23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

JOKATE: UVCCM LAZIMA IBADILIKE KUANGALIA CHANGAMOTO ZA VIJANA

JOKATE Mwegelo

Na JOHANES RESPICHIUS,

JOKATE Mwegelo ni miongoni mwa vijana wenye ushawishi katika jamii kutokana na kuwa na vipaji vingi huku akijituma katika kuitumikia jamii.

Jokate ambaye pia ni mwanamtindo alianza kujulikana mwaka 2006 baada ya kushinda Miss Tanzania namba mbili.

Pamoja na majukumu mengine aliyonayo, mwanadada huyo, Aprili mwaka huu aliteuliwa kuwa Kaimu Katibu wa Uhamasishaji wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa.

Hivi karibuni gazeti hili limefanya mahojiano na Jokate ambapo pamoja na mambo mengine amezungumzia mikakati yake ndani UVCCM na changamoto anazokumbananazo.

MTANZANIA: Wengi wanayafahamu maisha yako kwenye sanaa, pengine ni lini uliingia kwenye siasa?

JOKATE: Bibi yangu alikuwa muasisi wa CWT Mkoa wa Ruvuma kwa hiyo nimekulia katika mazingira ambayo bibi alikuwa akiishi kwa kupenda watu wengi licha ya kutofanikiwa kusoma alihakikisha watoto wake wanasoma.

Alikuwa mtu anayependa sana watu kwa hiyo nimekulia katika mazingira ya kujitoa sana katika sehemu zote ambazo nimekuwa nikisoma nimejikuta watu wakiniamini kuwaongoza.

Kwa hiyo ni kitu ambacho nimekuwa nikikifanya na kiko kwenye nafsi yangu kwamba napenda kusaidia watu katika sehemu moja na kwenda sehemu nyingine hivyo haikuwa kazi ngumu kuingia kwenye siasa kwani nina kipaji cha kuongoza.

Lakini kuingia rasmi kwenye siasa na kuonekana sana ilikuwa ni mwaka huu kwa sababu ndio mwaka nilioshiriki kikamilifu kwenye uchaguzi baadaye nikateuliwa kuwa Kaimu Katibu Idara ya Uahamasishaji na Chipukizi UVCCM Taifa.

MTANZANIA: Unaitumiaje nafasi hii ya uhamasishaji kuwavutia vijana wanaotarajia au kutamani kuingia kwenye siasa?

JOKATE: Kama UVCCM lazima tuwe chombo cha kutiliwa na vijana kuweza kufikia viongozi ambao wapo serikalini, ni lazima ibadilike na kugeukia kuangalia changamoto walizonazo vijana kuweza kuzisemea.

Vile vile kuhakikisha tunawahamasisha vijana washiriki, si tu kwenye siasa lakini hata kujiongoza wao wenyewe au katika sehemu waliyopo na kutengeza njia inayovutia wengine.

Kijana anapaswa kutambua kuwa uongozi unapaswa kuanzia sehemu alipo kwa kuwaongoza wengine hususani kuwa mbunifu kwa kipaji na kazi yake.

MTANZANIA: Changamoto zipi unazokumbananazo baada ya kuingia kwenye siasa?

JOKATE: Changamoto zipo na hakuna mtu ambaye anaishi bila kuwa nazo lakini ni jinsi unavyotumia vizuri vitu ulivyonavyo kuzitatua.

MTANZANIA: Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ni wasanii wengi walioshiriki kuifanyia kampeni CCM, ilikuwaje mpaka wewe ukapewa nafasi hii?

JOKATE: Unajua ukiona umeaminiwa kushika nyadhifa fulani lazima umshukuru Mungu kwa sababu ni kipindi tu ambacho utakuwapo lakini pia utatoka na kuja wengine si kwamba ni nafasi ya kuwapo milele.

MTANZANIA: Uteuzi wako ulizua manung’nuniko mengi, wewe unawaza nini katika hili?

JOKATE: Hakuna anayeweza kukwepa maneno na ni kawaida kwa mtu yeyote akichaguliwa si watu wote wanaweza kukuelewa kwa wakati huo lakini kinachoangaliwa zaidi ni kufanya kazi kwa ajili ya Watanzania wote.

Nimejitoa sana kwa ajili ya watu hata nilipokuwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), nimefanya vizuri sana katika masomo yangu na nilibakizwa kusoma Shahada ya uzamili pengine nisingeingia kwenye kusaidia jamii ningekuwa naitwa Dk. Jokate.

Kwa hiyo nikijiangalia mwenyewe na wengine nafikiri walikuwa wamezoea kuniona kwenye sanaa kwamba huyu ni msanii hawezi kuamini lakini nina kipaji cha kutumikia watu.

Ila ni jambo la kuwashukuru kwa kunipa changamoto na kunifanya nisiwe ‘Comfortable’ maana na mtu kuwa Comfortable si vizuri na ndio maana najitahidi kufanya vitu vikubwa.

MTANZANIA: Je una historia yoyote ya kuwa chipukizi ndani ya chama chako?

JOKATE: Hapana sijawahi kuwa chipukizi.

MTANZANIA: Hukuvunjika moyo kuona unachaguliwa halafu watu fulani wanaonekana kuwa na manunguniko?

JOKATE: Sikuvunjika moyo, ni kama kitu cha kukufanya ufanye kazi zaidi na hakuna mtu hata mmoja ambaye hajapata changamoto na akafanikiwa yaani ukiona una changamoto nyingi ujue mafanikio yanakaribia.

MTANZANIA: Nini unakiona mbele yako?

JOKATE: Mbele yangu naona vijana wengi wakiwa wamefanikiwa zaidi katika taifa hili.

MTANZANIA: Una matarajio gani kwenye siasa?

JOKATE: Kikubwa kilichonifanya niingie kwenye siasa na ninachokifanya kwa sasa ni kuwatumikia wananchi kwa weledi ili waweze kufaidi manufaa ya utumishi wangu.

MTANZANIA: Unatarajia kugombea nafasi yoyote kwenye Chama?

JOKATE: Sitarajii kugombea nafasi yoyote hii niliyonayo inanitosha kabisa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles