29.3 C
Dar es Salaam
Thursday, May 2, 2024

Contact us: [email protected]

Hemed Abdulla: Tutaendelea kuulinda Muungano kwa gharama yoyote

Nora Damian na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema Watanzania wanatakiwa kulinda Muungano kwa gharama yeyote na kuuimarisha kwa faida ya kizazi cha baadaye.

Amesema katika miaka 60 ya Muungano, Serikali zote mbili zimefanikiwa kusimamia utekelezaji wa masuala ya Muungano kwa ufanisi mkubwa na kuwezesha kuimarika kwa utaifa, umoja, amani, utulivu na hali ya maisha ya wananchi kutokana na ukuaji wa uchumi wa pande zote.

Ameyasema hayo leo Aprili 19, 2024 wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya Miaka 60 ya Muungano yanayofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

“Taasisi za Muungano zimekuwa na ufanisi katika kuhakikisha usawa wa utoaji huduma kwa wananchi wa pande zote mbili, zimefungua ofisi Tanzania Bara na Zanzibar. Hadi sasa taasisi 33 zimefungua ofisi Zanzibar kati ya taasisi 39 za Muungano hivyo, ni hatua kubwa katika kuimarisha huduma kwa wananchi wetu na kuimarisha Muungano,” amesema Abdulla.

Amesema kuwepo kwa Muungano kumesaidia kuimarisha hali za wananchi na kuinua uchumi wa pande zote mbili kutokana na kuwepo kwa soko la pamoja lisilokuwa na vikwazo vya kiutawala na kiuendeshaji.

Amesema hali hiyo imeongeza ushirikiano na utengamano unaorahisisha mtiririko wa rasilimali na bidhaa, mitaji, watu na huduma baina ya Tanzania Bara na Zanzibar na kwamba zipo fursa nyingi za kibiashara ambapo wafanyabiashara wadogo na wakubwa wanaweza kuwekeza pande zote za Muungano katika viwanda, hoteli na kujenga nyumba za biashara na makazi bila vikwazo.

Akizungumzia upande wa kijamii amesema mafanikio makubwa yamepatikana kwani huduma za kijamii zimeimarika hususani katika sekta ya afya, maji, elimu, ustawi na maendeleo ya jamii na makazi.

“Fursa za kijamii na utamaduni ni nyingi na zinazogusa mtu mmoja mmoja, vikundi na au taasisi, undugu wa damu umeimarika wananchi wa pande mbili za Muungano wameungana katika misingi ya ndoa na urafiki uliojengeka na kuimarika. Hali hii imechangia katika kupunguza migawanyiko ya kijamii na kuondoa hisia za ukabila na ubaguzi miongoni mwetu,” amesema.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Khamis, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeendelea kuchukua hatua za kutafutia ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa masuala ya Muungano.

Amesema maonesho hayo yanalenga kutoa elimu kwa makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi, wabunge, walimu na wengine ili kujua Muungano na fursa zilizopo.

Amesema kuanzia mwaka 2006 hadi 2024, hoja 25 zilipokelewa na kujadiliwa na kati ya hizo 22 zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano.

Amesema hoja zilizobaki zipo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi na kwa utashi na dhamira ya dhati ya pande zote mbili zitapatiwa ufumbuzi.

“Katika kipindi cha miaka mitatu, 2021 hadi 2024 hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi kati ya 18 zilizokuwepo. Utatuzi wa changamoto za Muungano umeongeza imani ya Watanzania kwa Serikali zetu na kuimarisha, kudumisha amani ya muda mrefu na utulivu wa Tanzania ambao ni Tunu muhimu na fahari ya nchi yetu,” amesema Khamis.

Kwa Upande wake Meneja Ukuzaji Biashara wa Mamlaka ya Maendeleo na Biashara (TANTRADE), Mohamed Tajin, amesema maonyesho hayo yataziwezesha taasisi kushiriki kwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya huduma wanazozitoa zikiwemo Uhamiaji, Benki Kuu, Zima Moto, RITA BRELA na zingine.

“Wanachi wajitokeze kwa wingi katika maonesho haya ili kupata elimu, historia ya muungano na watapata fursa ya kutoa maoni kuhusu Muungano,” amesema Tajin.

Mamlaka hiyo imewataka wananchi kutembelea katika banda lao ili kufahamu huduma wanazotoa ikiwemo ukuzaji biashara ndani na nje ya nchi kupitia maonesho yanayofanyika kila mwaka maarufu kama Sabasaba. Mwaka huu maonesho hayo yanatarajiwa kufanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 13.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles