31.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 5, 2022

Contact us: [email protected]

Jinsi wanafunzi 252 walivyokatisha masomo kwa kupata mimba

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki.

NA WAANDISHI WETU,

SERIKALI imeendelea kuboresha elimu na mazingira ya shule katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kutoa hamasa kwa wanafunzi kusoma huku mkazo ukiwekwa kwa watoto wa kike.

Kutokana na changamoto mbalimbali wanafunzi wengi wamejikuta wakiishia katika shule za msingi ama kidato cha nne jambo ambalo linaweza kuwa kikwazo kwa serikali kuweza kufanikisha adhma yake ya kuwakomboa kielimu.

Zipo sheria zinazowabana watu wanaojihusisha kimapenzi na wanafunzi ambapo mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali yakiendelea kupiga vita matukio hayo.

Hata hivyo matukio hayo bado yameendelea kuwepo kwani katika baadhi ya maeneo nchini uhalifu huo unaendelea kwa kasi kubwa.

MTANZANIA limefanya uchunguzi katika mikoa mbalimbali nchini kujua ukubwa wa tatizo hilo.

MTWARA

Shule ya Sekondari Nanyamba iliyoko mkoani Mtwara ni miongoni mwa shule zilizokumbwa na tatizo hilo ambapo kwa mwaka huu wanafunzi wanane wa kidato cha pili na nne wamepata mimba.

Kutokana na tukio hilo walimu wanane (wa kiume wanne na wa kike wanne) wamehamishwa na kupelekwa shule nyingine.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, Oscar Ng’itu, anasema ameunda tume ili kubaini chanzo cha ujauzito wa wanafunzi hao huku walimu nane wakihamishwa katika shule hiyo.

“Jambo hili limenishitua kutokana na wingi wa wanafunzi hao kupata ujauzito katika kipindi kifupi cha muhula mmoja, nimeamua kuwawajibisha baadhi ya walimu,”   anasema Ng’itu

Anasema wanafunzi hao walikuwa wakificha ujauzito huo hadi wengine kufikia miezi nane bila walimu wao kujua hatua ambayo imemshangaza na kuamua kuwahamisha walimu hao kwa kushindwa kufuata taratibu za shule za kuwapima wanafunzi hao wakati wa kufungua shule na wakati wa kufunga.

Pia walimu wawili waliohamishwa shuleni hapo ambao walikataa majina yao yasiandikwe gazetini, wanasema kitendo cha kuhamishwa kimewatia na kusababisha wanyooshewe vidole na jamii.

Wanasema hatua hiyo imekuwa ikiwatesa na kuwafedhehesha katika mazingira waliyohamia kutokana na jamii kuwahusisha na wanafunzi waliopata ujauzito na kuomba serikali kuwahamisha nje ya wilaya ili waweze kufundisha kwa amani.

Mmoja wa wakazi wa Nanyamba, Said Abdallah, anasema baadhi ya wanafunzi waliokumbwa na kashfa hiyo wengi walikuwa wanaondoka kwao usiku kwa kusingizia kwenda kujisomea.

“Wazazi nao wamechangia kwa kiasi kikubwa kutokana na kushindwa kusimamia na kuchunguza kama kweli nyakati hizo watoto wao walikuwa shuleni.

“Nilichoona mimi wanafunzi wengi wana tamaa ndio maana waliweza kudanganyika kwa vitu vidogo ikiwemo fedha na chips wakaingia katika mahusiano ambayo leo hii yamekatisha ndoto zao,” anasema Said.

Naye Ndiriko Diliku ambaye ni bibi wa mmoja wa wanafunzi waliopata ujauzito, anasema baada ya kupata taarifa hizo alichukua hatua za haraka kwenda zahanati kumpima mjukuu wake na kubaini kuwa kweli ni mjamzito.

“Hali hii imeniumiza sana, katika maisha yangu yote sikuwahi kuona mtoto mwenye umri kama wa mjukuu wangu (miaka 15) anapata ujauizto. Nimefanya jitihada kubwa kuweza kuwasomesha wajukuu zangu wawili na huyu aliyepata ujauzito niliachiwa miaka mingi na mama yake ambaye alielekea Dar es Salaam na hakuwahi kurudi hadi leo.

“Mimi sina nguvu kabisa siwezi hata kulima, lakini pamoja na ugumu wa maisha nilionao nilikuwa najitahidi wajukuu wangu wasome ili baadae waweze kunisaidia, ndio maana mjukuu mkubwa nilihakikisha kuwa anafika sekondari. Nasikitika amefukuzwa akiwa kidato cha pili na hapo alipo ujauzito wake una miezi tisa siku si nyingi atajifungua,” anasema bibi huyo kwa uchungu.

Kwa upande wake mwanafunzi aliyepata ujauzito (jina linahifadhiwa), anasema alikuwa na mahusiano ya kimapenzi kwa muda mrefu na kukiri kwamba fedha azilizokuwa akipewa na mwenzi wake ndizo zilimshawishi hadi akajikuta amepata ujauzito.

“Aliniahidi vitu vingi ndio maana nilikuwa naenda kwao mara kwa mara lakini alipojua kuwa nina ujauzito alinikimbia na hadi sasa sijui alipo,” anasema mwanafunzi huyo.

TANGA

Shule ya Sekondari ya Kwamatuku iliyoko Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, nayo imekuwa ikikumbwa na changamoto hiyo hali inayochangia kukwamisha juhudi za upatikanaji wa elimu bora kwa wanafunzi wa kike.

Faustin Mroso ni Mkuu wa shule hiyo, anasema changamoto ya mimba za utotoni pamoja na utoro vimekuwa vikichangia kuathiri hali ya ufundishaji kwa kiasi kubwa.

Ambapo anasema kati ya Januari hadi Juni mwaka huu, wanafunzi sita wamepata mimba.

Anasema changamoto hizo zimekuwa zikichangiwa na wazazi wengi kukosa mwamko wa elimu kwani hata shule ikipeleka taarifa za kutooneka kwa mwanafunzi wazazi huwa hawatoi ushirikiano.

“Ukiwapelekea wazazi kesi ya utoro au mimba wengi huwa wanawatetea wanafunzi badala ya kushirikiana na uongozi wa shule kuchukua hatua
ili kuweza kumsaidia kijana wao,” anasema Mroso.

Anasema kuwa wanapowabaini wanafunzi wenye ujauzito hupeleka taarifa kwenye ofisi ya kata lakini kesi nyingi zimekuwa zikimalizwa kwa wazazi kukubaliana na mtuhumiwa.

Anasema kwa kipindi cha miaka miwili tatizo hilo liliweza kudhibitiwa wakati wa kampeni ya ‘Niache nisome’ ambapo wanafunzi wa kike waliweza kudhibitiwa ili wasiweze kupata mimba na kukatisha masomo yao.

“Kampeni ili iliweza kuamsha hari ya wazazi kuchangia huduma ya bweni kwa wanafunzi wa kike ili wawe chini ya uangalizi wa walimu na kupata
fursa ya kusoma na hata matokeo yaliweza kuwa mazuri,” anasema.

Hata hivyo anasema baada ya sera ya elimu bure kuanza wazazi waligomea kuchangia huduma ya bweni na kuamua kuwapangishia nyumba vijana wao katika maeneo ya makazi ambapo hakuna uangalizi kwa wanafunzi hao.

KILIMANJARO

Mkoani Kilimanjaro wanafunzi 238 wa shule za msingi na sekondari wamepata ujauzito katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki, anasema Wilaya ya Rombo ndiyo inaongoza ambapo wanafunzi waliopata ujauzito ni zaidi ya 60.

“Sasa sijui mpaka Desemba watakuwa wangapi maana ni kama wanashindana kwa sababu Mei walikuwa 24. Wilaya inayofuatia ni Same ambapo wanafunzi zaidi ya 50 wamepata ujauzito.

“Hili suala si la kufurahi hata kidogo, tumepoteza wasomi ambao pengine hapo baadae wangelisaidia taifa, Jeshi la Polisi fanyeni kazi kuwakamata waliohusika kuwapa ujauzito wanafunzi hao haraka iwezekanavyo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake,” anasema Sadiki.

Kulingana na mkuu huyo wa mkoa, kati ya Januari hadi Mei mwaka huu kulikuwa na mimba 77 kwa mkoa mzima, lakini ripoti ya mwezi uliopita inaonyesha wanafunzi waliopata ujauzito kwa shule za msingi na sekondari ni 238.

Mkuu huyo wa mkoa pia anawataka wananchi kuacha mila potofu za kusuluhishana pale inapobainika kwamba mtoto kafanyiwa unyama wa kupewa mimba, kubakwa au kulatiwa kwani ndio chanzo cha kuongezeka kwa matukio hayo.

“Kuna mila ya kupeana jani linaloitwa Mashale na kusuluhishana, mila hii ni potofu na inawakandamiza watoto wa kike wanaopewa mimba na wale wa kiume ambao hulawitiwa. Jambo hili linasababisha Jeshi la Polisi kufanya kazi katika mazingira magumu sana,” anasema.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa, anasema wanaendelea kufanya uchunguzi na kuwakamata baadhi ya waliohusika kuwapa mimba wanafunzi hao.

Pia anasema makosa ya kubaka na kulawiti katika mkoa huo yameongezeka kwa kasi kutoka 99 mwaka jana hadi kufikia 151 mwaka huu.

Ambapo kuanzia Machi hadi Agosti mwaka huu, watoto 151 walibakwa na 12 walilawitiwa.

MRADI WA KIJANA WA LEO

Shirika lisilo la kiserikali la Amref kupitia mradi wake wa ‘Kijana wa leo’ unaotekelezwa katika kata tisa za Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, umeiingiza Shule ya Sekondari Kwamatuku katika mradi huo ili kuwasaidia wanafunzi kutimiza ndoto zao.

Christina Kavishe ni Mwalimu mlezi wa wanafunzi wa kike shuleni hapo ambaye ameweza kupatiwa mafunzo na shirika hilo kuhusu malezi ya vijana
upande wa afya na jinsia.

Anasema changamoto zingine zinazoathiri makuzi ya kimaadili kwa vijana ni kutopewa maarifa na taarifa sahihi jinsi ya kutumia miili yao bila kuathiri ndoto zao.

Kuhusu mimba anasema nyingi zinahusisha jamaa wa karibu wakiwemo ndugu, baba mdogo au mjomba ambapo wakati mwingine wazazi hufanya makusudi ili mwanafunzi asiweze kuendelea na masomo.

“Kwa huku Handeni bado jamii nyingi hazijaona umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike, hivyo kunafanyika njama za makusudi kuwakosesha fursa
hiyo kwa kuwapatia ujauzito,” anasema Kavishe.

Mwalimu huyo anasema kupitia mradi huo wanafunzi wengi wameweza kuelimika na hivyo kujitambua na kujua malengo yaliyowapeleka shule tofauti na awali.

“Kwa sasa suala la utoro hakuna kwani wanafunzi wameelewa nini maana ya shule na wanajua namna ya kuepuka vishawishi ili wasiweze kupata mimba ambazo zitafifisha ndoto zao.

“Tuliweza kumsaidia mwanafunzi mmoja wa kidato cha tatu ambaye wazazi wake walishachukua mahari kwa ajili ya kumuozesha, wanafunzi walituletea taarifa na tukazuia tukio hilo,” anasema.

Muelimishaji rika wa wanafunzi shuleni hapo, Ngaisari Kutandao, anasema kama wangepata elimu ya afya ya uzazi mapema suala la mimba shuleni hapo lingekuwa historia.

Meneja wa mradi huo, Dk. Aisha Byanaku, anasema wamebaini namna ambavyo umaskini unasababisha wasichana kutoka nje na kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi.

Makala haya yameandaliwa na Frolence Sanawa (Mtwara), Amina Omary (Tanga) na Upendo Mosha (Kilimanjaro).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,586FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles