25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

January atumbua vigogo NEMC

makambaNA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

MSIMAMIZI wa bomoabomoa  inayoendeshwa Dar es Salaam, Heche Suguta ambaye pia ni mwanasheria wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), amesimamishwa kazi.

Habari zinasema hatua hiyo imechukuliwa  na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira,  January Makamba.

Suguta ambaye ni wakili daraja la pili amesimamishwa kazi na wenzake wawili  kwa   kukiuka miiko ya kazi  katika kusimamia kiwanda cha kusindika minofu ya punda kilichopo   Dodoma.

Taarifa iliyotolewa  na Idara ya Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais jana ilieleza kuwa uamuzi huo umefikiwa  baada ya kikao kilichoitishwa juzi na waziri huyo   kuzungumzia njia za kuimarisha utendaji  ndani ya wa NEMC.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa  umekuwapo ukiukwaji wa makusudi  na wa wazi wa miiko ya kazi katika  kiwanda cha kusindika minofu ya punda uliofanywa na watumishi wa NEMC  walioshughulika na kiwanda hicho.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo,  Waziri ameagiza kusimamishwa kazi mara moja watendaji watatu wa baraza hilo.

Mbali na Suguta wengine waliosimamishwa ni Ofisa Mazingira Mwandamizi,  Dk. Eladius Makene   na Ofisa Mazingira,  Boniface   Kyaruzi.

“Waziri amewasimamisha kazi watumishi hawa wa Baraza   kwa  kukiuka miiko ya kazi  katika kusimamia kiwanda cha kusindika minofu ya punda   na kuagiza zichukuliwe  hatua nyingine za  nidhamu na  sheria,” ilieleza taarifa hiyo.

Alisema mbali na kusimamishwa   watumishi hao,  zitafuata hatua nyingine za  nidhamu na  sheria  kwa watendaji hao.

January pia  ameagiza  mamlaka husika kumpa barua ya onyo kali na la mwisho, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC,  Bonaventura Baya kwa udhaifu  katika usimamizi wa watumishi wa Baraza.

Barua hiyo ilitolewa baada ya kubainika kutakuwepo na usimamizi makini na thabiti kwa watumishi wa NEMC jambo linalosababisha malalamiko mengi kuhusu utendaji wa Baraza hilo.

“NEMC kama chombo muhimu nchini kilichopewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya  Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira inatarajiwa kazi zake zifanyike kwa ufanisi wa kiwango cha juu kulingana na majukumu yaliyoko kwenye sheria,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa  kwa upungufu unaojitokeza  January ameahidi kuunda jopo la wataalam wasiozidi watano ndani ya wiki moja  kutathmini utendaji wa NEMC na changamoto mbalimbali katika usimamizi wa hifadhi ya mazingira na kuishauri Serikali ipasavyo.

Alisema ndani ya wiki hiyo pia   litatolewa tangazo litakalokuwa na mambo mbalimbali ikiwamo anwani ya barua pepe, nukushi,namba ya simu, namba ya Whatsapp  ili mtu yeyote mwenye malalamiko au aliyewahi kuombwa rushwa chochote na watumishi  kinyume na  maadili ya kazi yao atoe taarifa mara moja na kufanyika uchunguzi.

January pia ameagiza kuitishwa  mkutano wa dharura wa bodi ya NEMC ndani ya wiki tatu    kufanya uamuzi juu ya changamoto za utendaji katika Baraza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles