24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 29, 2023

Contact us: [email protected]

Hujuma kubwa

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli,amefichua hujuma zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kodi kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wasio waaminifu wa Mamlaka ya MapatoTanzania (TRA).

Alifichua hujuma hizo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika kikao kilichowakutanisha viongozi wa TRA, mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa yote nchini pamoja na taasisi zinazohusika na udhibiti na ukusanyaji wa mapato.

Akizungumza katika kikao hicho, alisema wapo matajiri wawili wanaoingiza karibu mizigo yote inayouzwakwenye soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Alisema watu hao  wanaingiza makontena hadi 700 kwa mwaka. “Kila mtu anafahamu biashara inayofanyika Kariako, hao matajiri wawili ndio wanaoleta makontena mpaka 700 kwa mwaka na wale wanawaletea wengine pamoja na kwamba wana uwezo wa kuagiza na wana Tin Number wanawatumia hao baadaye wanakuwa wanatoa bidhaa kidogo kidogo wakati wana uwezo wa kuagiza hizo bidhaa wenyewe.

“Sasa nashangazwa kwamba ni kweli TRA, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, na wakuu wa wilaya hamjui haya? Sitaki kuwataja wale ambao ni super kuleta bidhaa leo mwingine anaishia neno ‘agency’ mwingine anaishia na neno ‘O’ huko mwishoni,”alisema.

Alisema anazo taarifa kuwa katika maeneo mbalimbali ya mipakani wapo wafanyabiashara wanapitisha bidhaa bila kulipa kodi na TRA, vyombo vya dola pamoja na waziri mwenye dhama wapo.

Alisema yupo mfanyabishara mmoja mkoani Mwanza (jina analo) anapitisha magari hadi 10 na anapopeleka bidhaa zake zinauzwa kwa bei ya chini kwa sababu hakulipia kodi.

“Mipaka yetu ni sehemu ya kupitisha bidhaa bila kulipishwa kodi mfano, Sirari kule Mara, Namanga na maeneo mengine wafanyabiasara wanaopitisha bidhaa zao bila kulipa kodi mimi ninayo majina yao na wanashirikiana na makamishna wa TRA.

“Mmoja pale Mwanza huwa anapitisha magari hata 10 na anapopeleka bidhaa zake zinauzwa kwa bei ya chini kwa sababu hakulipa kodi na wanashirikiana na maofisa wa TRA walioko katika mipaka hiyo inajulikana,”alisema.

Akizungumzia kuhusu kodi ya majengo, Rais Magufuli aliitaka TRA kuweka utaratibu rahisi wa kukusanya kodi ya majengo huku akielekeza nyumba ya kawaida iliyopo kijijini ilipiwe Sh 10,000 na ya ghorofa ilipiwe Sh 20,000.

“Kwa maeneo ya mjini, nyumba ya kawaida ilipiwe Sh 10,000, myumba ghorofa kila sakafu ilipiwe Sh 50,000 na kodi itozwe kwa kiwanja na si kila jengo lililopo katika kiwanja hicho.

“Unaweza kukuta mtu ana nyumba ndogo ya watoto wake na wakwe zake sasa kwa mtindo huo anajikuta anatozwa Sh 100,000 ndio maana Watanzania wengi wanakwepa kodi maana kuna watu wanakadiriwa kodi ya nyumba mpaka Sh milioni 2 mpaka 3.  

“Mfumo na taratibu zetu za ukusanyaji kodi bado kuna upungufu ukilinganisha na nchi zingine za Afrika. Tax base yetu ya makusanyo ni ndogo. Kwa hiyo mtaona kwamba kuna mahali tumeshindwa.

“Tumeshindwa kurasimisha sekta isiyo rasmi ambayo asilimia 60 hadi 70 kwa hiyo kwa sasa tunakusanya kwenye sekta rasmi tu ambayo kati ya asilimia 30 hadi 40. Hii ina maana kwamba kodi nyingi za nyumba maghala, hoteli zinapotea.

“Nchi yetu bado haijafanikiwa kutumia rasilimali zake kukusanya mapato. Hivyo Wizara ya Fedha na TRA haina budi kuzifanyia kazi hizi.

“Mianya ya ukwepaji kodi baadhi ya wafanyabiashara kwa kutumia udhaifu uliopo kwenye sheria zetu wameendelea kukwepa kodi …

“Ziko kampuni kila mwaka inatangaza kupata hasara ili isilipe kodi sasa TRA kwanini msifunge mtu anayepata hasara kila siku kwanini ukubali kupata ripoti ya kampuni ambayo inapata hasara kila mwaka?,”alihoji.

Pia alisema matumizi ya Mashine ya Kielektroniki (EFDs) bado haijaimarika kwani inasababisha upotevu mkubwa wa mapato.

AISHUKIA TRA

Aidha, Rais Magufuli alisema kuna matatizo ndani ya TRA, akisema kuna idadi ya watumishi wengi lakini tija haionekani na baadhi ya watendaji wazuri wanapigwa vita.

Alitaja udhaifu mwingine uliopo TRA kuwa ni pamoja mawasiliano hafifu kati ya viongozi wa juu na wafanyakazi wa chini, kupanga malengo bila kufanya utafiti.

Vile vile alisema wale wafanyabiashara ambao wana uhusiano mzuri na watumishi wa TRA ndio wanaoruhusiwa kuingiza EFDs kwa bei ya juu wakati zingenunuliwa kwa bei ya chini.

Pia alisema mameneja wa TRA wa wilaya na mikoa hawawajibiki kwenye majukumu yao ipasavyo.

“Baadhi ya wafanyakazi wa TRA wanawaomba rushwa wafanyabiashara wadogo au kuwabambikizia kodi kubwa hivyo kuwalazimu kufunga biashara zao na mwishoni kuifanya waichukie serikali yao.

“Mtu ana biashara kadogo tu lakini anaambiwa atoe milioni ambayo haiendani na kile anachokipata na mwishoni anafunga biashara sasa akishafunga biashara anayepata hasara ni nani? TRA mnakuwa mmepata faida au hasara baada ya biashara kufungwa?,”alihoji.

Rais Magufuli alisema bado Tanzania haifanyi vizuri kwenye makusanyo yasiyo ya kodi pamoja na kwamba makusanyo yameongezeka kutoka Sh bilioni 284 mwaka wa fedha 2010-11 hadi Sh trilioni 2.2 mpaka kufikia  2017/18.

Alisema kiwango hicho bado ni kidogo kwa sababu mashirika mengi hayapeleki gawio hivyo mamlaka zote za makusanyo yasiyo ya kodi ikiwemo halmashauri ziongeze bidii.

“Sambamba na matatizo hayo ya kodi mazingira ya kufanya biashara katika nchi yetu pia sio mazuri sana, tuna shida katika kuvutia wawekezaji huduma za usafirishaji, umeme utitiri wa taasisi za usimamizi unaoambataza na tozo.

Katika miaka ya karibuni serikali imejitahidi kuimarisha miundombinu ya usafiri na upatikanaji huduma ikwemo umeme na kesho kutwa tunakwenda kusaini mkataba wa Stigler’s.

“Hata hivyo kuna ucheleweshaji bandarini vizuizi barabarani vingine ni rasmi vingine si rasmi, mtu anajisikia tu gari liko kwenye transit anajisikia tu alisimamishe na anaweza kusimamishwa hapo hata kwa saa 6 au 7 bila kujali muda na baadaye anakuja kumwachia yule ni mfanyabiashara anakuwa discouraged na mara nyingi hiki kitu kinafanywa sana jeshi la polisi.

“Wafanyabiashara wanahangika sana kutoa mizigo bandarini inacheweshwa kwa makusudi na wawekezaji huchukua muda mrefu kupata vibali vya kuwekeza.

“Upo uhusiano wa karibu katika mifumo na kuimarika kwa mazingira ya biashara. Taratibu za kodi zikiwa rahisi na viwango vyake vikiwa chini watu watahamasika kuwekeza kufanya biashara na mapato yataongezeka lakini viwango vikiwa juu watu watashindwa kufanya biashara na baadaye mapato yatapungua.

“Nawaagiza TRA, hakikisheni mnatengeneza mazingira mazuri ya watu kulipa kodi, pitieni upya viwango vya kodi mnazotoza, mpanue wigo wa walipa kodi.

“Mtoe adhabu kwa wakwepa kodi lakini msiwaonee hiyo ni baada ya kuboresha viwango vya ulipaji kodi. Mkasimamie maadili ya kutoza kodi, msionee watu kwa sababu nchi inapoteza mapato mengi

“Inashangaza sana watu tuko milioni 55 halafu wanaolipa kodi ni milioni 2.2 ni aibu kubwa kwa taifa,”alisema.

Alisema kuna mchezo unafanywa na TRA wa kufunga maduka ya wafanyabiashara labda anamdai Sh bilioni 2 lakini akiambiwa apewe kwanza Sh bilioni 1 anakataa na kufunga duka.

“Mtu anakwambia akupe bilioni moja au milioni 800 unazikataa halafu unafunga duka badala ya kupokea ili uendelee kumdai, wewe unafunga na baadaye huyo mfanyabiashara anafunga na anaenda kuanzisha duka mpya tunashindwa kutumia busara zetu wakati mwingine,”alisema.

Akizungumzia kuhusu maduka ya kubadilishia fedha za kigeni alisema kuna wafanyabiashara walikuwa wakifanya biashara bila TRA kupata asilimia yoyote.

“Gavana hapa hakutaka kutoa details zote lakini siku alipovamia maduka; waliopewa leseni amepewa  mmoja lakini maduka zaidi ya 7 hayakuwa na connection na TRA. tunaibiwa tunaibiwa.

“Pale Arusha kuna meneja wa TRA kwanini alisubiri mpaka gavana aende? kwanini wasingeungana na Mkuu wa Mkoa haya yote ni kwa sababu kila mtu anajifanyizia kwake,”alisema.

Vitambulisho wajasiriamali

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alitoa vitambulisho vya wajasiriamali 670,000 kwa wakuu wa mikoa yote ya Tanzania huku kila mkuu wa mkoa akikabidhiwa vitambulisho 25,000 kwa ajili ya kuwagawia wajasiriamali.

Alisema wajasiriamali ambao watapewa vitambulisho hivyo ni wale ambao mtaji wao si zaidi ya Sh milioni 4.

Alisema wajasiriamali hao watavilipia Sh 20,000 kwa kila kitambulisho kimoja kwa mwaka ambayo ni bei ambayo imetengenezewa vitambulisho hivyo kwa kila moja.

Alisema wajasiriamali watakaopatiwa vitambulisho hivyo wasibughudhiwe wakati wanafanya biashara zao.

“Mfanyabiashara mdogo akivaa kitambulisho hiki asisumbuliwe na mtu yeyote na niseme kwa dhati ndugu zangu viongozi wa siasa mtu utakayemkuta na kitambulisho hiki na anafanya biashara ya chini ya milioni 4 usimsumbue.

Gavana

Naye Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Florens Luoga alisema wataendelea kudhibiti biashara ya ubadilishaji fedha ili kuhakikisha sekta ya fedha haiyumbi.

Aidha, alisema BoT ina akiba ya kutosha ya fedha za kigeni zinazoweza kutumika kwa kipindi cha miezi mitano.

Alisema hakuna haja ya kuwa na maduka mengi ya kubadilishia fedha na badala yake yatapatikana katika sehemu maalumu pekee ikiwemo hoteli za kitalii na benki.

“Pia nawaonya wafanyabiashara wanaobeba fedha kwenye mabegi wanaopenda kulipia bidhaa nje ya nchi akisema kufanya hivyo ni kuvunja sheria,”alisema Profesa Luoga.

Naye Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere alisema asilimia 80 ya wafanyabiashara wanaostahili kuwa mashine za EFDs wanazo na kwamba changamoto ni matumizi sahihi ya mashine hizo.

Alisema kuna wengine pamoja na kuwa na mashine hizo lakini hawatoei risiti huku wengine wakitoa yenye thamani ya fedha pungufu kuliko aliyolipa mteja na wengine wanatengeneza risiti za kughushi.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango alisema atasimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Rais Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,259FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles