kwamba Sh milioni 200 kitapelekwa mkoani humo kwa ajili ya mradi husika.

“Gharama za kufikisha maji hapa Ismani tarafani ni  Sh milioni 600, ninawahakikishia ifikapo Julai 20 mtakuwa tayari mmepokea Sh milioni 200 na ninawapa siku mbili hizi kuhakikisha mnajipanga kwa kuanza kutekeleza ikiwa ni pamoja na kutafuta vijana wa kuchimba mtaro wa kulaza mabomba,” alisema Sanga.

Alisema shughuli ya uchimbaji mitaro ifanywe na wananchi wa maeneo hayo ikiwa ni njia mojawapo ya kuwaongezea kipato na taratibu za ununuzi wa mabomba zianze mara moja.

Kwa upande wake Meneja Ufundi wa Iruwasa, Fabian Maganga, alisema ujenzi wa mradi huo ulianza Aprili 15, mwaka huu na kwamba tayari Wizara ya Maji imeshatoa Sh milioni 450.

Alisema hadi kukamilika kwa mradi huo, Sh bilioni 9.27 zitakuwa zimetumika ambapo zaidi ya wananchi 58,821 kutoka vijiji 29 watanufaika.

Alisema mradi utatumia chanzo cha maji cha Mto Ruaha mdogo chenye maji ya kutosha na maji ya chanzo cha kijito cha Mgela yatakuwa yanatumika kwa dharura endapo itabidi kufanya hivyo.

“Kwa usanifu tuliofanya, uzalishaji wa maji kutoka vyanzo hivyo utakidhi mahitaji ya mradi hadi mwaka 2038 na hapatakuwa na sababu ya kuchimba visima,” alisema  Maganga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
191,701FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles