HECHE ATAKIWA KUKUTANA NA MWIGULU

0
1390
MBUNGE wa Tarime Vijijini,  John Heche (Chadema)
        MBUNGE wa Tarime Vijijini,  John Heche                                              (Chadema)

NA KULWA MZEE-DODOMA 

MBUNGE wa Tarime Vijijini,  John Heche (Chadema) ametakiwa kuonana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba  wapate njia sahihi ya kutatua tatizo lililopo katika mgodi wa North Mara.

Ushauri huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu baada ya Heche kuomba mwongozo kuhusu vurugu zilizotokea katika mgodi huo siku tatu zilizopita.

“Mheshimiwa mwenyekiti, wananchi wameingia katika Mgodi wa North Mara kuzuia wezi lakini cha ajabu polisi wanatumia nguvu kubwa kuwapiga wananchi na kuwaumiza,”alisema Heche.

Akijibu Zungu alimuelekeza Heche kuonana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi apate njia sahihi ya kulitatua tatizo hilo.

Akichangia katika bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18, Mbunge wa Viti Maalum, Jacqueline Msongozi (CCM) alisema alichozungumza Heche anajikosha kwa sababu  kinachotokea katika mgodi wa North Mara ndicho alichokitaka na Rais Dk. John Magufuli hakusema wakafanye hayo waliyofanya.

“Hilo ni kosa Mheshimiwa Mwenyekiti, Heche aunganishwe kama mhalifu namba moja, alihamasisha humu ndani tumemsikia,”alisema.

Heche aliomba kutoa taarifa na aliporuhusiwa alisema mbunge huyo anatumia jina lake vibaya, Rais Magufuli alisema hadharani wananchi walimsikia na yeye aliwaambia wananchi wachukue hatua za kuzuia mwizi.

Juzi wananchi wa Tarime walivamia mgodi wa North Mara kwa siku mbili mfululizo hatua iliyoelezwa kuwa ni kupinga uonevu unaofanywa na wawekezaji hao kupitia Kampuni ya Acacia.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana juzi, wananchi walikwenda hadi kwenye mtambo wa kufua dhahabu na   kufanya uharibifu  kabla ya kudhibitiwa na polisi.

Inadaiwa wale ambao hawakuona majina yao kwenye malipo walichukuana na kuvamia   mtambo  wa kufua madini lakini polisi walifika na kuwatawanya kwa  mabomu ya machozi.

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM) akichangia bajeti hiyo alimpongeza Rais kwa kuzingatia kero za wananchi.

“Naomba kuchukua nafasi hii kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya hasa kwenye kusimamia rasilimali za nchi, ameonyesha mfano mzuri.

“Kwa mjadala unavyokwenda wengi wanamuunga mkono, wanaweza kupatikana wachache wanye mawazo tofauti lakini isitufanye tusisonge mbele.

“Ni vizuri ukweli huu ukasemwa, hizi juhudi za kulinda raslimali za nchi yetu hazikuanzia awamu ya tano, zilianza awamu ya kwanza, enzi za Mwalimu Nyerere.

“Yako mambo alifanya katika kuhakikisha raslimali zetu zinalindwa, awamu ya pili ya Rais Ally Hassan Mwinyi, awamu ya tatu, Rais Benjamin Mkapa, awamu ya nne Rais jakaya Kikwete yapo mambo mengi mazuri walifanya hata kama kulikuwa na upungufu.

“Hakuna namna ambayo tutapuuza juhudi za watangulizi wa Rais Magufuli sababu nao wana mchango, kwa nafasi yao walitimiza wajibu wao ni vizuri tutambue michango yao badala ya kubaki tunawaonyooshea vidole kama vile hawakufanya kitu katika juhudi za kulinda raslimali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here