Mohamed Kassara -Dar es salaam
KIUNGO mkabaji Himid Mao ameungana na Mtanzania mwenzake, Shiza Kichuya kuichezea klabu ya ENPPI, baada ya kujiunga nayo kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Petrojet iliyoshuka daraja.
Petrojet imeshuka daraja ikitoka Ligi Kuu Misri hadi Ligi Daraja la Kwanza, baada ya kumaliza nafasi ya 16, miongoni mwa timu 18, ikimaliza na pointi 35, baada ya kucheza michezo 34.
Timu nyingine zilizoshuka daraja ni El Dakhleya na Nogoom.
Himid ambaye ni nahodha msadizi wa kikosi cha Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’, alijiunga na Petrojet Juni mwaka jana akitokea Azam FC ya hapa nchini.
Himid ameungana na nyota mwenzake katika kikosi wa Stars, Kichuya ambaye anaichezea klabu hiyo kwa mkopo, akitokea klabu ya Pharco inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini humo.
Kichuya alijiunga na Pharco Februari mwaka huu akitokea Simba, kabla ya kutolewa kwa mkopo kwenda ENPPI, ambapo alianza kuichezea timu katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Al Alhly uliomalizika kwa kuchapwa mabao 2-1.