25.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

HALI MBAYA WAZAZI WA WATOTO WALIOTEKWA

Na JANETH MUSHI-ARUSHA

WAZAZI wa watoto wawili waliotekwa na watu wasiojulikana katika eneo la Olerian, Kata ya Olasiti, jijini hapa, wamesema hawana amani.

Wakizungumza na MTANZANIA jana kwa nyakati tofauti, wazazi hao walisema tangu Agosti 21 mwaka huu, watoto wao walipotekwa, hawali chakula wala kunywa maji kwa amani kwa sababu hawana uhakika na usalama wa watoto wao.

Watoto hao Maurine David (6), ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi, Lucky Vincent, aliyetekwa tangu Agosti 21, mwaka huu na Ikram Salim (3), aliyetekwa tangu Agosti 25, mwaka huu.

Katika mazungumzo yake, babu yake Ikram aliyejitambulisha kwa jina la Kassim Hassan, alisema tangu mjukuu wake atekwe, familia imekuwa na hali mbaya.

“Tuna hali mbaya sana kwa sababu wazazi hawali chakula na hata kulala tunalala kwa shida kutokana na mawazo tuliyonayo.

“Nakueleza ukweli, chakula mpaka uwalazimishe kwani watu hawali, wameshaanza kudhoofika, hali ni mbaya kwa ujumla kwa sababu kila mmoja ana masikitiko tu.

“Tunajitahidi sana kuwaliwaza wazazi, lakini hawaelewi kitu na hata kazini hawawezi kwenda, saa zote wako nyumbani.

“Hadi sasa hatujapata taarifa za msingi kutoka polisi kwa sababu kila tukiwauliza, wanasema wanapambana, tuendelee kusubiri.

“Kwa hiyo, kesho (leo), nimepanga kwenda kwa RPC nimsikie mwenyewe ili nijue wamefikia wapi maana muda umekuwa mrefu mtoto wetu  hajapatikana,” alisema babu huyo.

Kwa upande wake, baba mzazi wa Maurine, David Njau, alisema kwa sasa haelewi anaelekea wapi au anatoka wapi kwa sababu kichwa chake hakifanyi kazi tangu mtoto wake atekwe, Agoti 21, mwaka huu.

“Kwa kweli siko vizuri kwa sababu sina taarifa yoyote ya kupatikana kwa mwanangu. Kwa sasa nipo nipo tu, nasikitika na sijui naelekea wapi au natoka wapi.

“Japokuwa tunafarijiwa na ndugu, tunakula kwa shida na wakati mwingine tunaangalia chakula na hatuelewi tukifanyeje.

“Tukiwauliza polisi, wanasema wanashughurikia, kwa hiyo tupo tupo tu ili mradi kunakucha,” alisema mzazi huyo.

Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema hadi sasa wanawashikilia watu watatu wanaodaiwa kuhusika na matukio hayo ya utekaji wa watoto.

Pia, aliwataka wananchi kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za mitaa jijini hapa, kuwa walinzi katika maeneo yao ili kuepusha matukio kama hayo yanayojenga hofu kwenye jamii.

“Wananchi wote kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za mitaa, washirikiane ili tuweze kudhibiti matukio haya kwani hadi sasa tumewakamata watu watatu ila siwezi kutaja majina yao kwa sababu za kiupelelezi.

“Lakini pia, wazazi tuwe makini na watoto wetu, tusiwaache wacheze muda mrefu kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha madhara kwao,” alisema Kamanda Mkumbo.

Aliwataka pia wajumbe wa Serikali za Mitaa, kufahamu familia zinazoishi katika maeneo yao ili iwe rahisi kugundua watu wabaya na kuwachukulia hatua.

Taarifa za kutekwa kwa watoto hao, zilitolewa mwanzoni mwa wiki hii na  Mwenyekiti wa Mtaa wa Olkereyani, Kata ya Olasiti, Daudi Safari, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Mbali na Maureen na Ikram, watoto wengine waliotekwa na kupatikana ni Ayub Fred (3) na Bakari Selemani (3), wakazi wa Mtaa wa FFU, Kata ya Muriet, jijini hapa.

Katika matukio hayo, watekaji walikuwa wakiwaomba wazazi wawatumie Sh milioni 4.5 ili wawaachie watoto wao, jambo ambalo lilizidi kuwapa hofu wazazi hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles