24.8 C
Dar es Salaam
Friday, June 2, 2023

Contact us: [email protected]

HATIMA YA KINA MBOWE KUJULIKANA LEO

NA KULWA MZEE  – DAR ES SALAAM


HATIMA ya viongozi wa Chadema, akiwamo Mwenyekiti Freeman Mbowe na wenzake watano itajulikana leo kama watafanikiwa kufikishwa mahakamani na kutimiza masharti ya dhamana ama la.

Viongozi hao ambao walipelekwa katika Gereza la Segerea, Dar es Salaam tangu Machi 25, walikwama kupata dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa sababu mbalimbali.

Mbowe na wenzake wanatarajiwa kufikishwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri.

Machi 25 mwaka huu kina Mbowe walifikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka manane yakiwamo ya uchochezi na uasi, kisha Jamhuri ikiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi walipinga wasipewe dhamana kwa madai wakitoka watakwenda kuyatekeleza yale waliyosema Februari 16, mwaka huu.

Pia Wakili Nchimbi alidai washatakiwa hao wakitoka nje kwa dhamana itakuwa hatari kwa usalama wa nchi.

Hata hivyo, madai hayo yalipingwa na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, kwa madai kwamba hayana msingi na hakuna ushahidi washtakiwa wakitoka watahatarisha usalama wa nchi na watatekeleza yale waliyosema Februari 16, mwaka huu.

Baada ya majibizano hayo ya kisheria, mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Machi 28, mwaka huu kwa uamuzi wa dhamana na kina Mbowe walienda kulala rumande hadi tarehe hiyo.

Machi 28 mwaka huu wafuasi wa Chadema walifurika mahakamani kusikiliza uamuzi wa viongozi wao kuhusu kupata ama kukosa dhamana.

Katika hali ambayo ilizua taharuki, viongozi hao hawakuletwa mahakamani kwa madai kwamba gari la kuwaleta mahabusu kutoka Segerea liliharibika.

Hata hivyo, mahakama iliamua kutoa uamuzi wa kuwapa dhamana bila wenyewe kuwapo kwa masharti kwamba wawe na wadhamini wawili kila mmoja, wenye barua na vitambulisho, wasaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni 20 na washtakiwa wanatakiwa kuripoti polisi kila siku ya Alhamisi.

Wakati wa kesi hiyo inayoonekana kuwa na mvutano wa kisheria, iliwalazimua polisi kuimarisha ulinzi siku washtakiwa hao walipofikishwa mahakamani hapo.

Askari wengi walifika kuimarisha ulinzi katika mahakama hiyo tangu alfajiri, huku kila aliyetaka kuingia katika mahakama hiyo alihojiwa na kuruhusiwa kuingia, huku wengine walizuiwa.

Wananchi waliozuiwa nje ya lango kuu la mahakama, walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali wakionyesha kuwa wana imani na Mbowe, Msigwa, Mnyika na viongozi wengine waliopo gerezani.

Wafuasi wa Chadema na viongozi wengine wa juu wakiwamo mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na wabunge wa chama hicho, walifika mahakamani hapo kusikiliza uamuzi wa dhamana.

MAWAKILI WA SERIKALI

Akiiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, alidai washtakiwa hawapo mahakamani na katika kufuatilia kwa uongozi wa Magereza Segerea na kwa Inspekta Shabani taarifa iliyopatikana ni kwamba mahabusu wote kutoka katika gereza hilo hawakufika mahakamani.

Akitoa maelezo mahakamani, Inspekta Shabani alidai alipata taarifa kwa msaidizi wa mkuu wa gereza kwamba gari lililowabeba washtakiwa lilipotoka gerezani likaharibika, hivyo hakuna mahabusu kutoka Segerea.

“Gari mpaka muda huu halijatengamaa, uwezekano wa kuwaleta mahabusu umeshindikana,” alidai Inspekta Shabani.

Hakimu Mashauri alisema kutokana na hoja hizo, mahakama itatoa uamuzi wa dhamana bila ya washtakiwa kuwapo.

Akitoa uamuzi alisema haibishaniwi kwamba mashtaka dhidi ya washtakiwa yanadhaminika na hakuna ushahidi wa madai ya Serikali kwamba wakidhaminiwa watakwenda kutekeleza yale waliyozungumza Februari 16, mwaka huu.

“Mahakama imepitia hoja za pande zote mbili, baada ya kufikiria yote, ili mahakama ionekane inatenda haki itoe dhamana kwa washtakiwa sababu ni haki yao kikatiba.

“Nakubaliana na hoja ya Wakili Peter Kibatala kwamba maelezo ya hati ya mashtaka si sababu tosha ya kuzuia dhamana kwa washtakiwa, hivyo mahakama inakubali maombi ya dhamana na kutupilia mbali pingamizi lililowasilishwa na Jamhuri,” alisema Hakimu Mashauri.

Hakimu Mashauri alisema upande ambao haujaridhishwa na uamuzi huo wanayo haki ya kukata rufaa ndani ya siku 30.

Jamhuri iliwakilishwa na mawakili wa Serikali, Dk. Zainabu Mango, Nchimbi, Wankyo Simon na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita, huku upande wa utetezi uliwakilishwa na Kibatala na Hekima Mwesigwa.

Washtakiwa ni Mbowe, Katibu Mkuu wa chama hicho, Vicent Mashinji, Salum Mwalimu, Peter Msigwa, John Mnyika na Ester Matiko.

MASHTAKA

Washtakiwa wote wanadaiwa kufanya mkusanyiko au maandamano yasiyo halali, kuendelea na mkusanyiko usio halali wenye vurugu baada ya kutolewa tamko la wao kutawanyika.

Mbowe peke yake alisomewa mashtaka ya kuhamasisha chuki miongoni mwa wanajamii isivyo halali, uchochezi na kusababisha chuki miongoni mwa wanajamii, uchochezi wa uasi na ushawishi utendekaji wa kosa. Msigwa alisomewa shtaka la kushawishi raia kutenda kosa.

Nchimbi alidai washtakiwa wote Februari 16, mwaka huu, wakiwa katika Barabara ya Kawawa, Kinondoni Mkwajuni, Dar es Salaam, kwa pamoja wakiwa wamekusanyika kutekeleza lengo la pamoja kinyume cha sheria, waliendelea na mkusanyiko katika namna iliyowafanya watu waliokuwa kwenye eneo hilo waogope watakwenda kwenye uvunjifu wa amani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,264FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles