23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

Hospitali Handeni haina huduma kwa watoto njiti

AMINA OMARI-HANDENI

HOSPITALI ya Wilaya ya Handeni   inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa chumba maalum cha uangalizi wa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) na kusababisha baadhi yao kufariki dunia.

Kauli hiyo ilitolewa na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Faisal Said alipozungumza MTANZANIA  jana.

Alisema hali hiyo imesababisha kuongezeka vifo vya watoto wachanga.

Alisema   huduma hiyo kwa sasa inapatikana katika Hospitali ya Rufaa   Bombo pekee ambayo ni umbali wa zaidi ya kilometa 150  kutoka wilaya hiyo.

  Mganga huyo aliwaomba wadau wa maendeleo kujitokeza kuchangia ujenzi wa chumba hicho  kusaidia kusogeza huduma hiyo karibu na kunusuru maisha ya watoto wachanga.

“Umbali wa huduma hiyo nao unachangia kwa kiasi kikubwa   mnapopata mtoto ambaye amezaliwa njiti, hivyo wakati mwingine anafia njia kabla ya kufikishwa Bombo,” alisema Dk. Faisal.

Muuguzi wa Wodi ya Wazazi Hospitalini hapo, Mwajuma Mvungi alisema kitengo cha huduma ya mama na mtoto licha ya kufanya vizuri kinakabiliwa na uhaba wa vifaa tiba.

Alisema hali hiyo inazorotesha utoaji wa huduma kwa sababu hospitali hiyo wakati mwingine hulazimika kupokea wajawazito kutoka   wilaya ya jirani ya Kilindi.

Baadhi ya wajawazito waliozungumza na MTANZANIA, Tahiya Ali alisema licha ya huduma nzuri zinazotolewa kuna ukosefu wa kipimo cha mapigo ya moyo ya mtoto kwa wajawazito.

 “Nilipoteza mimba ya mtoto wa tatu kwa ukosefu wa kifaa hicho kumbe mtoto alikufa mapema mpaka kujua ilikuwa imeshapita miezi miwili,” alibainisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles