25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 11, 2024

Contact us: [email protected]

HAMKANI SI SHWARI KWA RAIS GNASSINGBÉ NCHINI TOGO

KIMEWAKA! Ndivyo ilivyo hali ya sasa nchini Togo ambako vurumai zimetamalaki mamia ya waandamanaji wakiingia mitaani kuchagiza ukomo wa Rais kukaa madarakani, wakikerwa na Rais Faure Gnassingbé aliyeko madarakani tangu mwaka 2005 akirithi utawala kutoka kwa baba yake Hayati Rais Eyadema ambaye aliingia madarakani kwa Mapinduzi ya kijeshi miaka 50 iliyopita miaka saba baada ya Taifa hilo kujipatia uhuru.

 

Ilianza kama njiti ya kiberiti takribani miezi miwili iliyopita lakini sasa kimewasha moto nchi nzima maandamano yakiongezeka ambapo juma lililopita watu takribani 800,000  walishiriki, walianza kwa amani lakini kadiri wanavyoendelea vurugu zinaongezeka na kusababisha mauaji  kama ilivyotokea sku chache zilizopita mtoto mwenye umri wa miaka 10 alipouawa kwa risasi na vikosi vya kutuliza ghasia, huku watu wengine 70 wakijeruhiwa katika Mji wa Bafilo Kaskazini mwa Mji Mkuu wa Lomé ambako kazi zimesimama vikosi vya ulinzi vikirandaranda mitaani. Taifa hilo limejaribu kutanzua mkanganyiko huo bila mafanikio kutokana na mvutano baina ya Serikali na wapinzani.

 

Uhasama unafukuta miongoni mwa wananchi kwa uchomaji nyumba za wanaohisiwa kuwa wafuasi wanaoiunga mkono Serikali, lakini hilo haliwastui vinara wa upinzani akiwamo Jean Pierre Fabre wanaozidi kuwachagiza wafuasi wao kuandamana.

 

Mfupa wa sakata zima ni kushindwa kukubaliana kuhusu ukomo wa muda wa Rais madarakani licha ya Serikali kuwasilisha Muswada bungeni juma lililopita wa kuweka ukomo wa kutawala na kupigiwa kura ya kupitishwa, ili kuwa na vipindi visivyozidi viwili madarakani kama kura ya maoni itaridhia kabla ya uchaguzi wa mwaka 2020 lakini wapinzani hawakubaliani na kupitishwa muswada huo wakiituhumu Serikali kujikosha ili ionekane inataka mabadiliko yanayodaiwa na wananchi.

 

Wapinzani wanadai kuwa ni changa la macho litakalomuwezesha Rais Gnassingbé kusalia madarakani hadi mwaka 2030, wanataka ajiuzulu na asigombee mwaka 2020 kwa kuwa tayari ameshakaa madarakani kwa mihula mitatu tangu mwaka 2005 na kuchaguliwa tena mwaka 2010 na 2015. Upinzani unataka kipengele cha Katiba ya mwaka 1992 kinachobainisha mihula ya ukomo kutozidi miwili kifufuliwe, si wapinzani tu lakini hata viongozi wa kiimani nao wamejitosa katika songombingo linaloendelea nchini humo, kwa maaskofu kupitia umoja wao kudai Katiba iheshimiwe na kutaka kuhitimishwa kwa ‘Ufalme hodhi’ wa familia ya Gnassingbé uliodumu madarakani kwa nusu karne.

 

Lakini hii si mara ya kwanza kwa mkanganyiko unaofukuta hamkani ya mauaji kutokea nchini humo, mwaka 2005 watu takribani 500 waliuawa katika maandamano ya upinzani, kinachosababisha fukuto zaidi ni mgawanyiko wa pande mbili katika Taifa hilo ambapo Kusini kwenye mashiko ya upinzani kunavutana na Kaskazini ambako ndipo inakotokea familia ya Gnassingbé  inayoungwa mkono zaidi na jamii zinazoishi upande huo, ingawaje taratibu kadiri miaka inavyopita Kaskazini nako wameanza kuichoka familia hiyo ya watawala kutokana na maandamano mapya ya hivi karibuni kuhusisha wakazi wa miji iliyoko upande huo ya Dapaong na Mango.

 

Mwamko wa upinzani unashika kasi Kaskazini kutokana na kuibuka kwa wanasiasa wanaoipinga Serikali akiwamo Kiongozi wa chama cha National Panafrican Party (PNP), Tilpi Atchadam anayeshutumiwa na wanaoiunga mkono Serikali kwamba anatumia uhafidhina wa Kiislamu japokuwa shutuma hizo hazina mashiko. Serikali kwa upande wake imepagawa ikitapatapa kujaribu kuzuia upinzani kuungana pamoja kwa kupeana taarifa na kufikia hatua ya kuzima mitandao ya kijamii ambayo inatumiwa zaidi na wananchi kupashana taarifa za mikusanyiko ya maandamano.

 

Togo iliyojipatia uhuru kutoka kwa Wafaransa kwa miaka mingi haina sifa nzuri kuhusiana na haki za binadamu, lakini pia inachechemea kiuchumi kutokana na umaskini kwa kutegemea misaada ya wafadhili licha ya uzalishaji mkubwa wa madini ya phosphate yanayotumika kuzalisha mchanganyiko wa viatilifu na mbolea.

 

Shutuma nyingine ni kuwa kichaka cha majangili wa ghafi za wanyama zilizoharamishwa duniani yakiwamo meno ya tembo, wakiitumia nchi hiyo kujipenyeza kwenye nchi inazopakana nayo na kusafirisha ghafi hiyo katika nchi za Bara la Asia, kutokana na kutokuwa na utangamano kwenye Taifa hilo lililotawaliwa na familia moja kwa takribani miaka 50 kati ya 57 tangu lilipojinyakulia uhuru. Baba wa Rais wa sasa alitawala kwa miaka 38 lakini hata mabadiliko ya Katiba kuhusu ukomo wa mihula ya kutawala yakipita yataanza kutumika baada ya chaguzi za mwaka 2020 na 2025, hivyo kutoa fursa kwa Rais Faure kusalia madarakani jambo ambalo wapinzani hawataki kulisikia.

 

Togo ndiyo nchi pekee katika eneo hilo ambayo haina ukomo wa muda wa kutawala huku majirani zake zikiwamo Gambia na Burkina Faso zililazimika kukubali ukomo baada ya vurugu kuzifungasha virago Serikali zilizong’ang’ania madaraka. Baba wa Rais wa sasa Hayati Gnassingbé Eyadéma aliyefariki dunia Februari 5, 2005 aliyewahi kupindua Serikali mara mbili mwaka 1963 na 1967, ndiye mwasisi wa chama cha RTP (Rally Of Togolese People) kilichoongoza wakati wa utawala wa chama kimoja, licha ya kushutumiwa kwa utawala wa mabavu lakini alishinda katika chaguzi za vyama vingi za mwaka 1993,1998 na 2003.

 

Mwisho…..

 

 

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles